Kipa mpya Liverpool amvuruga Klopp

Muktasari:

  • Alisson amejiunga na Liverpool katika usajili wa majira ya kiangazi na juzi alipewa nafasi ya kusimama katika milingoti mitatu.

Jurgen Klopp amesifu kiwango bora cha kipa Alisson Becker muda mfupi, baada ya Liverpool kuichapa Napoli mabao 5-0.

Alisson amejiunga na Liverpool katika usajili wa majira ya kiangazi na juzi alipewa nafasi ya kusimama katika milingoti mitatu.

Klopp alisema mchezaji huyo aliyetua kwa Pauni65 milioni kutoka AS Roma, ndiye kipa namba moja katika kikosi chake msimu ujao. Alisson alicheza kwa kiwango bora mchezo huo ukiwa ni wa kwanza tangu alipojiunga na klabu hiyo yenye maskani Anfield.

Mchezaji huyo ameingia katika rekodi ya kuwa kipa ghali zaidi katika mashindano ya Ligi Kuu England.

Kipa huyo alifanya mazoezi kwa siku tano kabla ya kupewa jukumu la kuikabili Napoli katika mchezo uliochezwa mjini Dublin.

Liverpool ilitawala mchezo kwa dakika zote tisini mbele ya mashabiki 51,512 waliojitokeza kushuhudia mchezo huo.

“Ni mchezaji bora. Kila mmoja ameshangaa kumuona akicheza kwa kiwango bora katika mchezo wa kwanza, amezoea haraka mazingira,” alisema kocha huyo wa zamani wa Borussia Dortmund.

Pia alisema mchezaji James Milner alicheza kwa kiwango bora akiwa chachu ya mafanikio ya kikosi hicho katika mchezo huo. Milner alianza kuifungia Liverpool bao la kwanza kabla ya Georginio Wijnaldum kuongeza bao la pili kwa mpira wa kichwa.

Mshambuliaji nyota na nahodha wa Misri, Mohamed Salah aliweka wavuni bao la tatu kabla ya Daniel Sturridge kuongeza jingine na Alberto Moreno alifunga bao la tano. Timu hizo zipo katika ziara ya michezo kujiandaa na msimu mpya.