Hizi ndizo Derby tano kali duniani

Muktasari:

  • Mwaka 1971 mashabiki 66 wa Rangers walifariki uwanjani, baada ya kuangukiwa na ukuta muda mfupi timu yao ilipopata bao la kusawa-zisha dakika ya 89 dhidi ya Celtic katika mchezo wa Ligi Kuu Scotland

Mpira wa bongo Simba na Yanga zinapokutana utasikia mashabiki wa klabu hizo kongwe nchini wavyopigana vijembe na tambo za hapa na pale, lakini yote hiyo ‘tisa’, kuna derby tano kali zinazotikisa dunia.

Iko hivi. Ilimuhitaji askari mmoja kufanyiwa upasuaji wa jicho, baada ya mlipuko wa bomu kutokea ilipopigwa mechi ya kibabe kati ya wapinzani wakubwa wa soka nchini Bulgaria baina ya CSKA dhidi ya Levski Sofia.

Zaidi ya mashabiki 20 wa Levski Sofia walikamatwa April 18, mwaka huu baada ya mlipuko wa bomu kudaiwa kutokea upande wa mashabiki wa klabu hiyo.

Licha ya matukio ya kihalifu yanayosababishwa na vurugu kwenye viwanja vya soka, Bulgaria siyo nchi pekee yenye klabu zenye upinzani mkali ambazo zinaibua hisia za mashabiki wa soka. Zifuatazo ndiyo derby tano kali duniani.

Boca Juniors vs River Plate

Inawezekana Boca Juniors na River Plate zinazotoka Argentina ndizo zinatengeneza derby maarufu zaidi duniani kutokana na uhasama wa klabu hizo.

Miamba hii ya soka imekuwa na uhasama ambao mara kwa mara umekuwa ukisababisha maisha ya watu kuwa hatarini zinapocheza.

Itakumbukwa hivi karibuni, mechi ya fainali ya watani hao wa jadi imeshindwa kufanyika mara mbili baada ya kutokea vurugu kubwa katika mji wa Buenos Aires.

Mashabiki wa River Plate walirusha mawe katika msafara wa wachezaji wa Boca Juniors walipokuwa wakitoka hotelini kwenda uwanjani.

Miongoni mwa wachezaji wa Boca Juniors waliojeruhiwa ni mshambuliaji nyota wa zamani wa Manchester United, Manchester City na Juventus, Carlos Tevez.

Vurugu hizo zimeufanya mchezo huo wa pili wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Amerika Kusini, kuhamishwa nchini humo na kupelekwa Hispania.

Celtic vs Rangers (Scotland)

Hizi ndizo klabu kubwa Scotland na zote zinatoka katika mji mmoja wa Glasgow. Mechi inayokutanisha timu hizi inaitwa Old Firm.

Upinzani wa klabu hizi umechangiwa na mgawanyiko wa dini ambao umekuwa ukileta ‘zahma’ tangu enzi hizo na mara kwa mara damu humwagika miamba hiyo inapokutana katika mechi ya aina yoyote.

Utamaduni wa Rangers umechagizwa na uprotestanti na Celtic kama lilivyo jina lao wanapata msaada mkubwa kutoka kwa wakatoliki ambao wengi wao ni wavamizi kutoka visiwa vya Ireland (Wairish).

Hisia za mashabiki wa klabu hizo kutokana na imani zao, zimechangia kuingia hadi ndani ya uwanja timu hizo zinapocheza hatua inayosababisha vurugu miamba hiyo inapocheza.

Mwaka 2001 saa chache baada ya Celtic kuibuka na ushindi wa mabao 6-2, shabiki wa klabu hiyo, Gary Rodgers alijikuta akipokea kifungo cha maisha baada ya kumchoma kisu na kumuua mwenzake wa Rangers, James Hardie.

Rodgers alikimbia eneo la tukio na kuacha kofia ya mchezo wa ‘baseball’ ikiwa katikati ya bustani ya damu iliyomwagika baada ya kutekelezwa kwa tukio hilo.

Tukio jingine lilitokea mwaka 1995, Mark Scott alichomwa na kitu chenye ncha kali na kufa baada ya kukatiza karibu na baa iliyojaa mashabiki wa Rangers akiwa amevaa nguo yenye rangi ya Celtic.

Derby ya Old Firm ni moja kati ya mechi iliyowahi kusababisha majanga makubwa uwanjani katika historia ya Uingereza.

Januari 1971 maelfu ya mashabiki wa Rangers walipoanza kutoka kwenye Uwanja wa Ibrox baada ya Jimmy Johnstone kuipatia bao Celtic dakika 89, lakini sekunde chache tu Colin Stein alifunga bao la kusawazisha kwa Rangers.

Kuingia kwa bao hilo kulisababisha mashabiki wa Rangers kurejea uwanjani na wengine walisimama pembeni ya ukuta ambao ulidondoka na watu 66 walifariki katika ajali hiyo mbaya.

Fenerbahçe vs Galatasaray (Uturuki)

Mji mkubwa wa Uturuki ni Instanbul unaopambwa na klabu kubwa tatu Besiktas, Fenerbahce na Galatasaray.

Mechi kati ya yeyote hapo huchukuliwa kama ya ushindani, lakini hali inakuwa tofauti sana zinapocheza Fenerbahce na Galatasaray.

Derby hii hufahamika zaidi ‘Intercontinental Derby’ kutokana na Fenerbahce kutokea upande wa Asia Bosphorus huku Galatasaray ikiwa upande wa Ulaya.

Mpaka mwaka 2011 uwanja wa nyumbani wa Galatasaray ulijulikana kama Ali Sami Yen ukiwa na jina la utani kuzimu. Bango la uwanja huo linasomeka “Karibu Kuzimu”.

Mechi ya kwanza baina ya miamba hiyo ilipigwa mwaka 1909, lakini ilipata umaarufu baada ya kupigwa mchezo wa kibabe 1934.

Moja kati ya vurugu kubwa iliyowahi kutokea ilikuwa mwaka 2013 wakati Fenerbahce iliposhinda 2-1 dhidi ya Galatasaray.

Vurugu zilianza baada ya mechi kumalizika na Burak Yildirim mwenye umri wa 19, alichomwa kisu na mashabiki wa Galatasaray na kufariki.

Olympiacos vs Panathinaikos (Ugiriki)

Mwambao wa bahari ya Aegean hisia ni kali nchini Ugiriki miamba miwili Olympiacos Piraeus na Panathinaikos zinazotoka mji mkuu wa Ugiriki, Athens zinapovaana.

Ugiriki siyo miongoni mwa nchi ambayo ina mchanganyiko wa watu, hivyo derby yao hujulikana kama mechi ya mahasimu wa ndani.

Shabiki wa Olympiacos, Nikos Papandopoulos anasema mgawanyiko ulitokana na madaraja, Olimpiacos walitokana wafanyakazi wa Bandari wa Piraeus na Panathinaikos wakiwa ni wafanyakazi wa daraja la kati.

“Lakini kutokana na kufahamika kwake Olympiacos ilitokea kuwa timu yenye nguvu kubwa ina zaidi ya asilimia 50 ya mashabiki wote wa Ugiriki,” anasema Papandopoulos.

Anasema timu nyingi Ugiriki zimekuwa zikipigwa faini au kupokwa pointi na mamlaka husika na wakati mwingine hata kutowaruhusu mashabiki wageni kuingia kwenye Uwanja wa Panathinaikos.

“Hivi sasa kila Serikali inayoingia madarakani inawatukuza mashabiki wa Panathinaikos kwa kuwa ndiyo wapigakura wao,”anaongeza.

PSV vs Ajax Amsterdam

Uhasama wa PSV na Ajax ni mkubwa Uholanzi, miamba hiyo pindi inapokutana katika mchezo wao unaofahamika kama De Topper mji unaochezwa mechi hiyo unazizima.

Matukio ya kukamatwa kwa mashabiki wa klabu hizo na kuwekwa rumande ni matukiko ya kawaida. Mechi hii ya watani wa jadi mara nyingi imekuwa ikitia doa taswira ya mchezo wa soka nchini Uholanzi.