#WC2018: KOMBE LA DUNIA 2018: Fainali Russia zilinoga lakini teknolojia ya VAR ilitibua

Muktasari:

  • Ufaransa na Croatia zilikuwa zikicheza jana jioni fainali hiyo, iliyotanguliwa na mchezo kati ya Ubelgiji na England uliochezwa Jumatatu.

Bonanza la Fainali za Kombe la Dunia 2018 lililokuwa likifanyika kule Russia limemalizika jana jioni na kila mmoja amepata matokeo, bingwa ndiyo ameshapatikana na kutia kibindoni Sh852bil za ubingwa na kombe lililonakshiwa kwa dhahabu.

Ufaransa na Croatia zilikuwa zikicheza jana jioni fainali hiyo, iliyotanguliwa na mchezo kati ya Ubelgiji na England uliochezwa Jumatatu.

Ujerumani ilichemsha mapema kabisa huko Russia na kuliacha kombe na kurudi zao nyumbani huku mashabiki wakiwakaushia, hakuna kuwashangilia wala nini, wala kuwapa pole.

FAINALI ZA SAPRAIZI

Kutolewa kwa Ujerumani, kulishangaza. Ilifungwa na Mexico bao 1-0 na kukubali kipigo cha Korea Kusini 2-0. Hiyo ilikuwa kama sapraizi kwao.

Pia kulikuwa na nchi kama Argentina ya Lionel Messi na marafiki zake, Sergio Aguero, Paulo Dybala na Gonzalo Higuain. Hawakufua dafu kabisa.

Wengine ambao walishangaza ni Ureno ya Cristiano Ronaldo, Brazil ilikuwa na wakali kibao ambao walipigwa kibabe na Ubelgiji ambayo iliingia nusu fainali. Pia zimo; England, Misri, Hispania na Mexico ambazo zilipewa nafasi ya kufika mbali ikiwemo kuingia fainali. Senegal pia ilipewa nafasi sawa na Mexico.

England, Ubelgiji zilizocheza kusaka mshindi wa tatu Jumamosi zilikuwa zikipewa nafasi zaidi kucheza fainali.

TEKNOLOJIA YA VAR

Pamoja na Rais wa Fifa, Gianni Infantino kusifu, lakini unaweza kusema teknolojia ya VAR ilivuruga fainali za Russia. Ni wazi dunia haikuielewa.

Katika fainali za Russia, kati ya mambo yaliyotawala ni hizo (Video Assistant Referee) ambazo kazi yake ni kumsaidia mwamuzi mambo yanayoleta utata.

Katika fainali za mwaka huu, imetumika lakini kumekuwa na kelele nyingi kwamba matumizi ya VAR ni uamuzi wa mwamuzi kutaka msaada wa mashine hiyo au anaweza kushauriwa lakini bado uamuzi wa mwisho unabakia kwa mwamuzi mwenyewe. Hapa ndipo kwenye tatizo.

Bao la Diego Costa dhidi ya Ureno, penalti ya Ufaransa dhidi ya Australia pia penalti ya Sweden ilipocheza na Korea Kusini na nyingine nyingi, ni kati ya malalamiko yaliyopazwa, lakini uamuzi umeshatoka.

VAR haikuwa na maana pale waamuzi walipokaushia baadhi ya matukio hata kuonekana kama ni kwa ajili ya kuzibana baadhi ya timu. Mechi za Nigeria na Argentina, Brazil na Sweden pia Senegal ilipocheza na Japan ilionekana kulikuwa na uamuzi wa VAR kwa kuwa vitendo vya kukata ama kushika vilionekana, lakini waamuzi wakakausha.

Hata Shirikisho la Soka Brazil, CBF, lilituma waraka Fifa kutaka maelezo kwanini VAR haikutumika kwenye mchezo wao na Uswisi.

AFRIKA YABORONGA

Fainali za mwaka huu, timu zote za Afrika zimekomea hatua ya makundi. Kwa fainali za 2018 huko Russia, Afrika imebaki na masononeko kwa kushindwa kusonga mbali.

Ghana iliwahi kutikisa mwaka 2010 huko Afrika Kusini. Mataifa ya Afrika yamekuwa yakipapasa robo fainali na zaidi ni kutaka njia ya kusonga mbele zaidi japokuwa mambo yamekuwa magumu.

Timu nyingine za Afrika zilizowahi kuingia robo fainali ni: Cameroon mwaka 1990 na Senegal ilifaya hivyo 2002. Lakini matokeo yalipatikana muda wa ziada.

Mchambuzi wa masuala ya soka, Volker Finke alihojiwa na Sauti ya Ujerumani (DW), kabla ya fainali hizo na kusema moja kwa moja alibashiri kwa kusema haoni nafasi ya Afrika kufika mbali 2018.

Mwaka 2018, Mataifa ya Misri, Morocco, Nigeria, Senegal na Tunisia yaliingia kwenye Fainali za Russia, lakini yalishindwa kabisa kuonyesha kile Waafrika wamewatuma huko Russia n azote kuaga hatua ya makundi.

MASTAA WATUNDIKA DARUGA

Ni wazi fainali za Russia zimemaliza maisha ya ubingwa wa juu kwa baadhi ya mastaa wa soka. Wachezaji kama Cristiano Ronaldo aliyeisaidia timu yake kutwaa ubingwa wa Euro 2016 akiwa na Ureno, amekataa kuzungumzia hatma yake japokuwa inaonekana wazi hatoweza kucheza sababu ya umri. Fainali zijazo atakuwa na miaka 38.

Mwingine aliyekuwa akitazamwa ni Lionel Messi ambaye aliondoka kwa aibu. Messi hajasema lolote baada ya Argentina kutolewa kibabe na Ufaransa kwa kuchapwa mabao 4-3 na Ufaransa tena ndani ya dakika 90.

Baadhi ya waliotangaza kutundika daruga ni Gerard Pique, Andres Iniesta (Hispania), Javier Mascherano, Lucas Biglia (Argentina), Keisule Honda, Makoto Hasebe (Japan) na Sardar Azmoun wa Iran ambaye amestaafu akiwa na miaka 24 tu akielezea kuchukizwa na timu yake kutolewa.

REKODI YA UMRI

Kuna huyu kipa wa Misri, Essam El-Hadary ana miaka 45, ameweka rekodi kiboko kawashinda hata waliomtangulia kucheza Kombe la Dunia.

Tangu kuanza kwa fainali hizi 1930, kuna vibabu vitano vimecheza na Hadary kaongezeka mwaka huu kuwa wa sita. Kuna kipa wa Italia, Dino Zoff kacheza Kombe la Dunia akiwa na miaka 40 miezi minne na na siku 13. Hiyo ilikuwa mwaka 1982.

Kuna huyu kipa wa England, Peter Shilton kacheza Fainali za Kombe la Dunia 1990 akiwa na miaka 40 na alisimama langoni England ikilala 2-1 kwa Italia mechi ya mshidi wa tatu.

Kibabu kingine ni kipa wa zamani wa Ireland ya Kaskazini, Arsenal na Tottenham Hotspur, Pat Jennings alisimama langoni timu yake ikipigwa 3-1 na Brazil fainali za 1986 zilizofanyika Mexico akiwa na miaka 41.

Pia yupo mshambuliaji wa Cameroon, Roger Milla, alicheza fainali za 1990 akiwa na miaka 42 mwezi mmoja na siku nane. Alipiga mabao ya kutosha na kuifkisha mbali Cameroon.

Kipa wa Colombia, Faryd Mondragon alikuwa kwenye fainali za 2014 akiwa na miaka 43 na siku tatu.

MOSCOW YACHANGAMKA

Zilikuwa siku 30 zilizopamba na kuchangamsha jiji la Moscow. Inakadiriwa mashabiki na wageni zaidi ya milioni moja walifika kwa ajili ya fainali za mwaka huu.

Mashabiki walikwenda Russia huku wengine wakijaza migahawa na hoteli wakipata vinywaji na chakula. Baadhi ya maeneo yalifurika mashabiki wakijipatia misosi mbalimbali.

Watu wa utamaduni mbalimbali walikutana na inaelezwa kuwa unapokuwa kwenye treni za abiria maarufu metro, watu wote huwa kimya, lakini ilikuwa ni kelele mtindo mmoja za mashabiki. Hata masuala ya kibaguzi yalionekana kumalizika. Watu walitembea, wanazunguka huku na huko wakifurahi.

Kwa kiasi kikubwa, rangi za bendera za mataifa mbalimbali zilitawala maeneo mbalimbali kwenye miji ya Russia na zaidi ni mashabiki wakiwa na bendera za mataifa yao.

FIFA YATOA DONGE NONO

Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), mwaka huu limeboresha zawadi za washindi. Awali bingwa alikuwa akipata Dola358 milioni na kombe na mara ya mwisho zilichukuliwa na Ujerumani mwaka 2014 katika fainali za Rio de Janeiro, lakini bingwa wa mwaka huu, atalamba Dola400 milioni.

Fifa haikuziacha hata timu 16 zilizotolewa kwenye hatua ya makundi, kila mmoja amelamba Dola8 million wakati timu nane zitakazotolewa hatua ya 16 Bora zilipozwa na Dola12 milioni kila mmoja.

Timu zilizotolewa robo fainali zimelamba Dola16 milioni kila mmoja wakati mshindi wa nne Dola 22 milioni na mshindi wa tatu Dola24 milioni. Mshindi wa pili Dola28 milioni na bingwa Dola38 milioni.

Mbali na fedha hizo, Fifa ilitanguliza fedha za maandalizi kwa timu zote 32 kuwa kila mmoja alipata Dola1.5 milioni.

Fifa pia ilitenga Dola209 milioni kama bonasi kwa ajili ya klabu zilizoruhusu wachezaji wake kucheza Kombe la Dunia pamoja na Dola134 milioni kama fedha za kinga au bima kwa ajili ya fidia kwa wachezaji. Fifa imeongeza Dola791 milioni ikiwa ni asilimia 40 zaidi ya fedha zilizotolewa fainali zilizopita.