Kampeni za vijembe sio bora kuliko sera

Muktasari:

  • Monduli ni moto na Ukonga ni moto. Hizi zote ni juhudi za kupigania majimbo ya ubunge baada ya waliokuwepo awali kuachia ngazi kwa namna moja au nyingine.

Ninaweza kusema mambo ni moto kwa sasa, huku CCM kule ACT-Wazalendo, pale Chadema na vyama vingine.

Monduli ni moto na Ukonga ni moto. Hizi zote ni juhudi za kupigania majimbo ya ubunge baada ya waliokuwepo awali kuachia ngazi kwa namna moja au nyingine.

Tangu nchi hii iingie kwenye mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na uchaguzi wa kwanza ukafanyika mwaka 1995, siasa za nchini Tanzania zimechangamka kiasi cha kuchemsha vichwa vya wagombea wanapokuwa jukwaani kunadi sera zao kwa sababu ukizubaa imekula kwako.

Kwa sababu hiyo wagombea hujitahidi kwa kila namna kujieleza kwa wananchi kuhakikisha wanashinda na kupata ridhaa rasmi ya kuwawakilisha wananchi katika Bunge.

Hata hivyo, kadri siku zinavyozidi umakini wa wagombea kueleza sera zao umekuwa ukipungua badala yake kupigana vijembe kuliko kueleza sera kunaongezeka kwa kasi.

Jambo hili linawaweka wananchi njia panda katikia kufanya maamuzi kwani hawapati fursa ya kutosha ya kuelezwa mambo watakayofanyiwa.

Wiki kadha zilizopita niliandika makala kuhusu hamahama ya wanasiasa na wakitumia msemo wa “kuunga mkono juhudi za Rais”. Nilifafanua namna ambavyo wanasiasa hawa wanataka kutupeleka katika mtazamo usio sahihi kuhusu uungwaji mkono wa juhudi za Rais. Hii ndiyo sababu ya kurudiwa kwa chaguzi zitakazofanyika baadaye mwezi huu.

Jambo ambalo limenishangaza ni kuona hamahama hii ikigeuka mtaji kwa baadhi ya wagombea na kuifanya kama vile ni moja sera zao, hamahama hii imekuwa kijembe kwa mwingine.

Bado najiuliza, hivi wananchi wanataka kusikia sera au vijembe vya wagombea, sijapata jibu. Ninachoelewa ni kwamba wananchi watakupa ridhaa kwa kukupigia kura ikiwa yale utakayowaeleza yatakuwa na tija kwao na si kuwaeleza habari za mtu mwingine.

Ni jambo bora kuwaeleza watu mipango yako na sera zako kwa kuwa hayo ndiyo utakayoenda kuyafanya na sio mtu unayemzungumzia jukwaani.

Hapa ndipo ninaelewa maana ya dhana isiyo kweli ambayo mhusika anashindwa kupambana na hoja anaanza kupambana na mtoa hoja.

Hivi sasa kila wakati wa kampeni ukifika baadhi ya wagombea hushindwa kupambana na hoja za washindani wao badala yake wanaanza kuwashambulia wenzao kwa vijembe ambavyo havina maana yoyote.

Wagombea toeni hoja zitakazofanya wananchi waone sera ya mwenzako haifai ila yako inafaa, waeleze watu kwa nini wakuchague wewe na si mpinzani wako.

Hivi sasa si ajabu kusikia kwenye majukwaa ya kampeni mgombea akisema msimchague fulani kwa sababu mkimchua atakuja huku kwetu au mwingine atasema msimchague fulani kwa sababu mlimchagua lakini amewaacha.

Sasa hapa unaweza kujiuliza ina maana huyu anayezungumza haya anataka achaguliwe kwa sababu mwenzake kashindwa au kwa sababu yeye anayo atakayowafanyia wananchi?

Wananchi bado wanatafakari namna wabunge waliowaamini wamekimbia ukirejelea mifano ya majimbo ya wagombea ambao wamehama vyama, Singida Kaskazini, Ukonga, Monduli na kwingineko halafu hilohilo la kuhama linafanywa sera pamoja madhaifu mengine.

Ninatamani ifike mahala kila mgombea atambue kuwa watu wanapaswa kuwa na imani na wewe na si wewe kupitia mgongo wa mtu mwingine wala si chama. Ni kweli kwamba mnasimamia ilani ya vyama mnavyoviwakilisha, lakini msimamizi ni wewe pamoja na Serikali, kwa hiyo hebu waeleze watu ambacho wewe utakifanya kuliko kuwapotezea muda ukiponda wenzio na kuwapiga vijembe. Sikatai kwamba vijembe ni sehemu ya siasa lakini ninaona faida yake ni ndogo kuliko kuwaeleza watu ajenda ulizonazo ili wakuamini wewe mwenyewe.

Hebu ufike wakati tubadilishe gia angani kwa sababu wananchi wanajikuta kwenye masanduku ya kupigia kura bado wapo njia panda kwani walikuwa wanasikia vijembe na mbwembwe zisizo na maana yoyote.

Ukiachilia mbali wale ambao huwa wanapiga kura kwa sababu ya mgombea anatoka chama chake, yaani wao sera ziwe nzuri ziwe mbovu, mgombea aongee masuala ya msingi yasiwe ya msingi wao kura watampa tu, lakini wapo ambao huwa wana kiu ya kusikia kutoka kwa mgombea husika kwamba utafanya nini na nini kwa ajili yao.

Ni jambo la kustaajabisha kukuta mgombea anatumia muda mwingi kumwelezea mtu ambaye hahusiki kwenye sera zake na wananchi wanashangilia kwelikweli. Unatoa wapi muda wa kuanza kueleza udhaifu binafsi wa mtu? Unaweza kukuta mgombea anageuka mchekeshaji tu halafu anaacha kuzungumza mambo ya msingi, huko ni kukosa uwezo wa kuandaa sera na hoja zenye ushawishi watu.

Mtindo huu wa kwenda jukwaani kuwachekesha wananchi na kuwaponda watu ndio unasababisha tunapata wabunge wanaoenda kusinzia bungeni, wanaofuata upepo na wanakubaliana na kila kinachosemwa.