Kwanini sheria hairuhusu mtoto kuajiriwa mfanyakazi nyumbani?

Muktasari:

  • Kwamba mtoto mwenye umri wa kuanzia miaka 14 ana haki ya kufanya kazi lakini aajiriwe kufanya ‘kazi nyepesi’ na kupata malipo stahiki.

Japokuwa sheria zinazolinda maslahi ya mtoto hapa Tanzania zimeainisha juu ya haki ya mtoto kufanya kazi ili kumuandaa kujitegemea pindi awapo mtu mzima. Vilevile zimeweka ukomo wa umri na hata aina ya kazi ama ajira anazoweza kupewa mtoto.

Kwamba mtoto mwenye umri wa kuanzia miaka 14 ana haki ya kufanya kazi lakini aajiriwe kufanya ‘kazi nyepesi’ na kupata malipo stahiki.

Tafsiri ya kazi nyepesi inakufanya mhalifu wewe mwajiri wa mtoto kama mfanyakazi za nyumbani. Kazi nyepesi ni zile ambazo haziathiri afya ya mtoto, hazikwamishi maendeleo yake kielimu au makuzi yake.

Mwajiri wa mtoto anapaswa kuzingatia kuwa kazi zake hazizidi masaa sita kwa siku huku ujira ukizingatia viwango visivyo vya kinyonyaji.

Tena sheria inataka mtoto asifanye kazi saa za usiku, yaani muda wowote kati ya saa mbili za usiku hadi saa kumi na mbili za asubuhi. Mfano akianza kazi saa moja asubuhi basi ikifika saa sita mchana siku yake inakuwa imekwisha.

Itakuwa nadra sana kumkuta mwajiri wa mtoto kama mfanyakazi za nyumbani akizingatia vigezo hivi, yaani kazi nyepesi na masaa sita tu kwa siku ukiachilia mbali swala la ujira usio wa kinyonyaji.

Nina imani hamtapingana nami kwamba familia nyingi zinapaswa kuwa mahabusu na pengine kufungwa kabisa pale tu wasimamizi wa sheria hizi watakapoamka.

Tunakubaliana kwamba ni vigumu kuwaajiri watoto wawe wafanyakazi za nyumbani kwani ajira za majumbani ni moja ya kazi hatarishi kwa watoto ambazo huwalazimu kuamka alfajiri na kulala usiku sana huku muda wote wakitekeleza majukumu lukuki yaliyopo nyumbani.

Utafiti mdogo tuliofanya umeonyesha kuwa waajiri wengi huzingatia sana kigezo cha umbile la mwili kwa kutazama kwa macho tu hususan urefu ama unene wakati wa kuwaajiri watoto hasa wa jinsia ya kike huku kigezo cha umri kikitupiliwa mbali.

Hili ni kosa kwani wakati mwingine hujikuta wakiajiri hata watoto wenye umri wa chini ya miaka 14 pasipo kujua ama vinginevyo.

Inasikitisha sana kuona wimbi kubwa la watoto wakiingizwa kwenye ajira za majumbani ambapo idadi yao huongeezeka kila kukicha huku wengi wao wakikatishwa masomo na ndoto zao.

Rai yetu kwa waajiri wote ambao tayari tunaishi na watoto hawa kama wasaidizi wetu wa kazi za nyumbani, huu ni wasaa wetu wa kujitafakari upya na kwa mapana zaidi huku tukijihakikishia kuwa hakuna walakini wowote juu ya wasaidizi wetu wa kazi za ndani kwa maana tumekidhi vigezo vyote vilivyoelekezwa kwenye sheria husika. Tuache kuishi kwa mazoea na tupendelee kutii sheria bila shuruti ili kuhifadhi rasilimali watu hasa watoto wadogo.

Wito wetu wa pili ni kwa wazazi wa watoto wanaoajiriwa. Hakikisha unamwachia mwanao kwenda kuanza kazi walau akiwa ametimiza miaka 18 kwani uwezo wake wa kumudu ajira hizi unakuwa mkubwa.

Kumbukeni umri na aina za kazi wanazofanya ni baadhi tu ya changamoto za ajira hizi. Zipo changamoto kama kugeuzwa mke mwenza na baba mwenye nyumba, kupigwa, kunyimwa chakula na hata kutukanwa na nyinginezo nyingi.

Ni vyema tukajenga nia na jitihada za makusudi katika kushirikiana juu ya kulinda na kuheshimu haki za watoto pamoja na utu wao. Ajira za watoto majumbani sasa basi!

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org