HOJA BINAFSI: Kituko…Mshtuko…Mlipuko…Mkurupuko… Kituko

Muktasari:

  • Lakini baada ya barabara kutengenezwa sawasawa na lami iliyofaa, ghafla majini yakatoweka, ajali zikatoweka tukarudia hali yetu ya kawaida. Kumbe kilichohitajika tu kilikuwa lami imara, jambo ambalo lingegundulika iwapo watu wangefanya utafiti kwanza kabla ya kukurupuka na kumtafuta mchawi ambaye wala hakuwepo.

Nakumbuka, kabla ya kutengenezwa kwa barabara ya Hayati Waziri Mkuu kuelekea nchi ya kaskazini mwa Afrika, huko bondeni kulikuwa na ajali nyingi. Mpaka watu wakashtuka, wakalipuka kwa hasira, wakakurupuka kufanya maombi maalum, eti lile eneo lilifahamika kuwa na majini majiniasi wa kusababisha ajali.

Lakini baada ya barabara kutengenezwa sawasawa na lami iliyofaa, ghafla majini yakatoweka, ajali zikatoweka tukarudia hali yetu ya kawaida. Kumbe kilichohitajika tu kilikuwa lami imara, jambo ambalo lingegundulika iwapo watu wangefanya utafiti kwanza kabla ya kukurupuka na kumtafuta mchawi ambaye wala hakuwepo.

Na, kama kawaida, lawama zilimiminiwa kwa watendaji, yaani madereva. Sasa sijui, baada ya kutengeneza lami ghafla madereva shetani waligeuka malaika.

Jambo hilohilo linaonekana mara nyingi katika sehemu ya makutano ya barabara. Wakati hakuna taa za kuongoza, kila mtu anajitia mjuaji hadi wote wanakwama. Mashetani kabisa. Lakini hebu weka taa za barabarani, kwisha ushetani.

Tatizo hilo si kwa madereva tu. Kimsingi Serikali na wamiliki wa daladala wana mgogoro uliodumu kuliko mgogoro kati ya Ethiopia na Eritrea maana Serikali inatafuta kupendwa kwa kuwalazimisha wenye magari yao binafsi wale hasara kwa niaba ya Serikali na wenye daladala hawaoni kwa nini wao, peke yao, katika sekta binafsi, watolewe kafara kwa faida ya Serikali.

Matokeo yake ni nini?

Wanafunzi wengi sana wameumia, wengi wamenyanyaswa kijinsia, ugomvi kila siku lakini tunabaki tunawalaumu makonda wa daladala kana kwamba ni wao waliotengeneza bifu yote hii. Walaumu watendaji, watie hata ndani ili mradi chanzo cha tatizo kisionekane.

Mambo ni yaleyale kwenye sera kibao. Tengeneza sura ya sera yenye ahadi kibao, matibabu bure, elimu bure, n.k. Matokeo yake, zahanati au kituo cha afya hawana glovu za kuwasaidia akina mama wajifungue.

Lakini ole wake daktari anayejali usalama aamue kufanya mpango binafsi kutatua hili tatizo. Atamwagiwa kila aina ya tusi na lawama, hawapendi watu, mpinzani wa Serikali, mchochezi, lakini yeye alikuwa chanzo cha tatizo. Vivyohivyo mwalimu mkuu akiamua kuwachangisha wazazi kwa sababu ruzuku imechelewa.

Sikatai. Wapo madaktari, au wauguzi, au walimu wakuu ambao wametumia mwanya huu kuwaiga wale wa juu zaidi kufaidika na pengo katika mfumo lakini hii haiondoi kwamba, kimsingi, shida si watendaji bali ahadi isiyotekelezwa au kutekelezeka.

Na wakati wa matokeo wa mitihani, duara hili linapamba moto kweli. Matokeo kituko. Yaleta mshtuko, mlipuko, mkurupuko, watendaji wanatolewa kafara kisha tunasinzia tena hadi matokeo yajayo.

Mara kubadilisha mfumo wa matokeo na kubuni vipimo visivyokuwepo, mara nini sijui, ili mradi lawama isitupwe kwenye mfumo.

Juzi tu, mstaafu mmoja alikubali ukweli kwamba kuna haja ya kuwa na mjadala kitaifa kuhusu hali ya hatari katika elimu, wacha watu watoe povu chovu kuuliza kwa nini anasema sasa.

Kwa nini hakusema huko nyuma

Kweli, kwa nini hakusema huko nyuma lakini hii haiondoi hoja kwamba elimu iko kwenye kitengo cha wagonjwa mahututi.

Sasa kama Christopher alivyomwambia Obi katika Hamkani si Shwari Tena (No Longer at Ease) mimba haifichwi na mkono.

Matokeo, hasa ya shule moja iliyokuwa maarufu sana yamekuwa kituko … mshtuko … mlipuko … mkurupuko. Na wa kwanza kulaumiwa ni walimu. Utafiti uko wapi? Wasichana wameulizwa kulikoni? Wazazi? Walimu wenyewe?

Tumeangalia hali ya miundombinu ya shule? Tumeangalia hali ya miundombinu ya kwenda na kurudi shuleni. Mimi nakaa upande wa pili wa daraja la baba wa taifa na kuna wasichana wako barabarani saa kumi na moja asubuhi kila siku kwenda shuleni.

Na wanarudi gizani. Watasoma saa ngapi? Hata darasani hawatashindana na usingizi kutokana na kukosa usingizi wa kutosha wakati wako katika umri wa kukua haraka?

Mimi sisemi hii ndiyo sababu kuu lakini kama wengine wanakurupuka, kwa nini nisikurupuke na mimi? Labda sababu kuu ya Dar es Salaam kushika mikia kila siku ni matatizo ya usafiri.

Labda hiii ni sababu mojawapo ya wazazi ambao wangependa kukaa na watoto wao na kufuatilia maendeleo yao wao wenyewe, na wafaidi watoto wao kabla hawajakua na kukimbia nyumba na kuanza kujenga maisha yao, labda usafiri unachangia wazazi kuamua kuwapeleka watoto wao shule za bweni katika mikoa mingine ili mikoa mingine ionekane wanafanya vizuri kuliko Dar es Salaam.

Labda … Sijui … lakini wewe pia hujui na wale pia hawajui. Tunakurupuka pamoja na kutoa povu chovu ya kuwalaumu watendaji kama kawaida. Paza sauti …

Tatizo ni walimu? Fukuza walimu, hamisha walimu, walimu wasikae shule moja zaidi ya miaka mitano. Mkuu wa shule yenye matokeo mabovu atumbuliwe, tena hadharani tuweze kumtupia mawe.

Tatizo ni watoto

Watoto wa siku hizi Bwana. Walevi wa insta na kasheshe zote zingine. Hebu fikiria, wakati wanasubiri basi saa nzima na zaidi, wanaangalia simu zao. Simu ni sumu. Bla bla bla. Hatujui kwamba watoto katika shule zilizofaulu sana nao wana Insta.

Mara nyingine sikatai, wapo vijana ambao wamekuwa walevi wa simu zao lakini kuona kwamba simu ndiyo chanzo cha matatizo yote ni kuangalia juujuu tu. Mikoani wana simu, kwa nini hawakufeli hivyo?

Ndiyo maana nakumbuka msemo muhimu wa wanazuoni na watu wenye mamlaka ya kufanya maamuzi. No utafiti, no haki ya kusema. No uchambuzi wa kina, no haki ya kubwata.

Bila utafiti na uchambuzi wa kina tutabaki kukurupukia vituko mwaka nenda rudi, na kuwatolea watendaji kafara lakini tatizo litabaki palepale.

Tunaweza kusifu kweli hatua nzuri ambazo zimechukuliwa kuboresha shule lakini matokeo yanatuambia kwamba mambo baaaado.

Bila kusahau kwamba kuna siku nyingine tutauliza, kweli matokeo ndiyo elimu. Mbona tunaangalia matokeo tu? Kuna shule ambazo karibu wawageuze watoto misukule maana ni kitabu kitabu kitabu tu. Kukariri weee … kitabu bila michazo, kitabu bila sanaa, kitabu bila burudani.

Tunataka watoto wa aina hii? Na tutashangaa watoto wakiasi baada ya kutoka kwenye kiwanda cha kitabu cha aina hiyo? Tunataka nini upande wa elimu? Watoto wetu wanataka nini? Tuwaulize, tujadili, tuondokane na duara ya ko … ko … ko …