Je, unajua migogoro kwenye mahusiano ina madhara makubwa kiafya?

Sunday September 16 2018Dk Christopher  Peterson

Dk Christopher  Peterson 

Nilikutana na swali hili wiki iliyopita kutoka kwa Janeth mmoja wa wasomaji wa safu hii likisema, “Samahani daktari, niliingia kwenye mgogoro wa kimapenzi na kusababisha uhusiano wetu kuvunjika, baada ya kugundua ana mahusiano na mtu mwanamke mwingine nilipozikuta jumbe mbalimbali za kimapenzi walizokuwa wanatumiana kwenye simu yake. Lakini tangu hapo afya yangu imezidi kutetereka, naomba kujua kuna uhusiano wowote wa jambo hili na matatizo ya kiafya”?

Ni dhahiri kuwa kitendo cha kukuta ujumbe wa kimapenzi kwa mpenzi wako ambao unatoka kwa mtu mwingine tofauti na wewe kinaumiza sana. Hiyo ni ishara tosha kuwa kwenye mahusiano hayo hakuna uaminifu wowote na hii ndio moja ya sababu kubwa inayoongoza kusababisha kuvunjika kwa mahusiano mengi hasa siku za karibuni.

Wengi wamekuwa waathirika wakubwa wa jambo hili, kwani madhara yake sio tu kuvunjika kwa mahusiano lakini pia kusababisha matatizo kadha wa kadha ya kiafya ambayo huenda wengi hawalijui hili.

Ni vyema ikaeleweka kuwa suala hili lina matatizo zaidi ya kiafya kuliko hata kuvunjika kwa mahusiano yenyewe, na tafiti zinaonesha kuwa wanawake ndio waathirika zaidi wa madhara haya ya kiafya kuliko wanaume.

Kwanza kabisa, kitendo cha kukuta ujumbe wa kimapenzi kwenye simu ya mwenzi wako ambao umetoka kwa mtu mwingine, kinaanza kuathiri afya ya akili kutokana na kukupeleka ghafla kwenye hali ya hasira na masikitiko makubwa kutokana na kukiona kile ambacho hukuwahi kukitarajia na hapo ndipo unaweza kujikuta unaelemewa na mawazo na hivyo kujikuta unapata msongo wa mawazo.

Msongo wa mawazo ni tatizo kubwa la kiafya linaloathiri mfumo wa fahamu na afya ya akili kwa ujumla, japo wengi wamekuwa wakipuuzia tatizo la msongo wa mawazo na kuliona ni la kawaida.

Tatizo la msongo wa mawazo likidumu kwa muda mrefu kutokana na kuendelea kukumbuka lile tukio, ndipo sasa linaweza kuleta madhara mengine makubwa ya kiafya yakiwemo ugonjwa wa sonona, ambao kwa kitaalamu unaitwa depression.

Ugonjwa huu ni moja ya magonjwa ya akili ambayo mtu huyapata kutokana na kupitia matatizo kadhaa yaliyomfanya awe na masikitiko ya muda mrefu na kujiona hana thamani tena na hivyo hata kupata hisia za kutaka kujinyonga. Lakini tatizo lingine la kiafya linaloweza kusababishwa na tukio hili ni kupata magonjwa ya moyo na shinikizo lolote la damu aidha la kupanda au la kushuka.

Kibailojia, mfumo wa fahamu hufanya kazi kwa mawasiliano na mzunguko wa damu mwilini, hivyo kutetereka kwa afya ya akili kutokana na tukio hili kunaathiri moja kwa moja mfumo wa fahamu na hivyo kupelekea mzunguko wa damu kutofanya kazi kwa ufasaha ambako hatimae husababisha magonjwa ya moyo na matatizo ya shinikizo la damu.

Ushauri juu ya nini kifanyike, kwanza kabisa kwa wale ambao wanajikuta wanapitia hali hii wanapaswa kutambua ukweli kuwa, ni ngumu sana kupata suluhu pasipo ushauri wa kisaikolojia.

Hivyo watu wanashauriwa kuwaona wahudumu wa afya na hasa wa idara ya afya akili na viongozi wa imani za dini husika ili kupata ushauri stahiki wa kisaikolojia kwani kwa kufanya hivyo watajiepusha na msongo wa mawazo ambao mara zote ndio chanzo cha matatizo mengine ya kiafya na hasa sonona, magonjwa ya moyo na shinikizo la damu.

Advertisement