Kwa nini Wapinzani wameshindwa kuzitumia mahakama kudai haki?

Muktasari:

  • Pamoja na malalamiko hayo, upande wa pili kuna mwanya wa kisheria ambao wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaona unaweza kuwasaidia mahakamani kupata haki wanazolalamikia.

Kila kukicha kuna malalamiko lukuki ya vyama vya upinzani nchini kuhusu kupokwa haki zao mbalimbali. Ni malalamiko yanayoelekea kuzoeleka.

Pamoja na malalamiko hayo, upande wa pili kuna mwanya wa kisheria ambao wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaona unaweza kuwasaidia mahakamani kupata haki wanazolalamikia.

Hata hivyo, kwa muda mrefu, vyama hivyo vinaonekana ama kushindwa, kupuuza, kukwama kutumia fursa hiyo, badala yake vinaishia kulalamika kwa matamko yasiyo na nguvu kisheria, bali yaliyojaa hitaji la kuonewa huruma.

Miongoni mwa malalamiko ya vyama vya upinzani hasa katika awamu ya tano ni katazo la kufanya mikutano ya hadhara na maandamano, masuala ambayo ni halali kwa mujibu wa Katiba na sheria ya vyama vya siasa.

Mwanasiasa anayekumbukwa kwa kuisumbua Serikali mahakamani ni Mchungaji Christopher Mtikila, ingawa hata yeye baadhi ya masuala aliyoyashinda mahakamani, mfano suala la mgombea binafsi, hadi sasa hajapatikana.

Ni kutokana na mfano wa Mtikila, wadau wa siasa wanadhani hata wapinzani wanaweza kuitumia mahakama katika harakati zao za kisiasa.

Wakili wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke anasema bado vyama vya upinzani havijafanya juhudi kama za Mtikila kudai haki zao.

“Mchungaji Mtikila ametoa mchango mkubwa katika sheria zetu kutokana na kesi zake. Mahakama bado ni chombo kinachoaminika, naona bado wapinzani hawajaitumia ipasavyo,” anasema Dk Kyauke.

Kumbukumbu ya Mtikila

Mchungaji Mtikali aliyefariki alifajiri ya Oktoba 4, 2015 kwa ajali ya gari iliyotokea katika Kijiji cha Msolwa, Chalinze Mkoa wa Pwani, alikuwa mwenyekiti wa Chama cha DP.

Umaarufu wa Mtikila aliyezaliwa mkoani Iringa mwaka 1950 ulianza tangu miaka ya 1990 kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuongea, upinzani wake dhidi ya muundo wa Serikali ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar na madai yake kuhusu hujuma za uchumi zinazofanywa na raia wa kigeni.

Miongoni mwa kesi zake zilizoinyima Serikali usingizi ni ile ya mgombea binafsi, ambapo hatimaye Mtikila aliibwaga Serikali

kuanzia Mahakama Kuu hadi Mahakama ya Rufaa ambayo ikiwa chini ya majaji saba ilibatilisha hukumu hiyo. Hata hivyo, Mtikila alikwenda hadi Mahakama ya Afrika na kushinda.

Mtikila alitoka mbali na kesi hiyo ambapo tangu mwaka 1992 mfumo wa vyama vya upinzani ulipopitishwa, Serikali ilikataa suala la mgombea binafsi.

Ndipo mwaka 1993 Mtikila alipofungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma iliyosikilizwa na Jaji Kahwa Lugakingira ambaye alikubaliana na hoja zake, kwamba kugombea kama mtu binafsi ni haki ya kila raia kwa mujibu wa Katiba, kwa maana ya haki ya kuchagua viongozi na haki ya kugombea uongozi.

Lakini, katika hali ya kushangaza mwaka 1994, Serikali ilipeleka bungeni marekebisho ya mabadiliko ya 11 ya Katiba katika Ibara ya 34 kwa kuzuia wagombea binafsi.

Ndipo mwaka 2005, Mchungaji Mtikila alifungua kesi Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam akipinga marekebisho hayo ya Katiba. Hatimaye, jopo la majaji watatu chini ya Jaji Kiongozi, Amiri Manento lilikubali hoja za Mtikila na kuruhusu tena mgombea binafsi.

Hata hivyo, mwaka 2010 Serikali ikikata rufaa katika Mahakama ya Rufaa. Majaji saba wa mahakama hiyo walisikiliza kesi hiyo chini ya aliyekuwa Jaji Mkuu, Augustino Ramadhani. Serikali ilidai katika rufaa yake kwamba hakuna mahakama yoyote nchini yenye uwezo kisheria kusikiliza kesi inayotaka mgombea binafsi na kwamba mahakama za chini zilijipachika madaraka ya kibunge ya kutunga sheria badala ya kuzitafsiri.

Katika hukumu iliyokosolewa na wengi, mahakama hiyo, pamoja na kukubaliana na hoja ya haki ya kila raia kuchagua au kuchaguliwa bila kuwa mwanachama wa chama cha siasa, ilisema siyo jukumu la mahakama kujielekeza katika masuala ya kisiasa.

Ndipo Mchungaji Mtikila alikata rufaa katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu iliyoko Arusha na Juni 2013, mahakama hiyo ilitoa ushindi kwa mrufani na kuitaka Serikali ya Tanzania kutoa taarifa ndani ya miezi sita kuhusu namna inavyotekeleza hukumu hiyo.

Kesi nyingi alizowahi kufungua dhidi ya Serikali ni pamoja na wananchi wa Tanzania bara kuruhusiwa kwenda Zanzibar bila pasi na vyama vya siasa kuruhusiwa kufanya mikutano bila kuomba kibali cha mkuu wa wilaya au polisi.

Wengine wanaonaje mahakama?

Licha ya mtazamo huo, baadhi ya vyama vya siasa, mfano Chadema, inaonyesha tayari imeshafungua kesi kadhaa ikipinga kuzuiwa kufanya mikutano na maandamano tangu utawala wa awamu ya tano uingie madarakani, japokuwa haijapata mafanikio makubwa.

Kesi ya kwanza ilikuwa Na.79 ya mwaka 2016, iliyofunguliwa na kusimamiwa na mawakili watatu Gasper Mwanalyela, John Mallya na Paul Kipeja katika Masijala ya Mwanza.

Chadema walifikia hatua hiyo baada ya Jeshi la Polisi kusambaratisha mkutano wao uliokuwa ufanyike Kahama mwaka huo, ambapo mabomu ya machozi na magari ya ‘washawasha’ vilitumika kuwaondoa wafuasi wa chama hicho waliokuwa wasikilize hotuba za viongozi wa kitaifa.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwaambia waandishi wa habari jijini Mwanza kuwa wamefungua kesi hiyo baada ya kuona demokrasia ya vyama vingi inabakwa.

Mbowe aliwataja watu wanne waliotajwa katika kesi hiyo ya madai ni Kamanda wa Polisi wilayani Geita, Kamanda wa Polisi wilayani Kahama, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa polisi (Makao Makuu) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Hata hivyo, Chadema ililazimika kuiondoa kesi hiyo mahakamani baada ya kubainika mapungufu ya kisheria katika hati yao ya mashtaka.

Jaji Mohamed Gwae aliyepangwa kusikiliza shauri hilo alitaja upungufu ya kisheria uliobainika kwenye hati ya mashtaka ya Chadema kuwa ni pamoja na kumjumuisha katika hati ya mashtaka Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Mssanzya, ambaye kisheria alistahili kufunguliwa mashtaka katika Masjala Kuu jijini Dar es Salaam.

“Baada ya kushauriana na mawakili wa Chadema kuhusu suala hilo, waliamua kwa hiari yao kuondoa kesi yao kwa ajili ya kuifanyia marekebisho hati yao ya mashtaka,” alisema Jaji Gwae alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Akifafanua, Jaji huyo alisema Chadema wana njia mbili za kurekebisha kasoro hiyo; moja ni kufungua shauri hilo katika masjala kuu ya mahakama jijini Dar es Salaam ili kuendelea kumshtaki Kamishina Mssanzya au kuendelea na shauri hilo jijini Mwanza dhidi ya wakuu wa polisi wa wilaya za Maswa, Kahama na Geita bila kumjumlisha Kamishna wa operesheni.

Chadema hawakuishia hapo, bali ilifungua shauri Na.52/2016 kuhusu uhalali wa tamko la Jeshi la Polisi kuzuia maandamano na mikutano ya hadhara, undani wa kesi hiyo umebainika.

Shauri hilo lilisikilizwa na Jaji Kiongozi Ferdinand Wambali ambapo Baraza la Udhamini la Chadema lilikuwa likitetewa na Peter Kibatala dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Inspekta Jenerali wa Polisi.

Hata hivyo, shauri hilo nalo lilitupwa kwa hoja zilizojengwa na mawakili wa Serikali wakiongozwa Haruni Matagane, Daniel Nyakeha na Lilian Machange.

Wakili Matagane alipinga maombi ya Chadema lililotaka mahakama ipitie upya na kufuta amri ya Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano yasiyo na kibali, kwamba ombi la Chadema limewasilishwa kwa namna isiyo sahihi kwa mujibu wa kifungu cha 43(6) cha Sheria ya Jeshi la Polisi (The Police Force and Auxiliary Service Act).

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Sheria ya Jeshi la Polisi inaeleza kuwa kabla ya kupinga amri ya Polisi ya kuzuia mikutano na maandamano ni lazima kwanza wahusika wawasilishe rufaa yao kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, suala ambalo Chadema haikulifanya.

Katika hoja ya pili, mawakili wa Serikali walitaka Chadema iwasilishe ombi la mapitio likiwa na kiapo kinachojulikana kisheria kama ‘statement’. Mawakili wa Chadema waliwasilisha kiapo hicho lakini kilikuwa batili kwa sababu ya kusainiwa na chama badala ya wadhamini wa Chadema.

Jaji Wambali alikubaliana na mawakili wa Serikali na kutupilia mbali shauri hilo.