JPM kaona mbali suala la uzazi wa mpango

Wakati mwingine tunashindwa kumuelewa Rais wetu John Magufuli. Pengine kutokana na wasaidizi wake kutotoa ufafanuzi wa kina pale anapotoa maelekezo, mapendekezo au amri.

Napata msukumo wa kuandika makala haya, kufuatia kauli iliyotolewa na Rais kuhusu uzazi wa mpango Tanzania.

Naamini Rais hakutoa tamko hili kiushabiki. Alimaanisha hasa kutokana na misingi ya sheria za asili, kizazi cha kabila lolote, jamiii au Taifa ili kiendelee na kuongezeka, (kisitoweke), kiwango cha wanawake kuzaa kisiwe chini ya 2.11.( kutokana na kanuni za kiafya, 2.11 inamaanisha watoto wawili kwa kila mwanamke mmoja)

Endapo kiwango hiki kitashuka hadi 1.99 kwa kipindi cha miaka 30, kurudi katika hali yake itachukua miaka 80 au 100.

Mifano ni mingi, Wajerumani waliozoea kujidai wao ndio Wazungu asilia, sasa wanazidi kutoweka. Tangu mwaka 2007 kiwango cha kuzaana Ujerumani ‘fertility rate’ kilikuwa ni 1.3 kwa jamii ya Wajerumani wenyewe tu. Ukichanganya na wahamiaji ndio kinafika 1.5, Ufaransa, 1.8 Uingereza 1.6 Ugiriki 1.3 Italia 1.2 Hispania 1.1 na nchi za Umoja wa Ulaya kwa ujumla wao fertility rate yao ni 1.38. Watu wa asili wa mataifa haya lazima wanatoweka.

Hata nafuu ndogo iliyopo inatokana na wahamiaji kutoka mataifa mengine. asilimia 90 ya Ongezeko la watu katika nchi za Umoja wa Ulaya tangu mwaka 1990 ni kutoka nchi za Kiarabu na asilimia 10 kutoka Afrika.

Inakadiriwa, asilimia 30 ya Wafaransa wenye umri wa miaka 30 na kushuka ni wahamiaji. Hadi mwaka 2027 mtu mmoja kati ya Wafaransa watano atakuwa ni mhamiaji.

Hii haikuanza ghafla. Walianza kuona kuzaa ni mzigo, kujinyima starehe. wakisahau bila ya wazazi wao kuamua wao kuwazaa wasingelikuwepo. Waliathiriwa na mifumo yao ya maisha kama ushoga. Hawazai. Wanaishia kuasili ‘adopt’ watoto. Baadhi wamewafanya mbwa, paka kuwa watoto au wapenzi wao. Mpaka huwarithisha mali zao. Angalau Afrika hatujaathiriwa sana na hali hii. Wameharibu kwao wanataka kuharibu na kwetu.

Kauli ya Rais haionekani kuwa ya bahati mbaya, “Wanawake sasa wanaweza kuacha kutumia dawa za kupanga uzazi, Ukiwa na chakula cha kutosha zaa.” Na pengine akitumia neno “fyatueni tu na Serikali itawasomesha …wale ambao hawafanyi kazi, wavivu ndio wanajipangia watoto”.

Alifahamu Watanzania milioni 23 kati ya 54 ndio wanaoishi kwa kipato cha chini ya dola mbili kwa siku na kuwa ongezeko la watu nchini ni milioni 1.6 kwa mwaka.

Anaona Taifa lina hitaji ongezeko la watu. Na sio kutoa tena pesa kuhamasisha watu wasizae. maana bajeti ya 2018/19 Serikali ilitenga Sh22 bilioni kwa ajili hiyo na ndio maana akazuia, matangazo ya aina hiyo.

Dhima ya Rais wetu ni Tanzania yenye viwanda. Taifa likiisha kuwa na mkakati kama huu lazima ukinzane na ‘wakubwa’, maana wanaamini chanzo cha uharibifu wa mazingira ya dunia yetu ni ongezeko la watu na maendeleo ya viwanda. Hakuna jinsi. Unataka uchumi viwanda lazima, vivyo hivyo ongezeko la watu.

Je, Tanzania tunaogopa ongezeko la watu, au kwa sababu ya mtizamo wa ‘wakubwa’? Hata tukiangalia msongamano wa watu nchini ‘density’ bado tupo vizuri, ni watu 57 kwa kila kilomita mbili. Wenzetu Kenya ni watu kwa kila 79 kilomita mbili, Uganda kwa kila 165 kilomita mbili. Mbona Rwanda wamefikia watu 440 kwa kila kilomita mbili wakati fertility rate yao ni 4.0? Ona uchumi na maendeleo yao. wanafanya vizuri.

Uganda ambao fertility rate yao ni 5.59 hali ya msongamano wao ni 165.5 pia wanafanya vizuri kiuchumi.

Angalia mfano wa Taifa la Israel ambalo lina maendeleo ya hali ya juu, kielimu kiteknolojia na kiuchumi. Huwaambii hii habari ya zaa watoto wawili. Ni taifa dogo sana, hali ya (density) ni 401 kwa kila kilomita mbili wakati kiwango cha uzazi ‘birthrate’ yao ni 3.11 wanajua thamani ya kuwa na watu.

Hata ukiangalia orodha ya nchi zenye idadi kubwa ya msongamano wa watu ikilinganishwa na eneo la ardhi waliyonayo sisi ni wa 146 namba tatu ni Singapore ambayo ni 3,188 kwa kila kilomita mbili. Na bado uchumi wao upo juu. Kumbe density sio sababu ya uchumi duni.

Dhima ya Rais wetu ni Tanzania yenye viwanda. Taifa likiisha kuwa na mkakati kama huu lazima ukinzane na ‘wakubwa’, maana wanaamini chanzo cha uharibifu wa mazingira ya dunia yetu ni ongezeko la watu na maendeleo ya viwanda. Hakuna jinsi. Unataka uchumi viwanda lazima, vivyo hivyo ongezeko la watu.