Licha ya miaka 57 ya uhuru bado wanasiasa wanadai demokrasia

Jumapili iliyopita Desemba 9, ilikuwa siku ya maadhimisho ya miaka 57 tangu Tanganyika ilipopata Uhuru. Siku hiyohiyo kwenye Hoteli ya Ledger Plaza, Bahari Beach, Kunduchi, Dar es Salaam, kulikuwa na mkutano wa vyama vya siasa visivyo na dola.

Vyama 10 vya siasa vilikutana Ledger Plaza ili kuunda nguvu ya pamoja, kuhakikisha muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa haupiti, kwa kile ambacho wanalalamikia kuwa endapo muswada huo utapita kuwa sheria, vyama vitakuwa havipo huru.

Kimsingi hoja ya vyama hivyo ni demokrasia. Wanalalamika kuwa siasa za vyama hazipo katika uwanja huru na sawa kati ya vyenyewe na kile kinachotawala, yaani CCM. Wanaona CCM kinatumia nguvu za dola kujipa upendeleo wa kisiasa.

Maswali mawili; miaka 57 baada ya Uhuru bado vyama vinadai demokrasia? Miaka 26 tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa bado hakuna utaratibu mzuri wa kufanya siasa katika uwanja sawa? Maswali hayo mawili yanatupeleka kwenye hili lingine; je, Uhuru maana yake nini?

Kwa tafsiri rahisi uhuru ni hali ya kujiamulia mambo bila shuruti au kivuli cha mamlaka nyingine. Uhuru ni kutokuwa kifungoni wala utumwani. Ni kufanya mambo yako kwa faida yako mwenyewe. Ni kujitegemea kifikra, kiuamuzi na kimatokeo.

Kabla ya Desemba 9, 1961, Tanganyika ilikuwa koloni la Uingereza. Kwa maana hiyo nchi haikuwa huru. Watanganyika walikuwa wanatawaliwa. Harakati za kudai huru zililenga kuwafanya Watanganyika wajitawale wenyewe. Baada ya uhuru kupatikana, miaka 57 baadaye bado inaonekana nguzo za uhuru hazipo mahali pake. Na hiyo ndiyo aibu kubwa.

Kwa nini ni aibu?

Taasisi ya kiraia inayoitwa Directory of Social Change (DSC), yenye makao yake makuu, Liverpool, Uingereza, katika chapisho lake la “Three Pillars of Independence”, yaani nguzo tatu za uhuru, mambo matatu yaliyoguswa ni;

Mosi ni uhuru wa siasa za vyama, pili ni uhuru wa tabaka la watu wa kawaida na tatu ni uhuru wa vyombo vya habari.

Maana yake ni kuwa kama hakuna uhuru kwenye siasa za vyama, tabaka la watu wa kawaida na vyombo vya habari, maana yake nchi inakuwa huru pasipo nguzo zake. Tunapaswa kujiuliza; ni sahihi kujivunia uhuru bila nguzo za uhuru?

Nguzo hizo tatu ndiyo alama ya demokrasia. Hivyo, ni sawa na kusema kwamba nguzo kuu ya uhuru ni demokrasia. Ikiwa miaka 57 imepita tangu Tanganyika ipate uhuru na bado kuna harakati za kudai demokrasia, unaweza kuona ni aibu kubwa kiasi gani inayolikumba taifa.

Turudi nyuma. Ndoto za waasisi wa Taifa hili wakati wa kudai uhuru ni ili kujitawala wenyewe. Na demokrasia ndiyo rutuba ya nchi kujitawala yenyewe. Malalamiko kuwa demokrasia inaminywa inalitia aibu Taifa kwamba baada ya kupata uhuru, watu hawajitawali, isipokuwa wanatawaliwa. Malalamiko kuhusu demokrasia ni kielelezo kuwa kuna tabaka linajiona linatawaliwa badala ya kujitawala.

Ugumu ni nini?

Uhuru wa makundi yote kwenye nchi ndiyo alama ya uhuru wa Taifa. Kuna wajibu mkubwa kwa walio madarakani kuhakikisha kila mwananchi anafurahia na anafaidi uhuru wa nchi yake.

Mkutano wa vyama vya siasa Ledger Plaza una lengo la kukwamisha muswada wa sheria mpya ya vyama vya siasa. Unaweza kujiuliza ni kwa nini waliotunga muswada huo hawakuzingatia haki za wengine ambao wanaona sheria hiyo ikipitishwa vyama havitakuwa huru?

Kuna katazo lilishatolewa la kufanya mikutano ya siasa wala maandamano. Wakati huohuo tumeona kuwa uhuru wa kukutana, kuhutubia na kupinga ni nguzo za uhuru wa watu. Uhuru wa siasa za vyama ni moja ya nguzo tatu za uhuru wa nchi. Je, wanaokataza au kutunga sheria hawajui nguzo za uhuru wa nchi na watu wake?

Ikiwa tunapenda kusherekea uhuru wa nchi bila aibu, basi inafaa kuangalia malalamiko yenye kuonesha kuwa kuna makundi ya watu hayana tabasamu na uhuru wetu.