Jinsi siasa zinavyovuruga utendaji wa mipango miji

Muktasari:

  • Pamoja na kutajwa kwenye Katiba, Serikali za mitaa kama inavyoelezwa katika ibara ya 145 na 146, bado muundo na utekelezaji wake si huru kama ilivyo Serikali Kuu na kwa sababu hiyo na changamoto nyingine, zinashindwa kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 6 inatambua “Serikali” kama Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Serikali za Mitaa na mtu yoyote anayefanya kazi kwa niaba ya serikali.

Pamoja na kutajwa kwenye Katiba, Serikali za mitaa kama inavyoelezwa katika ibara ya 145 na 146, bado muundo na utekelezaji wake si huru kama ilivyo Serikali Kuu na kwa sababu hiyo na changamoto nyingine, zinashindwa kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Miongoni mwa changamoto zinazojitokeza ni pamoja makusanyo ya kodi na mapato mengine katika vyanzo vya halmashauri, huku pia kukiwa na ucheleweshwaji wa bajeti kutoka serikali kuu.

Changamoto hizo nyingine ni pamoja na utendaji wa mabaraza ya madiwani unaoonekana kuathiriwa na wateule wa Rais, wakiwamo wakuu wa mikoa na wilaya na masuala mengine ya kisiasa, kama inavyobainishwa katika tafiti mbalaimbali.

Utafiti wa ESRF

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Ardhi na Chuo Kikuu cha Mzumbe katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma, Arusha, Mbeya na Mtwara umeonyesha jinsi siasa zilivyoathiri utendaji wa Serikali za mitaa na mabaraza ya madiwani yanavyodharauliwa.

Katika utafiti huo, kila taasisi ilichukua eneo lake ambapo Chuo Kikuu cha Mzumbe (MU) kilijikita katika eneo la uhusiano kati ya ngazi ya Taifa na Serikali za miji kwenye utoaji wa huduma za miundombinu.

Akitoa matokeo ya utafiti huo, Dk Stella Kinemo wa MU anatoa mfano wa Halmashauri za Miji ya Tunduma na Ujiji Kigoma, akisema kumekuwa na mivutano kati ya madiwani na wakuu wa wilaya.

“Mivutano kati ya madiwani na wakuu wa wilaya imesababisha kubadilishwa kwa ardhi za shule, hospitali na vituo vya mabasi. Isitoshe kuna tabia ya wakuu wa mikoa na wilaya kutoheshimu uamuzi wa madiwani,” anasema Dk Kinemo.

Anasema kutokana na hali hiyo, nguvu ya mabaraza ya madiwani hutekwa na maamuzi ya kisiasa kiutawala.

Akizungumzia nguvu ya Serikali Kuu katika ukusanyaji wa mapato, Dk Kinemo anaelezea hatari ya wafanyabiashara wa Tanzania katika eneo la Tunduma waliofunga maduka yao na kukimbilia nchini Zambia.

“Kumekuwa na mazingira mabaya ya biashara na kusababisha baadhi ya wafanyabiashara kuhamia nchini Zambia na hivyo kushuka ukusanyaji wa mapato,” anasema.

Akifafanua zaidi, anasema hata maelekezo ya sera ya elimu bila malipo imezua utata katika ngazi ya serikali za mitaa ambako nako hawana uwezo wa kukabiliana na changamoto ya gharama za elimu zilizokuwa zikitolewa kwenye michango ya wazazi.

“Baada ya kukatazwa kwa michango shuleni, wazazi wamekataa kuchangia Sh100 ya maji na kusababisha vyoo vya kisasa visitumike. Baadhi ya wazazi wamechukua madawati, mahindi na maharage waliyochangia, masomo ya ziada yamesimamishwa na madarasa yanafurika wanafunzi,” anasema.

Dk Kinemo anafafanua zaidi jinsi walivyobaini nguvu ya Serikali kuu katika kuajiri watumishi wa kada mbalimbali wa serikali za mitaa.

“Vyanzo vya mapato navyo vinachukuliwa na Serikali kuu kwa matarajio kuwa fedha zitarejeshwa kwa wakati, lakini mara nyingi hazipelekwi kulingana na bajeti zilizowekwa.

“Vilevile hakuna mawasiliano rasmi kati ya idara zinazotoa huduma, bali iwapo kunakuwa na mahitaji tu. Kwa mfano, Manispaa ya Dodoma imejenga barabara ya lami halafu baada ya muda mfupi, Mamlaka ya Maji (Duwasa) inakuja kuchimba ili kupitisha bomba la maji,” anasema na kuongeza:

“Angalau katika halmashauri ya Nyamagana na Manispaa ya Dodoma (wakati huo), mamlaka husika zilikuwa zikifanya vikao rasmi.”

Mgawanyo wa fedha

Akieleza matokeo ya utafiti huo, mtafiti mwandamizi wa ESRF, Dk Daniel Ngowi anasema katika kipindi cha mwaka 2013/14 hadi 2016/17 inaonekana utoaji wa fedha za bajeti ya maendeleo kutoka Serikali kuu haukutabirika jambo linaloathiri maendeleo ya miji katika majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Mkoa wa Mtwara.

“Utoaji wa fedha hautabiriki, kwa mfano katika jiji la Arusha walipata asilimia 20 ya mahitaji yao mwaka 2014/15 lakini kwa mwaka 2016/17 wakapata asilimia 131, jambo linalofanya kazi ya mipango miji kuwa ngumu, ikiwa ni pamoja na ukarabati wa miundombinu,” alisema Dk Ngowi.

Hata hivyo, anasema ukusanyaji wa mapato katika majiji hayo uko vizuri, ambapo kwa jiji la Dar es Salaam limekuwa likikusanya asilimia 97 kulingana na bajeti yake, huku jiji la Arusha likikusanya asilimia 95, Mtwara asilimia 86, Dodoma asilimia 84, Mbeya na Mwanza asilimia 61.

“Ukiondoa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Halmashauri zote zimekumbwa na uhaba wa fedha baada ya kuondolewa kwa kodi ya majengo katika Serikali za Mitaa iliyokuwa ikichangia asilimia 30 ya mapato ya mapato na kuhamishiwa TRA,” alisema.

Akifafanua zaidi, Dk Ngowi anasema katika kipindi cha miaka mitano (2013/14-2016/17) jiji la Dar es Salaam lilipewa wastani wa asilimia 36.1 (Sh28.3 bilioni) huku Sh50.1 bilioni sawa na asilimia 63.9 zilizopitishwa kwenye bajeti zikikosekana.

“Kwa hiyo, mamlaka za Dar es Salaam, haziwezi kutegemea mapato ya Serikali kuu kugharamia miundombinu ikiwa pamoja na ukarabati,” anasema.

Hata hivyo, anasema kwa jiji la Mwanza kumekuwa na ahueni katika utoaji wa fedha za bajeti kwa kipindi cha miaka minne ambapo ni asilimia 11.4 tu ya bajeti ndiyo haikutolewa, ikiwa ni kiasi kidogo kuliko halmashauri zote zilizofanywa utafiti. Kwa upande wa jiji la Arusha anasema mapato yaliyokusanywa yalifikia Sh12.4 bilioni ikiwa ni upungufu wa Sh4.4 bilioni. Hata hivyo, fedha ambazo hazikutolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni Sh3.48 bilioni kwa mwaka sawa na asilimia 40.5.

Kwa jiji la Mbeya, asilimia 40.7 sawa na Sh5.6 bilioni hazikupelekwa ili kutekeleza bajeti iliyopangwa, huku pia ikishindwa kukusanya Sh6.4 bilioni sawa na asilimia 39 kutoka kwenye vyanzo vyake. Kwa jiji la Dodoma, wastani wa asilimia 32.5 sawa na Sh7.6 bilioni zilizopangwa kwenye bajeti hazikutolewa, utafiti huo umebaini. Lakini, kwa kulinganisha bajeti na mapato halisi inaonekana Halmashauri inafanya vizuri kwa kuwa na upungufu wa asilimia 17.1 tu.

Matokeo ya utafiti

Kutokana na utoaji fedha za bajeti usioaminika, watafiti wameshuhudia hali mbaya ya miundombinu ya afya na maji kwa jiji la Dar es Salaam.

Akieleza uzoefu wake, kwa jiji hilo, Dk Nathalie Jean-Baptiste wa Chuo Kikuu cha Ardhi anasema hali ya vyoo ni mbaya ambapo kati ya watu 10 hadi 16 wanashirikiana choo kimoja.

“Tulichokiona kwenye mitaa ya Keko Machungwa kwa mfano, ni hali mbaya ya vyoo, hivyo kunahitajika maboresho ya haraka ya usafi wa majitaka. Tumegundua kuwa watu hawana uwezo wa kununua maji kwa ajili ya usafi, wakati maji ndiyo muhimu kwa usafi wa mazingira,” anasema Dk Nathalie.

Anasema kinachoonekana ni kuwa hakuna uwekezaji wa kutosha katika usafi na majitaka na kwamba vyoo vinavyoonekana kwenye makazi duni haviwaridhishi wakazi wake.

“Wananchi hawaridhishwi na gharama na upatikanaji wa maji. Kuna haja ya kuboresha miundombinu ya maji lakini maboresho hayo yasiongeze gharama za upatikanaji wake,” anasema.

Hata hivyo, anasema baadhi ya wanawake katika eneo la Keko Machungwa walioungana na kuanzisha kikundi cha kuchimba vyoo mitaani ikiwa ni sehemu ya kujipatia kipato.

Mapato na matumizi

Ukusanyaji wa Mapato Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982 imeainisha vyanzo vya mapato kwenye Halmashauri za wilaya na vijiji.

Serikali za mitaa zinapata mapato yake kutoka kwenye vyanzo mbalimbali. Vyanzo hivi ni pamoja na fedha zitokanazo na biashara, viwanda, huduma, ada ya leseni, ushuru na vibali.

Hata hivyo, baadhi ya makusanyo ya mapato katika Serikali za Mitaa yanafanywa na taasisi za Serikali Kuu (ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania). Pamoja na kwamba fedha hizi zinakusanywa kutoka kwenye serikali za mitaa, matumizi yake yanaamuliwa na Serikali Kuu.

Kwa mujibu wa sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982, Waziri anayehusika na Serikali za Mitaa baada ya kushauriana na wadau wengine anaweza kuamua mgawanyo wa vyanzo vya mapato kwenye ngazi tofauti za halmashauri.

Ufinyu wa demokrasia

Maamuzi katika ngazi ya Serikali za Mitaa Moja kati ya shughuli kuu za Serikali za Mitaa ni kuimarisha demokrasia katika eneo lake na kutumia demokrasia kuharakisha maendeleo ya wananchi (ibara 146).

Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria ya Serikali za Mitaa (toleo la 2000), maamuzi ya kanuni na miongozo ya uendeshaji wake yanategemea kibali cha waziri anayehusika na Serikali za Mitaa ambaye kimsingi ni mtumishi wa serikali kuu.

Wakati halmashauri za wilaya, manispaa na miji zikipewa nafasi finyu ya kujiamulia mambo yao, wananchi hawana sheria inayowasaidia kuwabana viongozi na watendaji wao kuwajibika moja kwa moja kwa wananchi hasa wanaposhindwa kutekeleza wajibu wao.