Kigogo ACT aibuka, amshauri JPM mambo matatu

Katibu Mkuu wa ACT- Wazalendo, Doroth Semu

Katibu Mkuu wa ACT- Wazalendo, Doroth Semu ametaja mambo matatu ambayo atamshauri Rais John Magufuli endapo ikitokea akakutana naye.

Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi, kuhusu mambo mbalimbali na miaka mitatu ya Magufuli madarakani, Doroth alisema mambo hayo ni pamoja na kuilea demokrasia ya kweli nchini, kufanyia kazi ushauri na serikali kukubali kukoselewa.

“Rais ndiyo anapaswa kuwa mlezi wa demokrasia endapo yeye ataionyesha kwa mtazamo hasi watendaji wengine hawawezi kuifanikisha,” alisisitiza Doroth.

Jambo jingine ambalo angependa kumshauri Rais, ni kuyafanyia kazi mpungufu yanayoelezwa na wapinzani kuhusu serikali na utawala wake badala ya kuona ni masuala ya binafsi.

“Awe kiongozi, afahamu kwamba wanachokifanya wapinzani ni utaratibu wa kujaribu kunyoosha baadhi ya mambo ambayo wanaona hayaendi.

“Suala la mwisho ningemshauri jinsi anavyoshughulikia masuala ya wanawake; hapa nazungumzia kauli zake na teuzi mbalimbali anazozifanya. Mara kwa mara amekuwa akifanya uteuzi bila kuzingatia nafasi sawa ya mwanamke,” alieleza.

Dorothy alisema kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake kilichokuwa na changamoto kubwa kwa vyama vya upinzani pengine za kuliko awamu nyingine zilizopita.

“Kama tulikuwa tunakimbia sasa unaweza kusema tumerudi nyuma, upinzani umebanwa, watu hawana uhuru tena; wana hofu lakini kikubwa ni kuogopa kufuata ndoto zao na kuziacha zifutike.

Katibu huyo alienda mbali zaidi na kusema hali hiyo imesababisha hata ndugu na jamaa wa karibu za wapinzani kuogopa, kuwaonea huruma kwa hali wanayopita hivyo kuwaonya waachane na masuala ya siasa.

Kwa mujibu wa Doroth, kuna athari kubwa wanazopata kutokana na demokrasia kutofuatwa kikamilifu katika kipindi hiki ambacho wamezuiwa kufanya mikutano ya siasa.

Moja ya athari hizo, alisema ni vyama vya siasa kupoteza wanachama kwa kuwa na hofu ya kujiunga nao.

“Mfano mzuri ni chama chetu cha ACT wakati kinaanzishwa tulijiwekea malengo ya kuongeza wanachama lakini mpaka sasa hatujayafikia lengo,” alisisitiza Doroth bila kusema ni kwa asilimia ngapi.

Alisema athari nyingine ni watu kutovutiwa na masuala ya siasa lakini pia kukosekana na ukosoaji unaojenga kwa kuwa tu wanachosema kinachukuliwa tofauti.

Kwa upande wa sekta ya uchumi, kiongozi huyo alisema kukua uchumi kunakoelezwa hakuakisi hali halisi ya maisha ya Mtanzania wa kawaida na kwamba hali kwa wananchi wa kipato cha kawaida imezidi kuwa ngumu kutokana na bei ya bidhaa kuwa juu.

“Ajira hakuna, viwanda, makampuni na biashara zimefungwa vijana wanahangaika kusaka ajira bila mafanikio, matokeo yake tutatengeneza bomu ambalo siku yoyote litalipuka na kusababisha uhalifu kuongezeka,” alisema.

Alisema nyingine ni kwa upande wa elimu ambako mpaka sasa bado changamoto ni zilezile ingawa elimu inatolewa bure.