Kuna sababu 1,000 za kuwashirikisha ‘diaspora’ katika ujenzi wa Taifa

Rais Jakaya Kikwete akibonyeza kitufe kuzindua Mtandao wa mawasiliano(website)ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi wakati wa mkutano February 2014 Jijini Dar es salaam.Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Neno hili likimaanisha Watanzania waishio nje ya nchi lilianza kuzoeleka katika vipindi vya serikali za awamu ya tatu na nne.

Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi alipata kutueleza kuwa kila zama ina kitabu chake. Kwa miaka ya nyuma neno ‘diaspora’ lilikuwa geni katika masikio ya Watanzania wengi.

Neno hili likimaanisha Watanzania waishio nje ya nchi lilianza kuzoeleka katika vipindi vya serikali za awamu ya tatu na nne.

Ni katika awamu ya tatu tulipoanza kusikia kwa msisitizo umuhimu wa diaspora katika kuendeleza nchi yetu. Ulikuwa ni wakati ambapo shughuli zinazohusiana na mambo ya nje na diplomasia zilikuwa chini ya waziri wa wa mambo ya nje wakati huo, Jakaya Kikwete.

Si ajabu kwamba suala la diaspora kujulikana lilipata kasi katika serikali ya awamu ya nne, ikiongozwa na Rais Kikwete huyohuyo.

Katika kipindi cha serikali ya awamu ya nne, neno lilitoka katika misamiati na kuwa la kawaida ambalo Watanzania wengi wanaweza kulielezea.

Hata hivyo hali ilikuwa tofauti kwa majirani zetu wa Uganda na Kenya ambako kwa miaka mingi nchi hizi zimekuwa zikifaidika na ushiriki wa raia wao wanaoishi nje katika ujenzi wa nchi zao.

Kwa mwaka 2015, nchi za Afrika ya Mashariki zilipokea zaidi ya dola za Marekani 3.5 bilioni kutoka kwa diaspora wao kwa ajili ya uwekezaji.

Kenya inaongoza kwa kupata sehemu kubwa ya fedha zinazotokana na diaspora ikifuatiwa na Uganda. Nchi hizi mbili kwa pamoja zinapata zaidi ya 75% ya fedha zinazokuja Afrika ya Mashariki kutoka kwa kwa raia wake walioko nje ya nchi.

Mchango kwa Tanzania

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kikanda akiwa bungeni hivi karibu, Tanzania hupokea wastani wa dola za Marekani 456.5 milioni kwa mwaka kutoka kwa raia wake walioko nje.

Pamoja na kupata sehemu ndogo tu ya mchango wa diaspora katika nchi za Afrika Mashariki, hatuna budi kuishukuru serikali ya awamu ya nne kwa juhudi zake kubwa katika uhamasishaji wa diaspora kushiriki katika ujenzi wa nchi yetu.

Katika kipindi hicho tulishuhudia kuanza kutambulika kwa diaspora kama mojawapo ya vyanzo vikuu vya uwekezaji na upatikanaji wa fedha za kigeni.

Tulianza kusikia na kuzifahamu jumuiya za Watanzania waishio katika nchi mbalimbali. Utambuzi wao ulikuwa pia katika uongozi wa juu wa nchi yetu ambapo Rais Kikwete alijiwekea utaratibu wa kukutuna nao katika ziara zake za nje ya nchi.

Utambuzi huo uliwafanya Watanzania hao waanze kuweka mikakati ya kuwekeza nchini mwao. Tulishuhudia misaada ya kibinadamu na shughuli nyingi za kiuwekezaji na uwezeshaji wa Watanzania, hasa wasanii, uliokuwa ukiratibiwa na diaspora wetu.

Kazi aliyoifanya Rais Kikwete imeweka msingi wa maana kwa nchi yetu kufaidika na uwepo wa Watanzania nje ya nchi.

Nafasi ya Tanzania

Pamoja na kuwa nyuma ya jirani zetu katika kufaidika na mchango wa diaspora katika ujenzi wa nchi, Tanzania bado ina nafasi kubwa ya kufaidika na mchango wa diaspora kwa kuangalia fursa nyingi tulizonazo na ambazo wanaweza kushirikishwa.

Tuna vivutio vingi vya utalii, tuna madini, ardhi ya kilimo, fursa ya kuanzisha viwanda, mazao ya kilimo na misitu yanayoweza kuuzwa nje ya nchi, na hata uendelezaji wa miundombinu.

Kwa kuchukulia mfano wa nchi kama Rwanda, suala la sera na sheria zinazowavutia diaspora kuwekeza nchini mwao ni muhimu sana. Pamoja na sera na sheria zinazovutia uwekezaji, suala la uhamasishaji kama alivyofanya Kikwete linaongeza hamasa kwa Watanzania wenzetu kushiriki katika ujenzi wa nchi yao.

Tumeona uwekezaji uliofanywa na diaspora kwa kununua nyumba 108 kutoka Shirika la Nyumba (NHC) badala ya kuzifaidisha nchi za ugenini.

Suala hili linatukumbusha kuwa ikiwa kutakuwa na fursa nzuri kwa dispora kuwekeza nyumbani kwao, wanaweza kufanya mambo makubwa zaidi kwa uzalendo wao na kutambua kuwa Tanzania ni nyumbani.

Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli imetoa kipaumbele kwa mabalozi wetu kuhakikisha wanaitangaza Tanzania na kuhamasisha uwekezaji.

Suala hili ni muhimu likaangaliwa kwa mtazamo wa uhamasishaji wa diaspora wetu pia. Upimaji wa mafanikio yake uwe na kigezo cha jinsi mabalozi wetu walivyofanikiwa kuongeza uwekezaji wa diaspora.

Mabalozi wapimwe mafanikio yao si tu kwa kuangalia uwezeshaji wao katika uwekezaji uliofanywa na wageni bali, pia na diaspora kama kundi linalojitegemea. Diaspora tayari ni mabalozi wetu huko nchi za nje na kama watapewa nafasi inayostahili wanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi yetu.

Hawa ni Watanzania na inakuwa rahisi kwao kuwa na mwamko wa kuwekeza nyumbani kutokana na mahusiano ya kinasaba na nchi yao. Bado wana hamu ya kuona Tanzania ikibadilika, zaidi ya sababu za kibiashara na faida tu, kama ilivyo kwa wawekezaji wageni. Uhusiano wao wa kinasaba na Tanzania unawafanya wajitume na kuhakikisha Tanzania inafaidika kwanza na si vinginevyo.

Diaspora walio wengi hawahitaji kufundishwa hili, bali kuwekewa mazingira mazuri ya kuleta mitaji na uwekezaji nchi mwao. Hawana wasiwasi na hisia za hatari zitokanazo na uwekezaji nje ya nchi, kama ilivyo kwa wawekezaji wageni, maana wanawekeza nyumbani na wao ni sehemu ya Watanzania.

Tanzania ni kwao maana babu, bibi, mama, baba, kaka, dada, wajomba, shangazi na marafiki zao ni Watanzania na wako Tanzania.

Si vibaya tukajifunza kwa jirani zetu sababu zilizowafanya wakafanikiwa kuvutia ushiriki wa diaspora wao kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa nchi zao.

Nina hakika yako mengi ya kujifunza na kurekebisha hapa na pale ili watoto hawa wa Kitanzania wawe na hamasa zaidi ya kuwekeza nyumbani.

Mabalozi na wizara zinazohusika na hilo wawe wabunifu ili kuweka mazingira rafiki na yenye upendeleo kwa diaspora maana ni Watanzania.

Ukiliangalia kwa makini hili neno diaspora unaweza kusema kuwa wawekezaji wa kigeni hapa Tanzania watakuwa na tabia ya ‘u-diaspora’. Yaani, niwekeze Tanzania ili nchi ninayotoka ifaidike.

Diaspora wa Kitanzania ataliona hili kwa jicho tofauti kuwa niwekeze nyumbani ili Tanzania yangu ifaidike. Hivyo, kumwezesha diaspora wa Kitanzania kuwekeza nyumbani unafaidika kwa asilimia 100, wakati wawekezaji wageni nao wanahitaji kupeleka kwao pia hiyo faida.

Diaspora vs wawekezaji wa kigeni

Sipingi uwekezaji wa wageni hapa Tanzania bali unaonyesha faida kubwa kwa nchi ikiwa tutahamasisha uwekezaji wa diaspora wetu.

Hivyo ni wazi kuwa diaspora lazima wapewe upendeleo kupitia mfumo unaoeleweka na unaojitegemea wa uratibu wa shughuli zao hapa nchini na katika balozi zetu, wapate masharti rafiki ya uhamishaji wa mitaji kuja nchini kuleta fedha za kigeni tofauti na wageni.

Diaspora wapate uhamasishaji na uwezeshaji wa uwekezaji usio na urasimu na vizingiti visivyo vya lazima kwa kutambua kuwa ni Watanzania na pia watambuliwe na kushirikishwa katika uandaaji na utekelezaji wa mipango yetu ya Maendeleo.

Catherine Magige ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM)