Kiki na muziki wa enzi zetu

Siku chache zilizopita nilipigiwa simu na mtangazaji kutoka luninga mojawapo maarufu, alikuwa ananialika kuwa mmoja wa wazungumzaji katika kipindi ambacho maada ingekuwa ni utamaduni wa ‘kiki’.

Mjadala huo ulikuwa uwe pia na wanamuziki kadhaa wa Bongo Fleva na nilialikwa ili kuongea kuhusu utamaduni huo enzi nilipokuwa mwanamuziki kijana.

Kichwa changu kikaanza kuchemka kujaribu kukumbuka Je, enzi zile ‘kiki’ ilikuwaje? Labda kwanza nieleze kwa wepesi ‘kiki’ ni nini.

Neno hili limechukuliwa kutoka neno la Kiingereza ‘kick’ lenye maana teke. Hapa likiwa na maana kujipiga au kupigwa teke ili usogee mbele, na kwa sababu ni teke, kuna maumivu kiasi lakini muhimu ni ‘kurushwa mbele’. Kabla sijajipanga vizuri kimawazo, nikapigiwa tena simu kuwa watayarishaji wameona kipindi chao hakihitaji ‘mtu wa zamani’.

Nikashukuru kwani wahenga walisema akunyimae mbaazi kakupunguzia…… Lakini nikaona hebu leo niandike kuhusu suala hili la ‘kiki’. Nimejaribu kukumbuka kama kulikuwa na jina lililokuwa likitumika wakati huo kuelezea utamaduni huu, sikuweza kukumbuka, lakini nilikumbuka matukio kadhaa ya enzi hizo ambayo unaweza kuyaweka kundi la kuyaita ‘kiki’.

Wakati kundi la muziki la Boney M lilipoanza kupoteza umaarufu, ilienea habari kuwa kundi hilo lilipata ajali ya ndege na wanamuziki wote kufariki.

Muda mfupi baada ya hapo ndipo wakatoa kibao chao cha Boonoonoos. Habari zilizokuja patikana baadae ni kuwa meneja wao alitunga hiyo hadithi ya kifo ili kuongeza mauzo ya santuri yao hiyo.

Kwa sababu ya upatikanaji habari kutoka nje ya nchi wakati huo ulikuwa mgumu, tulisikia fununu kuwa huko Ulaya kuna machezo wa wanamuziki kujitangaza wamekufa ili kuongeza mauzo ya santuri zao. Mchezo wa kujitangaza kufa haukufanyika hapa kwetu, nadhani wote tunajua utamaduni wetu unavyo tufundisha kutokutania kifo.

Wakati wa ujana wangu wangu wanamuziki walikuwa katika vikundi na wachache sana waliokuwa mmoja mmoja kama sasa, hivyo vituko vya mwanamuziki mmoja mmoja havikutegemewa kusaidia umaarufu wa kikundi. Tabia zilizokuwa kinyume cha maadili kama vile ulevi na umalaya hazikushabikiwa kabisa, na wanamuziki waliweza hata kufukuzwa kutoka kwenye vikundi ikionekana tabia zao za aina hiyo zilikithiri.

Nakumbuka tukio moja ambapo wasichana wawili waimbaji walilewa kupindukia na wanaume waliokuwa nao wakawanyoa nywele na hivyo kuamka vipara asubuhi.

Bendi yao iliwasimamisha kazi siku hiyohiyo, mpaka nywele zilipoota. Wanamuziki wengi wanaume nawakumbuka waliofukuzwa bendi kwa ulevi, ugomvi na vituko vya aina hiyo.

Bendi hazikutegemea ‘kiki’ kupata umaarufu, bali kujitahidi kupiga muziki mzuri. Pengine jambo jingine lililofanya kusiwepo na ‘kiki’ kama za siku hizi ni kutokuweko na vyombo vya habari vyenye kushabikia matukio hayo.

Chombo pekee cha utangazaji kilikuwa Radio Tanzania Dar es Salaam, chombo hicho hakikuwa na nafasi ya kutangaza mambo ya binafsi ya wanamuziki, labda ndoa au kifo. Hivyo wananchi walikuwa wakisikia kazi mbalimbali za wanamuziki na kuwapenda kwa kazi zao na si vituko nje ya muziki. Magazeti yalikuwa yakiandika mengi kuhusu wanamuziki, lakini yalikuwa yakiongea kuhusu ufanisi wao katika muziki si vituko vyao.

Kulikuwa na staha sana kuhusu maisha binafsi ya watu. Gazeti moja kutoka Kenya lililoitwa Baraza, lilikuwa na ukurasa maalumu wa vituko vya mjini, katika ukurasa wake wa pili wa gazeti hilo, ukurasa uliokuwa unaendeshwa na mwandishi aliyeitwa Khamis Khamis, ukurasa alioupa jina Panapofuka Moshi, ndio lilikuwa gazeti pekee la Udaku, baadhi ya vichwa vya habari vilikuwa kwa Naizi Afumaniwa, Taiti ya Kisura Yachanika Night Club, Naizi Asahau Pijo 404 Bar au Lofa Ashindwa Kulipa Bili Bar na kadhalika, hawa wanaoitwa Vigogo siku hizi, wakati huo walikuwa wakiitwa Manaizi.

Hii ilitokana na sera ya Waafrika kuchukua nafasi za wazungu mara baada ya Uhuru kitu kilichoitwa Africanization, hawa waliochukua nafasi za wazungu wakaitwa Manaizesheni au kifupi Manaizi. Kutokana na hadithi hizo za Manaizi, visura na kujitapikia Bar, gazeti hilo likapigwa marufuku.

Aina ya malezi pia ilikuwa tofauti sana , hivyo mambo mengi ambayo siku hizi yanaonekana ni kawaida yalikuwa ni mwiko kabisa kuonekana au hata kuongelewa hadharani.

Nitoe mfano wa juzijuzi tu, kuna video mbili zimesambaa katika makundi ya whatsapp zikiwaonyesha wanamuziki wawili maarufu wakiimba matusi machafu mbele ya umati wa watu wa mashabiki, bila wasiwasi kitendo hicho kingefanyika enzi ya ujana wangu, wanamuziki hawa wangebebwa na wapenzi wa muziki moja kwa moja mpaka kwenye usalama wakalale mahabusu, siku hizi inaitwa ‘kiki’ na mashabiki walikuwa wanashangilia.

Naweza kusema kwa uhakika kuwa ‘kiki’ ni kitendo kinachoonyesha kuwa mwanamuziki ameshindwa kutengeneza muziki bora.