#WC2018: Kombe la Dunia la babu na wajukuu

Muktasari:

  • Tangu kuanza kwa fainali hizi 1930, kuna vibabu vitano vimecheza na Hadary kaongezeka mwaka huu kuwa wa sita. Kuna kipa wa Italia, Dino Zoff kacheza Kombe la Dunia akiwa na miaka 40 miezi minne na na siku 13. Hiyo ilikuwa mwaka 1982.

Kuna huyu kipa wa Misri, Essam El-Hadary ana miaka 45, ameweka rekodi kiboko kawashinda hata waliomtangulia kucheza Kombe la Dunia.

Tangu kuanza kwa fainali hizi 1930, kuna vibabu vitano vimecheza na Hadary kaongezeka mwaka huu kuwa wa sita. Kuna kipa wa Italia, Dino Zoff kacheza Kombe la Dunia akiwa na miaka 40 miezi minne na na siku 13. Hiyo ilikuwa mwaka 1982.

Kuna huyu kipa wa England, Peter Shilton kacheza Fainali za Kombe la Dunia 1990 akiwa na miaka 40 na alisimama langoni England ikilala 2-1 kwa Italia mechi ya mshidi wa tatu.

Kibabu kingine ni kipa wa zamani wa Ireland ya Kaskazini, Arsenal na Tottenham Hotspur, Pat Jennings alisimama langoni timu yake ikipigwa 3-1 na Brazil fainali za 1986 zilizofanyika Mexico akiwa na miaka 41.

Pia yupo mshambuliaji wa Cameroon, Roger Milla, alicheza fainali za 1990 akiwa na miaka 42 mwezi mmoja na siku nane. Alipiga mabao ya kutosha na kuifkisha mbali Cameroon.

Kipa wa Colombia, Faryd Mondragon alikuwa kwenye fainali za 2014 akiwa na miaka 43 na siku tatu.

Funga kazi ni fainali za mwaka huu. Huyu ni kipa wa Misri, Essam El-Hadary (45) ameweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kucheza Kombe la Dunia nchini Urusi,

Huyu amewazidi wachezaji wote, lakini sasa unaweza kusema babu anacheza na wajukuu au wanawe. El-Hadary anacheza na nyota ambao wanacheza fainali hizo wakiwa na nusu ya umri wake.

Nyota hao walikuwa hawajazaliwa kipindi ambacho, Essam alipoanza kucheza soka la kulipwa nchini kwao kwenye klabu ya Damietta SC mwaka 1991, akiwa na miaka 18.

Spoti Mikiki inakuletea nyota 20 ambao wanacheza fainali hizo, lakini walikuwa hawajazaliwa kipindi ambacho mkongwe Essam alipoanza kucheza soka kwenye timu ya vijana ya Damietta SC kabla ya miaka miwili baadaye kupandishwa.

Albert Gudmundsson

Gudmundsson ambaye yupo kwenye timu ya taifa la Iceland, alizaliwa Juni 15, 1997. Mwaka huo ambao alizaliwa winga huyo wa PSV ya Uholanzi, Essam alikuwa amejiunga na Al Ahly SC baada ya kuichezea, Damietta SC kwa miaka mitatu.

Kinda huyo mwenye miaka 20, alianza soka lake kwenye akademi ya PSV na kufunga mabao 28 katika michezo 63 ya timu hiyo upande wa wachezaji wa akiba na hatimaye akapandishwa kwenye kikosi cha kwanza na kucheza michezo tisa kabla ya kuitwa timu ya taifa.

Gudmundsson amekuwa na mwanzo mzuri kwenye kikosi cha timu yake ya taifa la Iceland kwa kufunga mabao matatu katika michezo mitano aliyocheza ya ushindani.

Amine Harit

Amine ambaye ni Mmorocco, alizaliwa Juni 18, 1997 kipindi hicho Essam alikuwa na miaka 24, kinda huyo amechipukia kwenye akademi ya Nante nchini Ufaransa.

Hakudumu kwenye akademi hiyo na baadaye akajiunga na Schalke ya nchini Ujerumani ambako amefanya vizuri kwa kucheza jumla ya michezo 29 ya Ligi Kuu nchini humo ambayo ni marufu kama Bundersliga.

Kiungo huyo ambaye alikuwa akihusishwa kuichezea timu ya wakubwa ya Ufaransa kutokana na kulichezea taifa hilo ngazi ya vijana, ameamua hivi karibuni kuitumikia Morocco na tayari amecheza mechi tatu za ushindani.

Bassem Srarfi

Siku ya mwisho ya usajili wa Januari kwa mwaka jana barani Ulaya, Bussem ambaye alizaliwa Juni 25, 1997 alijiunga na Nice akitokea nyumbani kwao, Tunisia kwenye klabu ya Africain.

Kiungo huyo mara baada ya kutua Ufaransa alienda na kucheza jumla ya michezo 37 katika mashindano yote naye ni miongoni mwa wachezaji wenye umri mdogo kwenye mashindano ya kombe la Dunia hakuzaliwa huyo wakati Essam ameanza kucheza soka.

Bassem alianza kuichezea timu ya taifa ya Tunisia mwezi Machi mwaka huu kwa kucheza michezo kadhaa ya ushindani.

Rodrigo Bentancur

Rodrigo wa Uruguay , alizaliwa Juni 25, 1997 ni miongoni mwa wachezaji 23 ambao wanaunda kikosi cha taifa hilo katika michauno yab kombe la Dunia nchini Urusi ambayo tamati yake itakuwa Julai 15.

Kiungo huyo ambaye amejiunga na Juventus ya Italia msimu uliopita akitokea Boca Juniors ya Argentina amekuwa kwenye kiwango bora ambacho kimemfanya kuitwa mara kwa mara kwenye timu yake ya taifa.

Kiungo huyo ambaye amepata nafasi ya kucheza jumla ya mechi 27 za mashindano yote kwenye msimu wake wa kwanza nchini Italia, kiwango chake kimefanya kuitwa kwenye timu ya taifa ya Uruguay ambayo ameichezea mechi sita.

Kasper Dolberg

Ajax inajivunia sana kumuibua, Dolberg ambaye alizaliwa Oktoba 10, 1997 kwenye akademi yao na kuwa mshambuliaji wa kutumainiwa kwenye kikosi hicho toka apandishwe 2016.

Mshambuliaji huyo wa Kidemark amefunga jumla ya mabao 32 kwenye michezo 77 ya mashindano yote.

Dolberg ameitwa mara nne tofauti kwenye timu ya tafa lake ambalo pia linamshambuliaji mwenye asili ya Tanzania, Yussuf Poulsean anayecheza soka la kulipwa Ujerumani kwenye klabu ya RB Leipzig.

Nikola Milenkovic

Mserbia Nikola alizaliwa Oktoba 12, 1997 baada ya kuwa na msimu mzuri akiwa na Partizan Belgrade, Nikola alijiunga na timu ya Serie A, Fiorentina msimu uliopita.

Beki huyo wa kushoto, amecheza michezo 16 ya Ligi Kuu Italia na tangu ameanza kuitwa timu ya taifa lake mwaka 2016, hii ni mara yake ya tatu ambayo ni ya kwanza kuitwa kwa ajili ya Kombe la Dunia.

Hamza Mendyl

Beki wa kushoto wa Lille ya Ufaransa, Hamza ambaye akizaliwa Oktoba 21, 1997 ni Mmorocco alianza kuichezea klabu yake hiyo kuanzia mwezi Februari mwaka jana.

Beki huyo mwenye miaka 20, ameichezea timu yake ya taifa michezo 13 ya michuano mbalimbali na mara yake ya kwanza ilikuwa kwenye michezo ya kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika ndani ya mwezi Aprili, 2016.

Edson Alvarez

Mmexico Edson mwenye miaka 20, alizaliwa Oktoba 24 anaichezea klabu ya nyumbani kwao, America ambapo tangu apewe nafasi ya kucheza mchezo wake wa kwanza, 2016 alipata namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza ambapo ampaka sasa amecheza jumla ya mechi 67.

Beki huyo amekuwa akipata nafasi ya kuanza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza cha timu ya taifa la Mexico na anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuifungia bao Mexico katika mashindano.

Marcus Rashford

Mshambuliaji wa Manchester United, Rashford naye ni kijana ambaye atalitumikia taifa lake la England katika mashindano ya Kombe la Dunia naye alizaliwa wakati huo kipa wa Misri akiendelea kutesa kwenye soka.

Rashford ambaye alizaliwa Oktoba 31, 1997 aliingia kwenye kikosi cha kwanza cha Manchester United, 2016 alifunga mara mbili kwenye michunao ya Europa Ligi na baadaye akafunga tena mara mbili dhidi ya Arsenal.

Kinda huyo, amecheza jumla ya michezo 123 kwenye kikosi cha Mancheter United na amefunga jumla ya mabao 32. Amekuwa akipewa nafasi ya kucheza kwenye Kombe la Dunia na hivi karibuni aliifungia England bao kwenye mchezo dhidi ya Costa Rica.

Luka Jovic

Luka aliyezaliwa Desemba 23, 1997 ameingia mkataba wa miaka miwili na klabu yake ya Benfica. Mshambuliaji huyo alikuwa akiichezea Eintracht Frankfurt kwa mkopo.

Kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha Benfica ndio sababu iliyomfanya Luka kwenda kwa mkopo Eintracht Frankfurt ambako amekuwa akipata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.

Toka mwaka 2016, Luka ameichezea timu yake ya taifa ya Serbia michezo 48 na katika michezo hiyo amefunga jumla ya mabao 13 na amefunga pia mabao nane kwenye Bundesliga ndani ya michezo 22.

Lee Seung-woo

Mkorea Kusini, Lee Seung-woo alizaliwa Januari 6, 1998 kipindi hicho , Essam alikuwa ametimiza mwaka wake wa pili kwenye klabu yake ya pili kuichezea ya Al Ahly SC nchini Misri.

Msimu uliopita Lee Seung-woo alijiunga na klabu ya Italia, Hellas Verona akitokea Barcelona, lakini alitua kwa Waitaliano hao kwa kipengele kinachosema endapo akihitajika atasajiliwa bila pingamizi lolote.

Ismaïla Sarr

Winga wa Senegal, Ismaila alianza kuichezea Rennes ya Ufaransa mwaka 2017 mara baada ya kuondoka FC Metz akiwa na miaka 18, kinda huyo alizaliwa Februari 25, 1998. Winga huyo wa kimataifa wa Senegal, ameichezea klabu yake michezo 24 ya Ligi Kuu Ufaransa na kufunga mabao matano.

Ian Smith

Beki wa kulia wa IFK Norrkoping, Ian ambaye ni raia wa Costa Rica ameichezea michezo mitatu klabu hiyo ambayo amejiunga nayo mwanzoni mwa mwaka huu.

Aliingia katika mchezo wa maandalizi ya Kombe la Dunia dhidi ya England na walipoteza kwa mabao 2-0.

Jose Luis Rodriguez

Jose baada ya mkataba wake kumalizika akiwa kwa mkopo, Gent ya Ubelgiji aliamua kujiunga na klabu hiyo moja kwa moja, Disemba 2016, Mpanama huyo alizaliwa Juni 19, 1998.

Kiungo huyo mwenye miaka 19, alikuwa akicheza timu ya taifa lake la Panama kabla ya kujumuishwa kwenye orodha ya wachezaji watakao litumikia taifa hilo katika mashindano ya Kombe la Dunia ambayo hufanyika kila baada ya miaka minne.

Moussa Wague

Beki wa kuliwa wa Eupen ya Ubelgiji, Moussa ambaye alizaliwa Oktoba 4, 1998 amecheza jumla ya mechi 28 msimu uliomalizika kwenye klabu yake ambayo inshiriki ligi moja na KRC Genk anayoiochezea nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta.

Trent Alexander-Arnold

Kinda Trent ni beki wa Liverpool ambaye alizaliwa Oktoba 7, 1998, kinda huyo amefanya vizuri msimu uliopita na kuwa chaguo la kwanza kwenye kikosi hicho.

Francis Uzoho

Kipa wa Nigeria, Francis ambaye ni chaguo la pili kwenye timu ya Deportivo La Coruna ya Hispania nyuma ya Ruben Ivan Martínez, alizaliwa Oktoba 28, 1998 kipindi hicho, Essam alikuwa tayari ameshinda mataji matatu.

Mataji hayo yalikuwa ni Klabu Bingwa kwa Waarabu mara moja ambapo ilikuwa mwaka 1996 na kombe la ufunguzi wa michuano hiyo mara mbili kwenye miaka ya 1997, 1998.

Francis aliweka rekodi akiwa na miaka 18 ya kuwa kipa mchezaji mdogo zaidi wab kigeni kucheza mchezo wa Ligi KUU Hispania maarufu kama La Liga.

Achraf Hakimi

Mmorocco, Hakimi ni beki wa kulia wa Real Madrid ambaye amekuwa chaguo wa pili nyuma ya Dani Carvajal ambaye amekuwa akitumika mara kwa mara kwenye nafasi hiyo.

Beki huyo ambaye alizaliwa Novemba 4, 1998 alipandishwa kikosi cha kwanza baada ya kufanya vizuri kwenye kikosi cha wachezaji wa akiba.

Kinda huyo mwenye miaka 19, alifunga bao lake la kwanza kwenye La Liga katika mchezo dhidi ya Sevilla mwezi Disemba mwaka jana.

Kylian Mbappe

Mbappe aliyezaliwa Desemba 20, 1998 ni mchezaji bora chipukizi wa Ligi Kuu Ufaransa, alikuwa mchezaji wa kwanza wa kikosi cha Monaco pindi alipokuwa na umri wa miaka 16.

Alijiunga na Paris Saint-Germaine msimu uliopita na amefunga mabao 21 kwenye mashindano yote, kinda huyo aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa pili ghari Duniani nyuma ya mchezaji mwenzake wa timu hiyo, Neymar.

Daniel Arzani

Mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kwenye kKombe la Dunia, Urusi ni, Daniel ambaye alizaliwa Januari 4, 1999. Kiungo huyo anaichezea Australia katika mashindano hayo.

Arzani, ameichezea Melbourne City michezo 20 msimu huu na ameitwa mara mbili kwenye timu hiyo ya taifa ambayo wiki iliyopita alifunga bao lake la kwanza dhidi ya Hungary.