Kahawa itaamua hatima ya wanasiasa wa Kagera

Muktasari:

  • Kabla ya anguko la zao hilo na wakulima kukata tamaa, viongozi wa vyama vya msingi walikuwa na nguvu kubwa ya ushawishi hata kwenye majukwaa ya kisiasa na walitumika kama kundi muhimu la kufanikisha ushindi.

Hakuna jinsi unavyoweza kutenganisha siasa za Mkoa wa Kagera na kilimo cha kahawa, zao ambalo ni tegemeo kubwa la wakulima wengi. Ukitaja kahawa unagusa uchumi wao na mfumo wa maisha ya kila siku ya mkulima.

Kabla ya anguko la zao hilo na wakulima kukata tamaa, viongozi wa vyama vya msingi walikuwa na nguvu kubwa ya ushawishi hata kwenye majukwaa ya kisiasa na walitumika kama kundi muhimu la kufanikisha ushindi.

Ahadi ya CCM kwa wakulima hao ni kuboresha bei ya zao hilo pengine kuzidi awamu nyingine zote za uongozi zilizopita. Ni kukata mirija yote iliyonyonya jasho la mkulima, hatua iliyotarajiwa kuongeza bei maradufu.

Hatua za awali katika utekelezaji wa ahadi yake ilikuwa ni kufuta tozo 17 ambazo zilitajwa kuwa sehemu ya mirija iliyodhoofisha bei, na moja kupunguzwa. Uamuzi ulitangazwa na Waziri wa Kilimo, Charles Tizeba wakati akisoma Makadirio ya Bajeti mwaka 2017/2018.

Pia, kiwango cha makato kilichochukuliwa na halmashauri kilishushwa kutoka asilimia tano hadi tatu na wakulima walishangilia uamuzi huo wa Serikali kwa kuwa awamu zilizopita zilipata kigugumizi kufikia uamuzi kama huo.

Nyuma ya pazia

Hata hivyo, pamoja na Serikali kufuta idadi kubwa ya kodi katika zao la kahawa matokeo yaliyotarajiwa hayajapatikana. Pengine wakulima watalazimika kuendelea kupokea malipo ya awali ya Sh1,000 kwa kilo ya kahawa isiyokobolewa (maganda) mpaka hapo hali itakapoimarika.

Serikali bado inaendelea kutumia rasilimali zake kupambana na magendo ya kahawa inayovushwa kwenda nchi jirani, tatizo ambalo lilitarajiwa kuisha lenyewe bila msukumo endapo Serikali ingetumia rasilimali hizo kuhakikisha bei ya hapa nchini inavutia kuliko ya jirani.

Karata za wabunge

Suala la bei ya kahawa na mfumo mpya wa ununuzi wa zao hilo ambao kwa sasa ndiyo lugha ya wakulima, kwa upande wa pili umewaweka njia panda wabunge wa Mkoa wa Kagera na kuwafanya kuwa na tahadhari.

Hata waliozungumzia suala hilo, walitumia njia ya kupinga na wakati huohuo kuunga mkono pengine wasije kunyooshewa kidole kwa kukosoa mipango ‘mizuri’ ya Serikali ambayo sharti itetewe na kila mwakilishi wa wananchi aliyebeba bendera ya CCM.

Baadhi ya wabunge pamoja na kuonekana kama vile hayawahusu, wanatakiwa wakumbuke kuwa siku si nyingi watapata taabu sana wakati wa kutetea nafasi zao kwenye uchaguzi ujao kwa kuwa kero namba moja kwa wakulima wa kahawa ambao ndio wengi, huenda ikawa bei ndogo ya kahawa.

Itakuwa ni kujidanganya kwa mbunge kutegemea kujinadi kwa kutumia mafanikio ya serikali kwenye ujenzi wa miundombinu ya reli na barabara mbele ya wapiga kura ambao mfumo wao wa maisha unategemea zao la kahawa.

Mbunge wa Jimbo la Nkenge, Dk Diodorus Kamala wakati anachangia Makadirio ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2018/2019, alisema mpango wa Serikali wa kuwataka wakulima kuuza kahawa yao kupitia vyama vya ushirika ni mzuri ingawa unahitaji maandalizi ya kutosha.

Katika Bunge hilohilo, Profesa Anna Tibaijuka wa Muleba Kusini alihoji kwa mfumo huo, mkulima kikongwe mwenye kilo 20 tu za kahawa atawezaje kusafiri kufuata fedha zake Benki ambapo sasa malipo yatakuwa yanafanyikia badala ya utaratibu wa zamani wa kufuata malipo kwenye chama cha msingi. Huu ni mfumo mpya unaofuta leseni za ununuzi wa kahawa kwa kampuni binafsi, ambazo sasa zinaelekezwa kufuata bidhaa hiyo kwenye mnada kama inavyofanyika kwa zao la korosho kwa mikoa ya kusini.

Ukisikiliza lugha ya wakulima, hatua hiyo mpya inasaidia kuongeza ushindani na malipo yanafanyika siku hiyo.

Tafakari ya Rais Magufuli

Ikiwa kodi kero karibu zote zimefutwa katika zao hilo na bado wakulima wanashawishika kuwauzia kahawa wafanyabiashara wa magendo wanaozisafirisha kwenda nchi jirani, ni dhahiri kwamba bado kuna jambo halijafanyika sawasawa kwa upande wetu.

Kwamba wafanya magendo hawalipi kodi ya Serikali ndiyo sababu ya kununua kahawa kwa bei kubwa hayo haiwezi kuwa sababu inayojitosheleza. Kwamba mizani yao haina ubora, hivyo wanamwibia mkulima na hivyo ikawa sababu ya kulipa bei mara tatu zaidi, nayo si kweli.

Kauli ya Rais Magufuli hivi karibuni wakati akiwaapisha mawaziri wapya baada ya kufanya mabadiliko madogo kwenye Baraza lake, kwamba anasikitishwa na bei ndogo ya kahawa ni ujumbe kuwa maboresho zaidi yanahitajika ili bei iwe na tija na imvutie mkulima.

Rais Magufuli anasema ni bora kuwa na wanunuzi binafsi hata kutoka nje ya nchi kama wana uwezo wa kutoa bei nzuri kwa wakulima ambao jasho lao limenyonywa kwa miaka mingi.

Kama hivi ndivyo, suala la kumfuta jasho mkulima haliwezi kuwa jukumu la vyama vya ushirika pekee bali kazi hiyo inaweza kufanywa pia kwa ushirikiano na wanunuzi wengine, kwa kuwa na mfumo imara unaonufaisha pande zote kwa kutanguliza masilahi ya mkulima.

Mawaziri kazini

Siku nne baada ya kuapishwa, Naibu Waziri wa Kilimo, Omar Mgumba ziara yake ya kwanza ameifanya mkoani Kagera mkononi akiwa na ajenda ya bei ya kahawa ambapo pamoja na kufanya vikao vya kikazi, ongezeko la bei halikupata suluhisho.

Kwa nyakati tofauti pia Waziri Tizeba amefika na kufanya ziara na kutoa maelekezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutaka wakulima wasikopeshwe mazao yao na vyama vya ushirika lakini suala la bei limebaki palepale.

Miongoni mwa mambo yaliyomshangaza Mgumba ni kahawa kununuliwa kwa bei ndogo wakati nchi jirani bei ikitajwa kuwa kubwa, swali ambalo liko kwenye vichwa vya wakulima. Maswali yameongezeka zaidi baada ya wakulima chini ya mfumo mpya kukosa uhuru wa kuchagua mnunuzi wa mazao yao.

Baada ya kupokea taarifa ya Mkoa wa Kagera, Mgumba alisema wakulima wanatakiwa kusubiri malipo baada ya kahawa yao kuuzwa kwenye mnada na kuwa huo ndiyo msingi wa ushirika, ambao ni sauti ya wakulima walioamua kuungana.

Kimsingi vyama vya ushirika vimedhoofika. Hata wanachama waliojisajili kama wakulima, bei haikuwashawishi kupeleka kahawa yao ikilinganishwa na wanunuzi wengine binafsi, ingawa mfumo unawalazimisha kuuza kwenye ushirika.

Mbadala wa kahawa

Soko la kahawa limeendelea kutegemea wanunuzi wa nje na kufanya bei yake isiwe ya kuaminika kwa kuwa pia kwenye mnada wa kimataifa kahawa ya Tanzania inalazimika kushindanishwa na ile ya wazalishaji kutoka mataifa mengine yaliyopiga hatua kwenye shughuli za kilimo.

Tishio hilo linajenga sababu kwa wakulima wa mkoa wa Kagera kuwekeza nguvu katika kilimo cha mazao mengine ya biashara badala ya kutegemea zao kuu la kahawa, ambalo limezungukwa na changamoto nyingi kuanzia shambani hadi mnadani.

Mathalani zao la alizeti ambalo husitawi zaidi katika mikoa wa Singida na Tabora linaonyesha mafanikio kwa baadhi ya wakulima wa Kagera wanaolipanda kwa majaribio ambapo pia uzalishaji wake unaweza kuwa rahisi ikilinganishwa na kahawa.

Mafuta yanayozalishwa kwa alizeti soko lake kubwa liko nchini na mkulima ana nafasi ya kujipangia bei baada ya kupima nguvu aliyowekeza shambani, tofauti na kahawa ambayo huchukuliwa kwa mkopo bila hiari ya mkulima.

Ili kumsaidia mkulima, wanasiasa hawawezi kukwepa wajibu wa kuhamasisha kilimo cha mazao mbadala huku wakitetea masilahi bora zaidi na hata wakulima wanatakiwa kuwapima viongozi wao kuanzia hapo.