Monday, July 9, 2018

KOMBE LA DUNIA: Huko Russia ngumi zililika majukwaani hadi kwenye grosari

 

Usidhani waliokuwa Russia wamekwenda kwenye Fainali za Kombe la Dunia pekee, usidhani mambo yalikuwa kushangilia ushindi, kuna upande wa pili wa mabalaa.

Kwa ilikuwa ikitiliwa shaka mashabiki wa England. Hawa jamaa ni wamechizika kwa soka.

Ni wahuni hasa kwenye viwanja vya soka na wakilianzisha, mtiti wake si wa kawaida.

Lakini jamaa wa Russia walikwishalifahamu hili, kwani England na Russia walitifuana kwelikweli mwaka 2016 wakati wa Fainali za Euro. Zilipigwa na watu walipigika kisawasawa.

Russia na England kidogo uhusiano siyo kivile, na ndio maana waamuzi wakapigwa chini.

Kwenye soka sasa, Kamati ya maandalizi Russia walijua kuwa England wanakuja, na ndiyo magwiji wa ghasia katika viwanja. Jamaa hawashikiki hasa wakipata ile moja moyo kichwani.

Kabla ya kuanza kwa fainali zenyewe, Rais wa taifa hilo, Vladimir Putin na Rais wa

Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Gianni Infantino walikuwa na vikao vya mara kwa mara kuhusiana na suala la ulinzi kwa kuwa Russia imekuwa ikihusishwa na suala la Syria.

Hakuna ubishi kwamba Russia inahusishwa na mgogoro wa Syria na mgogoro huo umeingia

kwenye mataifa kadhaa na kuhusishwa na masuala ya kidiplomasia na kisiasa kwa baadhi ya

mataifa yakishutumiana kuhusiana na mgogoro wa Syria.

“Russia iko tayari kwa fainali na tutazilinda kwa nguvu zote,” anasema Rais Putin baada ya kukutana na Infantino kwenye mji wa Sochi.

“Mambo yatakuwa mazuri, fainali zitafanyika kama ilivyopangwa,” alihakikisha Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Arkady Dvorkovich.

ULINZI

Ukiacha mashabiki wa ghasia, Kutokana na mazingira ya kiusalama kwa taifa hilo, askari polisi 21,500 wametawanywa katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya usalama pekee, wakiwemo 17,000 watakaokuwa na kazi ya kulinda usalama maeneo yasiyofikwa na polisi pamoja na kutoa huduma.

Russia iliajiri askari wengi na kuwapa mafunzo maalumu kwa kile kilichoelezwa kutarajiwa kwa mashabiki wengi na zaidi wa England ambao dunia nzima wanafahamika kwamba wao ni watu wa fujo.

Mamlaka za kipolisi na usalama zimeanzisha operesheni za ulinzi wa anga pia kwa kutumia vyombo vya kisasa kibaini magaidi. Kamera za angani, ndege zisizokuwa na rubani ni kati ya vitu vinavyotajwa kulinda usalama wakati huu wa fainali hizo. Hayo ni masuala ya kigaidi na kidiplomasia ambayo kimsingi yamedhibitiwa hadi sasa.

Kauli ya Rais

Mapema itakumbukwa Rais Putin alisema kuwa walevi hawataonewa haya katika Fainali za mwaka huu kwani alikuwa na kumbukumbu nzuri ya mashabiki kupigana katika fainali za Euro 2016 kati ya Russia na England.

Baada ya kauli yake, meya wa jiji la Moscow mwenye kazi ya kuangalia usalama alisema: ‘Kama unakunywa, usihofu, wote watakaokuwa wanakunywa, wataingia uwanjani wakiwa hawana kilevi.

Wanasiasa wa Russia walikuja juu hasa baada ya kutokea vurugu katika baadhi ya viwanja na zaidi ni mashabiki wa soka wa England na Russia waliokuwa wakizipiga.

Pamoja na kauli mbalimbali, bado kumekuwa na matukio ya kuchapana makonde, wakati mwingine yaliwahusu mashabiki wenyewe kwa wenyewe ndani ya uwanja lakini pia nje kwenye pub mbalimbali.

VURUGU PUB

Kama ilivyo kawaida yao, mashabiki wa England walianzisha varangati kwenye grosari moja katika jiji la Moscow. Walikuwa wanapata kinywaji kabla ya kuibuka vurugu hizo.

Ugomnvi wenyewe ulikuwa hivi. Mashabiki wa England walikwenda kwenye grosary moja na kuagizia vinywaji, lakini waliambiwa meza moja wanatakiwa kulipa Pauni 50 (kama Sh110,000 za Tanzania).

Baada ya kuambiwa hivyo, wengine walilipa lakini mmoja akalianzisha kwa kugoma kutoa Pauni50.

Ukaanza mzozo na walipokuwa wakijiandaa kuondoka, mwanamama mmiliki wa grosari hiyo alilianzisha akitaka alipwa fedha yake. Hiyo ilikuwa usiku ambao England ilipoitoa Colombia kwenye mechi ya makundi.

Mwanamke mmoja alionekana akimshindilia makonde mwanamme mmoja aliyeonekana amelewa akigoma kutoa fedha.

Tukio hilo lilitokea kwenye grosari iliyoko Command House eneo la Chatham, Kent, ambalo lililamikiwa kwa kuwatoza wateja Pauni50kwa meza wanayotaka kujipatia huduma.

Wakati wa vurugu hizo, makopo ya bia yalikuwa yakivurumishwa huku pombe za watu zikimwagwa ovyo kwenye bilauri, kabla ya kijana mmoja aliyekuwa amevalia fulana ya England kushambuliwa na mashabiki wanaosemekana kuwa ni Warussia kabla ya polisi kuingilia kati.

Katika sakata hilo, watu zaidi ya 20 walikuwa wakisukumana na mmoja wa mashabiki hao, Linda Feheley alisema: “Wao kama watu kutoka England ilikuwa wakae pamoja wanyewe kwa kuwa timu yao inasonga mbele.”

Naye shabiki mwingine’ Georgina Hawes alisema: “Hapa wanatoza meza Pauni50 halafu hakuna hata usalama, ilitakiwa kuwa na usalama wa kutosha, lakini pia watu wanashindwa kujiheshimu na kuanzisha ghasia baa.”

Marylyn Ducasse-Hunter alisema: “Inatakiwa watu tufurahie ushindi, lakini si kupigana hivi...hii ni aibu sana.”

MMOJA AUAWA KWA KIPIGO

Wakati hali ikiwa hivyo kwenye baa hiyo ambayo polisi waliamulia ugomvi, polisi wa Devon and Cornwall walisema mtu mmoja aliuawa na mashabiki baada ya kuzuka ugomvi kwenye mchezo kati ya England na Colombia.

Raia huyo wa Uingereza aliuawa na watu wanaodaiwa kuwa ni mashaiki wa Russia alipkuwa anapata kinywaji kwenye baa ya The Three Elms katika mji wa Brixham, Devon na alifariki hospitalini baadaye.

Katika eneo lingine, polisi katika mji wa Moscow, wamewakamata mashabiki wa soka wa England baada ya kutokea vurugu zilizosababusha kuharibiwa kwa sanamu moja nje ya uwanja baada ya kuilaza Colombia.

VURUGU NYINGINE

Wakati fainali hizo zikiendelea, vurugu nyingine zilizuka kwenye Uwanja wa Spartak kwa mashabiki kurushiana makonde.

Mwanamke mmoja alionekana kuwa kinara wa vurugu, lakini hata hivyo walinzi wa usalama uwanjani walikwenda kutuliza rabsha hizo zilizoibuka katika mchezo kati ya Brazil na Serbia.

Katika mchezo huo, Brazil ilishinda mabao 2-0 ya Paulinho na Thiago Silva na kukata tiketi ya kucheza na Mexico hatua ya mtoano ambao nao iliwatoa.

Mwanamke huyo alikuwa amevalia fulana yenye bendera ya Brazil, alipigwa kwa kujichanganya na mashabiki kuokolewa na wanausalama kutuliza ghasia hizo.

MASHABIKI ARGENTINA WALIANZISHA

Unaweza kucheka. Mashabiki wa Argentina walianzisha ghasia lakini hii ilikuwa wao kwa wao. Ni baada ya timu yao kutolewa kwenye fainali za mwaka huu.

Mashabiki hao waliona kuwa kupoza machungu ya kutolewa ni kufanya ghasia. Ufaransa iliitandika timu hiyo mabao 4-3 mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Kazan na kumfanya Lionel Messi kushindwa kutinga robo fainali kwa mara ya pili tangu 1994.

Baada ya filimbi ya mwisho, mashabiki walikuwa wakiponda na wengine kusifu, sasa wengine wakashindwa kuvumilia kwa kupandishana hasira kuona timu yao imetolewa na kuanza kuzipiga wenyewe kwa wenyewe.

Vurugu hizo zilisambaa kwani kuna mtu mmoja aliyekuwa kifua wazi alionekana akimshambulia mwenzake na katika vurugu nyingine, mwanamke mmoja alijaribu kuwatenganisha, naye alichukua bonge moja la konde. Hii si mara ya kwanza mashabiki hao wa Artgentina kutwangana.

Picha mbalimbali pia zilikuwa zikimwoshesha shabiki wa Croatia akila mkong’oto kutoka kwa shabiki mwenzake.

-->