Kassongo asema unapoficha ukweli uandishi unakuwa na walakini

Wiki iliyopita tulianza kutoa makala inayohusu mahojiano yaliyofanywa kati ya gazeti hili na mtangazaji nguli, Hamza Kassongo kuhusu alivyotangaza tukio la Uhuru wa Tanganyika Desemba 8 na 9, 1961.

Kassongo ni maarufu kupitia kipindi chake cha kwenye televisheni cha “Hamza Kassongo Hour” kinachoendesha mijadala inayoshirikisha wanasiasa, wachumi na wataalamu mbalimbali kuhusu masuala ya ndani na nje ya nchi.

Kipindi hicho hurushwa hewani na kituo cha Channel Ten kila Jumapili saa 3:00 usiku na mara nyingi Kassongo huonekana amevalia tai ndogo au bow tie, wakati mwingine pamoja na mikanda maarufu ya cross belt. Leo tunaendelea na sehemu nyingine ya makala hiyo ya ana kwa ana...

Swali: Unatofautishaje vyombo vya habari vilivyopo sasa vya Serikali na wakati ule TBC ikiwa huru?

Jibu: Kuna sura mbili, kwanza kuna baadhi ya wana habari walioko kwenye vyombo vya habari vya Serikali wenye uthubutu kusema bila kupiga nyundo pale ambapo Serikali imekosea. Ni wachache sana, ukiniambia nikutajie mmoja simkumbuki.

Wengi, ama ni kwa kutambua au kwa kutokujua au kwa makusudi wamekuwa wakisifia sifia tu. sisi tulikuwa tukisema kile kinachotokea, iwe ni kibaya au kizuri.

Hao ndiyo maadili ya uandishi wa habari, unapoficha ukweli uandishi wako unakuwa na uwalakini.

Swali: Unaonaje vyombo vya habari kwa sasa, je vimemezwa na Serikali?

Jibu: Kusema vyombo vya habari vimemezwa na Serikali ni kuionea Serikali kabisa. Mimi nimefanya kipindi cha Hamza Kassongo Hour kwa karibu miaka 20 sasa. Kama msimamo wangu ulivyo nimekuwa nasifia sana na nilikuwa nashutumu sana.

Moja ya watu waliokuwa wakija kwenye kipindi changu ni Tundu Lissu wakati ule yuko Leat, chama cha mazingira. Tulifanya mambo mazuri. Nikawaambia watu ni kuionea Serikali kusema kuwa imemeza vyombo vya habari na nikajitolea mfano wangu mwenyewe.

Nimefanya kazi na marais watatu, Mzee Mwinyi (Rais mstaafu Ally Hassan), Mzee Mkapa (Rais Mstaafu Benjamin) na Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Siku zote sikuwa nafanya vipindi vya kuwasifia. Kuna vipindi vingine nilikuwa nazungumza maneno ambayo pengine siyo ya kuudhi lakini siyo ya kufurahisha.

Wote hawa kwa bahati nzuri wananifahamu binafsi, hasa Rais Benjamin Mkapa ambaye tumeanzia mbali. Lakini hata siku moja siku pigiwa simu na yeye mwenyewe au mfanyakazi wake kusema hapo umefanya nini.

Kwa hiyo kuna uhuru wa vyombo vya habari. Kitu kilichotokea sasa ni mambo mawili. Kwanza, ninyi waandishi wa habari wenyewe mmedhani kwamba Serikali haitaki tufanye hivi, kwa hiyo ndiyo mnajikosoa wenyewe.

Sisi tulifanya, mimi nilifanya katika vipindi vyangu, marais hao waliopita.

Pili, umahiri wa kufanya kazi umepungua, kwa sababu ukiwa mahiri na unajiamini huwezi kuogopa. Ukikosa umahiri labda kwa kukosa elimu au kukosa uthubutu. Ndipo itabidi katika taarifa zako utababaisha.

Swali: Waswahili wanasema ukiona mtu anaogopa unyasi ujue ameshang’atwa na nyoka. Kuna mambo mengi yamewaogopesha waandishi wa habari kiasi cha kujikosoa wenyewe. Kuna waandishi wa habari wameuawa na vyombo vya dola, wengine wamepotea. Pengine wewe ulikuwa na urafiki binafsi na hao watawala?

Jibu: Hapana. Hiyo nazungumza kwa sababu ni mimi, vituo vya habari vingine pia vilifanya na wengine pia walifanya.

Lakini huo mfano ulioutoa ni kweli, kina Mwangosi (Daudi) na Jeshi la Polisi na siyo tuhuma kwa sababu mhusika alishitakiwa. Absalom Kibanda sasa ni chongo, lakini sasa hiyo ni tuhuma, ni Serikali au majambazi? Azory (Gwanda) amepotea, lakini nayo ni tuhuma kwamba ni Serikali au watu wasiojulikana.

Lakini kama unavyosema kwamba wahariri nao wanapata vitisho, mimi sasa ndiyo ningeacha kazi.

Swali: Kwa nini uache usionyeshe uthubutu?

Jibu: Umesema mtu akiguswa na unyasi anaogopa, sasa na mimi ningeogopa. Ningeacha uhariri.

Swali: Sasa turudi kwenye uhuru, unadhani yale yaliyosemwa siku ile ya Desemba 9, 1961 yametimizwa?

Jibu: Hapana. Kwa sababu kaulimbiu tuliyokuwa tunaambiwa ni maadui watatu ambao ni maradhi, umasikini na ujinga. Bado vipo.

Swali: Huoni kwamba idadi ya watu imeongezeka, watakwambia shule zimejengwa hospitali zimejengwa?

Jibu: siyo kwamba maendeleo hayapo, yapo tena makubwa tu, lakini hayakidhi matakwa na matamanio. Kwa sababu inatakiwa mtoto akienda shule atoke kama ilivyokuwa zamani, anakuwa ameiva.