Kutana na mchuuzi wa nazi aliyefikiria nje ya boksi

Muktasari:

  • Mmoja wa watu ambao imekuwa ni fursa kwa ajira kwao ni Ester Batolemeo mfanyabiashara wa nazi katika soko la Buguruni Jijini Dar es Salaam.

Teknolojia imerahisha mambo mengi kufanyika kwa urahisi, japokuwa wapo wanaosema inapunguza ajira lakini kwa wengine ni fursa ya ajira kwao.

Mmoja wa watu ambao imekuwa ni fursa kwa ajira kwao ni Ester Batolemeo mfanyabiashara wa nazi katika soko la Buguruni Jijini Dar es Salaam.

Ester mwenye miaka 38, anasema alianza kazi ya kuuza nazi miaka 15 iliyopita katika soko hilo la Buguruni.

Mojawapo ya wateja wake wakubwa anasema ni mama Lishe ambapo wakati mwingine ili kutowapoteza ilibidi awakunie kabisa.

Hata hivyo ni hivi karibuni alipata nyenzo ya kumuwezesha kufanya kazi hiyo nayo si nyingine ni mashine maalum kwa ajili ya kukunia nazi.

Mashine hiyo inayotumia umeme sasa imemsaidia kupata hadi oda za hotelini za kuwakunia nazi ukiachilia mbali mama Lishe wake.

Mama huyo anasema kupitia mashine hiyo kwa siku hukuna nazi zisizopungua 1,000 huku gharama ya nazi moja anauza Sh800 na kukuna kwa Sh100.

Kwa hiyo kwa mteja atakayeenda kwake kununua nazi pamoja na kukuniwa itamlazimu kutoa Sh900 jambo ambalo anasema limemsaidia kuongeza wateja kwa kuwa shughuli ya kukuna nazi moja kwa mashine hiyo haizidi hata dakika moja.

Pia, uzuri mwingine mashine hiyo anasema haitumii umeme kwani kwa siku hutumia unit moja tu kwa nazi zote ambazo amekuwa akipewa kuzikuna.

Akizungumza na gazeti la mwananchi, Ester ambaye ni mama wa watoto wawili anasema tangu amepata mashine hiyo sasa ameanza kuwaza kuwa na eneo lake kwa ajili ya kufanyia shughuli hiyo tu.

“Unajua kwa miaka yote 15 nauza nazi hapa sokoni tena kwa kupanga chini, lakini mashine hii imenifanya nifikirie nje ya box kwamba nami nahitaji kuwa na frame yangu kwa kuongeza mashine nyingine ambazo zitanisaidia kuifanya kazi hii ya kukuna nazi kwa ufanisi zaidi.

“Kwani kwa sasa naifanyia kwenye baraza ya fremu ya mtu, ambapo kwa mwezi nalipia Sh40,000 fedha ambayo naamini nikijiongeza nakuwa nami na fremu yangu,”anasema.

Katika kufanikisha hilo, anasema tayari ameshanunua baadhi ya vifaa na anachohitaji sasa hivi ni Sh500,000 kwa ajili ya kujenga mindombinu ya fremu aliyoipata na kuanza kazi.

Anasema fremu hiyo itakapokamilika ataajiri na mtu mwingine wa ziada na hivyo atakuwa amezalisha ajira nyingine mpya.

Wito wake kwa kina mama anawashauri wasibweteke na kutumia kila fursa wanaoiona mbele yao na kujitolea mfano yeye kuwa mashine hiyo alioona kwa mmoja wanawake na hivyo kufanya jitihada za kuitafuta inapopatikana.

Japokuwa mama huyo hakumpa ushirikiano wa wapi inapatikana lakini aliulizia watu wengine hadi akahakikisha anaipata.