Jinsi unavyoweza kufanya maamuzi ya busara kuhusu pesa zako

Katika matumizi yako ya kila siku jifunze kujiwekea vikomo au mipaka, kujiwekea mipaka au vikomo katika matumizi hukusaidia sana katika uwezo wako wa kujizuia.

Kwa mfano katika nchi mbalimbali zilizoendelea, hata hapa Afrika ya kusini ambapo watu hufanya manunuzi kwa kutumia kadi, kila mtu anapewa uhuru wa kuamua kikomo cha manunuzi yake kwa siku kutokana na jinsi anavyoyajua matumizi yake.

Mara unapofikia kikomo hicho katika siku ile basi hakuna hela itakayotoka kupitia mashine za pesa “ATM” au katika kuchanja kwenye manunuzi ya bidhaa. Profesa Ariely ameongea sana na kufanya tafiti nyingi juu ya kuongeza uwezo wetu wa kujizuia kupitia kujiwekea vikomo vya matumizi.

Mfano mwingine ni vile vikopo, au visanduku watu wanajiwekea manyumbani, ambapo kila mtu anapopata hela fulani aliyojipangia huitumbukiza kwenye kopo na mazingira ya kuitumia au kuichukua fedha ile huwa yamedhibitiwa au kufanywa kuwa magumu ili tu hela ile ifikie malengo fulani.

Jipe muda wa kutulia na kupoa

Kama nilivyokwisha kudokeza awali, hisia zetu za kila siku ziwe mbaya au nzuri ninaweza kuathiri sana mchakato mzima wa maamuzi yetu ya kutumia pesa. Katika hili tunashauriwa sana kuchukua muda hususani kabla yakufanya maamuzi makubwa ya kifedha, kupoa kidogo na kujiuliza na kufikiri kwa kina kama kweli unachotaka kufanya kina faida kwa leo na kwa kesho.

Usifanye maamuzi yanayohusiana na matumizi ya pesa baada ya kushauriwa na kuhamasishwa sana na muuzaji. Ikibidi kama ni biashara ambazo wana vipeperushi omba kimoja nenda nacho nyumbani pumzika, kisome na ukitafakari.

Wengi wetu wamejuta sana baada ya kufanya maamuzi ya msingi sana yahusianayo na matumizi ya pesa pasipo kuwaza kwa kina au wakati ambapo nafsi na akili zao zilikuwa hazijapoa.

Chunga sana uwezo wako wa kujizuia

Nimesema kwamba uwezo wetu wa kujizuia huweza kuchoka pale unapotumiwa sana. Ni lazima kujifunza kuukagua uwezo wetu huu kila mara. Kama utaona uwezo wako wa kujizuia umechoka basi usifanye maamuzi yahusuyo matumizi siku au muda huo. Kwa mfano siku ambayo umeshinda kwenye maduka muda mrefu, siku ambayo umeshawishiwa sana na wauzaji wa bidhaa fulani, siku uliyochoka sana akili yako au ukiwa mwenye huzuni. Tulia, amua kufanya maamuzi hayo wakati ukiwa sawa.

Uwezo wetu wa kujizuia unaweza kuathiriwa na hisia zetu

Unapokuwa na huzuni ni rahisi sana kujikuta unatumia pesa nyingi katika kiu ya kutamani kujiburudisha ili ujisikie afadhali. Nimeongea na wengi ambao walipokuwa katika huzuni walikunywa sana pombe, labda zaidi sana ya matumizi yao ya kawaida. Hii ni pamoja na matumizi mengine ili tu kujifurahisha.

Imegundulika pia kwamba katika hali ya huzuni wengi hujikuta wakiwa rahisi kuuza walivyo navyo kwa bei ya chini sana na isiyo ya faida hata kama vitu hivyo ni vya gharama sana, au kununua kitu kwa gharama zaidi wakati vitu hivyo ni rahisi.

Hali ya kukinai pia inaweza kukufanya kujisikia kutokutaka tena kitu fulani na hivyo kutaka kipya, hali hii iko sana kwa jinsia ya kike, ambao wao wakijisikia kukichoka kitu (mfano nguo au viatu) basi hapalaliki mpaka kitu kipya kinunuliwe.

Kukinai huku sio kwenye bidhaa tu bali hata katika huduma au eneo, inawezekana umezoea kula au kukaa maeneo fulani ambayo ni gharama nafuu, ikitokea unajisikia kupakinai basi kwenda eneo lingine la gharama zaidi kwako haitokuwa ni tatizo.

Hisia nyingine inayoweza kuathiri uwezo wetu wa kujizuia ni hofu. Mara tunapokuwa na hofu kinachofuata ni jitihada za kujiwekea mazingira ya kutoihisi hofu hiyo hata kama mazingira hayo ni gharama sana.

Mfano angalia mtu mwenye hofu ya kuibiwa, hata kama hofu hiyo sio halisi sana ukilinganisha na mazingira basi nirahisi kwake kutumia gharama yoyote kwenye kujilinda. Ukizingirwa na hofu wala hupotezi muda kuwaza kutumia au kutotumia hela, bali unachokitaka wewe unahakikisha unakipata.