Monday, July 9, 2018

Kadi zilizowamaliza Senegal hata Serengeti Boys zinawahusuIbrahim Bakari

Ibrahim Bakari 

Fainali za Kombe la Dunia zinazofikia ukingoni huko Russia, ni wazi bado Waafrika hawajaielewa teknolojia ya VAR iliyokuwa ikitumika kwa ajili ya kuwasaidia waamuzi ilipotokea mazingira yenye utata.

Ninasema hivyo kwa kuwa zilishika kasi pale mataifa ya Afrika ama timu ambazo pengine hazihitajiki ilikaziwa. Ilifikia hatua watu tudhani hivyo kwa kuwa wakati mwingine kulikuwa na uamuzi tata lakini watu waliminya.

Nigeria ilinyimwa penalti ya wazi baada ya mchezaji mmoja wa Argentina kushika kwenye 18 sawa na Senegal, lakini mwamuzi alichunia na Afrika ikamaliza maisha yake kule Russia.

Hiyo ilikuwa VAR, ishu hapa ninataka kuiangazia hii ya Senegal kutupwa nje ya Fainali za Kombe la Dunia licha ya kufungana kwa kila kitu na Japan. Walimaliza mchezo wao kwa sare ya kila kitu, kucheza, kushinda, sare, kufunga, kufungwa na hata pointi.

Kilichotokea, kikosi hicho cha Simba wa Teranga kiliishia kukamata nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi lake.

Kukawa na utata, timu gani inayopaswa kutinga hatua inayofuata kwenye 16 bora, ndipo hapo kilipotumika kigezo cha kadi za njano, timu yenye kadi chache ndiyo inayosonga mbele. Japan, ikapenya na kutinga hatua 16 bora, wakati Senegal walishindwa kutokana na wao kuwa na kadi sita za njano, huko wenzao wakiwa na kadi nne tu.

Kadi njano nne za Japan, walizipata kwenye mechi hizo, moja dhidi ya Colombia, mbili dhidi ya Senegal na moja dhidi ya Poland. Lakini, kwa upande wa Senegal, ambao ilibidi waishie hatua ya makundi, hadi za njano zilizowaponza ni hizi hapa.

Salif Sane vs Poland, dakika 49, Idrissa Gueye vs Poland, dakika 72, M’Baye Niang vs Japan, dakika 59, Youssouf Sabaly vs Japan, dakika 90

Cheikh N’Doye vs Japan, dakika 91 na M’Baye Niang vs Colombia, dakika 51.

Hao ni wachezaji. Sasa ninachotaka kusema hapa, hili ni somo tosha kwa wachezaji wetu. Nimesema Serengeti Boys kwa kuwa mwakani tutakuwa nao kwenye Fainali za Afrika kwa vijana wa U-17,

Hili ni somo. Wachezaji wetu wamekuwa na tabia ya kuomba waonyeshwe kadi kwa maana ya kwamba wamekuwa na ukosefu wa nidhamu. Kadi hizo zimewagharimu kwa kiasi kikubwa Senegal.

Wachezaji wanatakiwa kucheza kwa kujituma lakini kwa nidhamu. Kama hao Serengeti Boys wapewe somo mapema kuepuka kadi zisizokuwa za lazima.

Hutakiwi kupiga mpira baada ya filimbi ya mwamuzi kusimamisha mchezo. Mchezaji hatakiwi kubishana na mwamuzi, kupingana na uamuzi wa mwamuzi, kupoteza muda kizembe na hata kumlalamikia mwamuzi na ni suala la nahodha na kinyume chake, hizo zote ni kadi pamoja na mambo mengine ya uwanjani.

Tumesema Kombe la Dunia ni somo tosha, kila eneo limesomeka kivyake ikiwemo hili tu nililoliangalia la kadi zilizoimaliza Senegal.

Ninaamini kati ya mafunzo watakayopata Serengeti Boys, nidhamu kwa mwamuzi litachukua nafasi yake.

Kinachotakiwa hapa, ni wachezaji kupewa somo katika kila eneo.

Uzuri tuna wakufunzi wa waamuzi, walioiva, waitwe na wapewe somo la nini wanatakiwa kukifanya uwanjani, wana saikolojia na ninajua kuna wengi watashirikishwa katika maamuzi yao, lakini kwa hili ninaamini litawasaidia na kuepusha wachezaji kupata kadi zisizokuwa za lazima na kusababisha kukosa wachezaji muhimu kwa mechi.

-->