Lugola: Kwa nini sitaachana na Ilani ya CCM hadi kaburini

Muktasari:

  • Amefikia hatua sasa anasema, Ilani ya CCM ni bora kuliko ya chama chochote na hata siku akifa, azikwe nayo.

Unaweza kujiuliza kwa nini kila anapokwenda, anapokuwa anatekeleza majukumu yake, haiachi Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2015/20. Si katika utekelezaji wa majukumu tu, hata akiwa ndani ya Bunge, ukifika wakati wa kwenda kujibu maswali yanayohusu wizara utamwona amebeba nyaraka kadhaa ikiwamo Ilani.

Amefikia hatua sasa anasema, Ilani ya CCM ni bora kuliko ya chama chochote na hata siku akifa, azikwe nayo.

Huyu si mwingine ni Kangi Lugola, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, aliyeshika wadhifa huo rasmi Julai 2 akiteuliwa kushika nafasi iliyoachwa na Mwigulu Nchemba. Alitokea katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) alikokuwa naibu waziri.

Lugola ambaye aliingia bunge katika Bunge la Kumi lililoongozwa Spika Anne Makinda na sasa Bunge la 11 chini ya Spika Job Ndugai, wiki iliyopita, Lugola alifanya ziara katika ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) zilizopo Tabata Relini jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine, alizungumzia Ilani anayoibeba kila anapokwenda. Lugola anasema hawezi kuachana nayo kwa sababu alikabidhiwa Ilani hiyo na Rais John Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2015 katika mkutano wa hadhara, mbele ya umati wa wananchi wilayani Bunda mkoa wa Mara. Anasema wakati anakabidhiwa Ilani hiyo mbele ya umma alijiuliza maswali mengi.

“Mheshimiwa Rais (Magufuli) alinikabidhi mbele ya uamati na kunieleza nihakikishe ninakwenda kuisimamia. Tangu nimekabidhiwa kitu hiki nilitafakari kwamba ni kitu ambacho nimekabidhiwa kuhakikisha kuwa muda wowote niko kuwatumikia Watanzania Ilani hii itakuwa kitendea kazi namba moja na kama fimbo ya kutembelea,” anasema.

Anaongeza, “Muda wote nikaamua kujua CCM imemwelekeza nini Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mimi ninayemsaidia napaswa kufanya nini. Na mimi kitabu hiki nakifanya kama rejea, kwa sababu muda wote nitakuwa kazini lazima nipate rejea kwa ajili ya kutekeleza.”

Lugola anakwenda mbali zaidi juu ya Ilani hiyo akisema, “Ningetamani siku nikifa, nizikwe na Ilani hii, ilani ya wakati huo itakayokuwapo kwani hakuna Ilani katika vyama vingine kama hii ya Chama cha Mapinduzi.”

Alipoulizwa kama siku moja angetamani kugombea urais, Lugola anasema, “viatu vya Magufuli vile kwangu ni oversize (vikubwa), kiatu kile sifikirii hata kuwa Rais, sasa kile kiatu mpaka upate fursa kuwatumikia si rahisi.”

Alivyopokea uteuzi

Lugola, baba wa watoto wanne, watatu wa kike na mmoja wa kiume anasema, siku ya uteuzi wa wizara ya mambo ya ndani Julai 1, alikuwa jimboni kwake Mwibara mkoani Mara.

“Ndipo nikapata taarifa za uteuzi, nilipopata taarifa nilifurahi kwa sababu Rais ambaye ni mkuu wa nchi, anapoonyesha imani kwako, kukutoa katika nafasi ndogo uliyokuwa nayo katika baraza lake na kukupeleka ngazi ya juu lazima utafurahi,” anasema Lugola.

Anasema lakini furaha inapokuja, inakuwa na mipaka na unajiuliza umepewa wizara hii na mambo yake nyeti, ina mambo gani na nakwendaje kuyatekeleza ili kile kilichomfanya akakuamini, unakwenda kukifanyaje ili usimwangushe yule aliyekuteua.

Akifafanua unyeti wa wizara hiyo anasema, taasisi zilizo chini ya wizara ya mambo ya ndani ni Zimamoto, Uhamiaji, Idara ya Wakimbizi, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Jeshi la Polisi na Magereza ambazo zinasimamia usalama na amani ya nchi.

Anasema amani, usalama na utulivu ukishakuwapo katika nchi, shughuli za wananchi zinaweza kufanyika, wananchi kushiriki katika imani zao unakuwapo, uwezekano wa wananchi kutoka huku kwenda kule unakuwepo.

“Yaani shughuli zote zinafanyika ni wizara hii na ndio maana Rais anapoapa kuilinda na kuihifadhi Katiba na hivi ndivyo vyombo vyake na mimi amenikabidhi, nihakikishe vinafanya kazi inavyotakiwa, hivyo sitaki kumuangusha,” anasema.

Azungumzia watu wasiojulikana

Katika mahojiano hayo, Waziri Lugola amesema kuanza sasa hatua zitaanza kuchukuliwa dhidi ya mtu yoyote anayeihusisha Serikali na watu wasiojulikana ili kuvisaidia vyombo vya dola katika uchunguzi. Anasema kila tukio linapotokea na watekelezaji wa matukio hayo, wanaposhindwa kuonekana jamii imekuwa ikiyahusisha matukio hayo na vyombo vya dola, na hivyo yeye hatataka Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli ipakwe matope.

“Kuanzia sasa, ikitokea matukio ya namna hiyo, ambao waliotenda tukio kimsingi hawajafahamika, halafu Mtanzania mwenzetu akasema hao wasiojulikana waliofanya tukio ni vyombo vya Serikali, Jeshi la Polisi popote mliko kamata kabisa huyo mtu kwa sababu anataka kuchonganisha Serikali na wananchi,” anasema Lugola.

Waziri huyo ambaye ni askari polisi mstaafu, anaongeza: “Nikiliacha hili likaendelea, likashamiri, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Magufuli itajulikana ni Serikali inayoua watu chini ya mwavuli huo.”

Waziri huyo anasisitiza, “kwa hiyo yeyote tu akisikika ama akitumia mtandao, huyu anayesema huyo anayesema ni vyombo vya Serikali atakamatwa kokote, iwe kwenye baa, starehe, atakamatwa tu kwani huo ni uchochezi.”

“Aje atuambie hao wasiojulikana ni vyombo vya Serikali, lazima akamatwe na atashughulikiwa,” anasema. Hata hivyo, alipoulizwa ni kesi ngapi ambazo Serikali imeshtaki za uchochezi na ikashinda, Lugola anasema duala la kutuhumu na kushinda au kushindwa ni vitu viwili tofauti. “Tusimaanishe, kama Serikali imechukua hatua kwa aliyefanya uchochezi halafu akashinda, tuache kukamatwa watu wanaochochea. Kutoshinda kesi tuliyoshtaki ya uchochezi, haiturudishi nyuma kukamata wale wanaoonyesha kufanya uchochezi,” anasema

Polisi kubambikiza kesi

Waziri huyo anakiri uwepo wa baadhi ya askari wanaolichafua Jeshi la Polisi kwa kuchelewesha upelelezi pamoja na kuwabambikia kesi baadhi ya wananchi, jambo ambalo anasema hatakubali kuona likiendelea.

“Ni kweli kwamba Jeshi la Polisi limekuwa likilalamikiwa kwamba linabambikiza kesi watu wake na hata mimi baada ya kuripoti, tuna kitengo cha malalamiko dhidi ya vyombo ninavyovisimamia na ninao ushahidi na uhakika kwamba baadhi ya askari wanabambikiza kesi watu,” anasema Lugola.

“Mimi nimekuja na eneo hili linapeleka kero kwa wananchi, wanaweza kuamini kwamba vyombo hivi ndivyo vinafanya hivyo. Nitakuwa mkali zaidi na yoyote atakayebainika kubambikizia mtu kesi, hakutakuwa na hiyo nafasi na tutaendelea kusafisha kwa hao wachache wanaochafua jeshi la polisi,” anaongeza.

Lugola anasema katika kutekeleza hilo, anaandaa waraka utakaokwenda Jeshi la Polisi ili ziwepo taarifa na hasa kutoka vituo vya pembeni ambavyo wanavifanya vituo vya polisi kama jela wakijua huko waliko hakuna mawasiliano na viongozi, hawawezi kubainika.

Kuhusu kuchelewa upelelezi wa kesi mbalimbali, anasema eneo hilo lina changamoto.

“Linaweza kuwa jambo jingine linahitaji kusafiri nje ya nchi, litahitaji rasilimali fedha na litahitaji vyombo vingine vya uchunguzi kama mkemia mkuu wa serikali lakini kwa sasa na sisi tuna DNA ya kuchunguza.

“Tunakiri kwamba wapo baadhi ya askari ni wazembe wanaweza kuchelewesha makusudi na ndio maana nasema lazima Jeshi la Polisi kupitia waraka huo wa kuwataka wakuu wa vyombo hivyo – Polisi, Magereza, Uhamiaji na Zimamoto kuleta ofisa mmoja wizarani ili awe kiungo na vyombo vyetu, hivyo ili kama kuna malalamiko tunayapata,” anasema