Kasi mpya ya Kangi Lugola, makosa na usahihi wake

Muktasari:

  • Kuondoka kwa Mwigulu kumefanya Wizara ya Mambo ya Ndani iwe imehudumiwa na mawaziri watatu ndani ya kipindi cha chini ya miaka mitatu. Mawaziri wawili walipokezana ndani ya nusu muhula wa miaka mitano. Ndani ya kipindi hicho cha nusu muhula, Mwigulu alipata kutumikia wizara mbili.

Julai Mosi mwaka huu, huduma ya Dk Mwigulu Nchemba kama waziri wa Mambo ya Ndani ilikoma. Hivyo, Mwigulu amebaki mbunge wa Iramba Magharibi peke yake. Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola amepokea kijiti baada ya kuapishwa na Rais John Magufuli, siku iliyofuata, Julai 2, 2018.

Kuondoka kwa Mwigulu kumefanya Wizara ya Mambo ya Ndani iwe imehudumiwa na mawaziri watatu ndani ya kipindi cha chini ya miaka mitatu. Mawaziri wawili walipokezana ndani ya nusu muhula wa miaka mitano. Ndani ya kipindi hicho cha nusu muhula, Mwigulu alipata kutumikia wizara mbili.

Desemba 10, 2015, Mwigulu alikuwa mmoja wa mawaziri 15 wa mwanzo kabisa walioteuliwa na Rais Magufuli, alipotaja baraza lake lililokuwa na wizara 18. Alibakisha kutaja mawaziri wa wizara nne kwa kile alichoeleza kwamba alikuwa bado anawatafuta. Wizara hizo ni Fedha, Elimu, Maliasili na Utalii, vilevile Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Desemba 23, 2015, Rais Magufuli alikamilisha kutaja idadi ya mawaziri na naibu mawaziri kutokana na muundo alioutengeneza. Hata hivyo, haikupita miezi mitano, alimwondoa kazini waziri wake wa kwanza wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga. Uamuzi huo ulisababisha mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.

Mwigulu ambaye awali alikuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvu, alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani, kisha kukawa na ingizo jipya, mbunge wa Buchosa, Charles Tizeba aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Hivi sasa wizara hiyo imegawanywa mara mbili; Kilimo imebaki peke yake, Mifugo na Uvuvi inajitegemea.

Mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri aliyofanya Rais Magufuli Oktoba 7, mwaka jana, yalimpa daraja Lugola kuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. Aliyekuwa akishika nafasi hiyo, Luhaga Mpina aliteuliwa kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Kangi aliapishwa kuwa naibu waziri Oktoba 9, mwaka jana. Hivyo mpaka Julai Mosi, mwaka huu, alipoteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, kisha kuapishwa Julai 2, hakuwa ametimiza hata miezi tisa kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.

Na kwa vile ibara 55 (2) ya Katiba inayotoa mamlaka kwa Rais kuteua naibu mawaziri baada ya kushauriana na Waziri Mkuu, vilevile inawanyima hadhi naibu mawaziri kuwa wajumbe wa vikao vya Baraza la Mawaziri, hivyo basi, Lugola bado ni mpya mno na pengine hajapata kuhudhuria kikao hata kimoja cha Baraza la Mawaziri.

Kasi ya Lugola

Yapo mambo kadhaa ambayo ameingia nayo wizarani, na kwa kuwa hajafikisha hata mwezi mmoja ofisini, ni vizuri kumpongeza pale alipoanza vizuri, vilevile kumweleza kasoro zake mahali ambapo hajaanza sawasawa. Lengo ni kumshauri au kumsaidia aweze kuihudumia nchi vizuri.

Lugola ameingia kwa kasi kubwa. Ukimsoma na kumwelewa kupitia matamshi yake na hata vitendo, anaonyesha ameingia kazini kuyaelekea matokeo yanayotakiwa na kiongozi wake, Rais Magufuli, pamoja na Watanzania wote. Kangi anatafuta matokeo ya haraka, anataka mabadiliko wizarani ndani ya usiku mmoja.

Ni kweli mafanikio ya haraka kila mmoja angependa ayapate. Hata hivyo, pale unapoingia kwenye ofisi ambayo mtangulizi wako ameondolewa kwa sababu ya matukio yenye kuonekana nje, inatakiwa kwanza kutulia na kupata ukweli kwa nini yaliyotokea yalitokea na kwa vipi hayakuwa yamepata ufumbuzi?

Sababu mojawapo ya Mwigulu kuondolewa kazini ni ajali za barabarani. Lugola baada ya kuingia ofisini, alipaswa kusoma kidogo kiini cha ajali za barabarani kukithiri, ajue tatizo lipo wapi, kisha apange timu yake kwenda mbele kuhakikisha matukio ya ajali yanapungua kwa kiasi kikubwa au yanakwisha.

Kinyume chake, alianza kwa kumshusha cheo aliyekuwa Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, Leopold Fungu. Siyo kwa maana ya kumwondolea madaraka tu, bali daraja la kijeshi, kutoka kuwa mrakibu wa polisi hadi kubaki mrakibu msaidizi. Uamuzi huo aliutoa Julai 6, mwaka huu. Siku nne baada ya kuapishwa.

Lugola alimshusha pia cheo Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto Kagera, George Mrutu. Uamuzi huo aliufanya kwa kumpa maagizo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Jacob Kingu. Kangi alisema, alipanga kuwafukuza kazi Fungu na Mrutu, ila bahati yao siku hiyo alikuwa anasherehekea kuzaliwa kwake.

Kwanza ni ile kuwa na haraka ya kufanya uamuzi bila kuchunguza kiini. Baada ya kumshusha cheo Fungu, ajali Mbeya ziliendelea. Pili ni kwamba nchi haiwezi kuendeshwa na hisia za viongozi, kwamba mtu anashindwa kufanya uamuzi kwa sababu siku husika ni Ijumaa na yeye alizaliwa Ijumaa. Haitakiwi kuwa hivyo. Uongozi wa nchi unapaswa kuzingatia utawala wa sheria.

Hiyohiyo Julai 6, Lugola alimtimua kwenye kikao aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Dk Juma Malewa, kisa alichelewa kuingia kwenye ukumbi wa mkutano kwa dakika moja zaidi. Kabla ya hapo, waziri huyo aliagiza kuwa ikifika saa 5:00 asubuhi, mlango ufungwe na asifunguliwe yeyote.

Saa 5:01, Dk Malewa aliingia ukumbini, Lugola akafoka: “Huyo ni nani anafunguliwa mlango wakati nimeagiza mlango ufungwe. Hakuna kuingia kwenye kikao changu.” Dk Malewa akaomba radhi, Lugola akaongeza: “Hakuna msamaha hapa, rudi nje.”

Hilo ni tukio mbele ya vyombo vya habari. Taarifa za baadaye zilieleza kwamba Dk Malewa alifika eneo la mkutano kuanzia saa 3:00 asubuhi lakini kikao kiliahirishwa mpaka saa 4:00 asubuhi. Kikaahirishwa tena mpaka saa 5:00 asubuhi.

Ilielezwa kwamba baada ya kikao kuahirishwa saa 4:00 asubuhi, Dk Malewa alikwenda kwenye ofisi nyingine zilizopo ndani ya jengo hilohilo la Wizara ya Mambo ya Ndani, ndipo alichelewa kwa dakika moja. Hivyo, Kangi kama angevuta subira, angetambua kwamba Dk Malewa hakuchelewa.

Julai 13, mwaka huu, taarifa ya Ikulu, ilieleza kuhusu uteuzi wa Kamishna Jenerali mpya wa Jeshi la Magereza, Phaustine Kasike aliyechukua nafasi ya Dk Malewa ambaye amestaafu. Hivyo ni vizuri kumshauri Lugola awe na subira katika uchukuaji wa uamuzi. Bila subira unaweza kuumiza wasio na makosa.

Pamoja na wito wa subira, kitu muhimu ni staha. Unapokuwa kiongozi haimaanishi wale wa chini yako ni watoto na unaweza kuamua chochote dhidi yao. Kuheshimiana ni jambo muhimu mno. Hata kama Dk Malewa angechelewa dakika 10, alipaswa kutumia hekima kuliko kumtoa nje mbele kamera na vinasa sauti vya vyombo vya habari.

Ilani ya CCM

Lugola alipofanya kikao na wakuu wa majeshi ya usalama ambavyo vipo ndani ya wizara yake, alimtaka kila mmoja aoneshe ilani ya CCM ya 20150-2020. Alisema, alipowaita aliwaambia kikao ni cha kazi, hivyo walipaswa kwenda kwenye mkutano na ilani ya CCM.

Ni kweli kuwa CCM ndiyo ilishinda Uchaguzi Mkuu 2015. Na kwenye uchaguzi CCM walinadi ahadi zao ambazo zimo ndani ya ilani yao. Ni vizuri pia kumpongeza Lugola kwa kuheshimu ahadi za chama chake kwa wananchi, kiasi cha kuahidi kutembea na ilani popote anapokwenda, kisha akaomba hata akifa azikwe nayo.

Hata hivyo, Lugola anapaswa kukumbushwa kuwa majeshi ya nchi hayatembei na ilani za vyama. Hata watumishi wa umma hawatakiwi kubebeshwa ilani za vyama. Badala yake, ahadi zote ndani ya ilani, hupaswa kupitishwa bungeni, zile zenye kuhitaji kutungiwa sheria, Bunge litunge na kutoa kibali cha utekelezaji.

Baada ya Bunge kutunga sheria, zinaingizwa kwenye utekelezwaji au yale yote yaliyotolewa idhini na Bunge, yanatekelezwa kama maagizo ya kiserikali, wala si ya chama.

Waziri anaweza kutoa maagizo kwa majeshi kwa niaba ya Rais, vilevile Rais ana mamlaka kamili ya kuyaagiza majeshi moja kwa moja.

Rais anapotoa maagizo kwa majeshi, nafasi yake inakuwa kama Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu. Rais hatoi maagizi kama mwenyekiti wa chama cha siasa. Uwepo wa vyama vya siasa ni utamaduni tu wa kidemokrasia kupata viongozi wa kuongoza dola. Utaratibu huo hauhusishi majeshi.

Lugola na mawaziri wengine, wakuu wa mikoa na wilaya, wao wakibeba nakala za ilani ya uchaguzi ya CCM ni sawa, maana wao nafasi zao ni za kisiasa. Majeshi hayapokei maagizo ya kisiasa bali ya kiserikali. Hivyo, siku nyingine Lugola asiwahoji wakuu wa majeshi yaliyo kwenye wizara anayoiongoza kuhusu ilani.

Masuala mengine

Lugola ameagiza mabasi yasizuiwe kutembea usiku na ametaka biashara na shughuli zote za kiuchumi ziendelee usiku na mchana. Hili pia anastahili pongezi. Maana nyakati hizi ambazo dunia inaelekea uchumi wa saa 24, haivutii kuona biashara zinafungwa usiku kisa usalama. Basi kutoka Kigoma, linafika Morogoro saa 4 usiku, linazuiwa kufika Dar es Salaam mpaka ifike saa 12 asubuhi.

Pamoja na hayo, ipo kauli iliyokosa utu kutoka kwa Lugola. Ni kuhusu kupotea kwa mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda. Waziri alipoulizwa kuhusu mkakati wa kumtafuta, alijibu kuwa wizara yake haishughuliki na mtu aliyeamua kutoweka kwa sababu zake za kimaisha.

Azory alichukuliwa na watu waliokuwa kwenye gari aina ya LandCruiser nyeupe Novemba mwaka jana. Tangu alipochukuliwa, polisi hawajaeleza nini wamekiona kwenye uchunguzi wao. Lugola alivyojibu ni kama ama alijua kila kitu kuhusu kutoweka kwa Azory kabla hajawa Waziri wa Mambo ya Ndani au alishapewa ripoti. Sasa kama hiyo ripoti ipo kwa nini haitolewi ili Watanzania waujue ukweli?

Lugola anapaswa kufahamu kuwa kupotea kwa Azory na kada wa Chadema, Ben Saanane, aliyetoweka tangu Novemba mwaka juzi, ni suala nyeti. Watu hao ni Watanzania, familia zao zinawahitaji, wananchi wenzao wanautaka ukweli. Wana haki za kuishi na kufanya kazi zao kama watu huru. Siyo sawa kutoa majibu utadhani kupotea kwao si suala la mguso kwa nchi.