Lwakatare na mkakati wa kurejesha hadhi ya ngumi

Mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2012 uliokuwa wa mwisho kabla ya umaarufu wa mchezo wa ngumi kupotea katika anga za kimataifa.

Kuporomoka kwa kiwango cha ngumi kimataifa, wadau walipaza sauti, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) likaona njia pekee ni kuwaondoa kwa busara viongozi waliokuwa madarakani.

Mambo yalianza hivi

Ilikuwa Februari, mwaka huu safari mpya ya Shirikisho la Ngumi za Ridhaa sasa Ngumi za Wazi (OBFT) ilianza kwa BMT kusitisha Uchaguzi Mkuu wa OBFT na kuuondoa madarakani uongozi uliokuwepo kabla ya kuunda kamati ya kusimamia shirikisho kwa muda.

Aliyekuwa Katibu Mkuu, Makore Mashaga, Makamu wa Rais, Lukelo Wililo, Anthony Mwang’onda na baadhi ya wajumbe waliwekwa kando hadi pale uchaguzi utakapoitishwa tena.

Katibu Mkuu wa BMT wa wakati huo, Mohammed Kiganja alisitisha uchaguzi kwa kuwa baadhi ya viongozi waliokuwa wakitetea nafasi zao hawakuwa na sifa na aliitaka kamati iliyoteuliwa kusimamia mchakato wa maboresho ya katiba ya OBFT kabla ya kurudi kwenye uchaguzi.

Siri Kurejeshwa OBFT

Kabla ya kupiga kura, siyo Lwakatare au washindani wake, Yono Kevela na Samwel Sumwa waliokuwa na uhakika wa kuchaguliwa, upepo ulikuwa mbaya zaidi kwao wakati wa kuhesabu kura ambapo Kevela alichuana vikali na Lwakatatare.

Baada ya mchuano mkali Lwakatare, alishinda kwa tofauti ya kura moja akishinda kwa kura 13 na Kevela kura 12 matokeo ambayo yamewasha taa ya kijani kwa Lwakatare. Katika mahojiano na Spoti Mikiki, Lwakatare alikiri ngumi za ridhaa zimepoteza umaarufu ingawa amechukua jambo hilo kama changamoto.

Sikia mkakati wake

Wadau wa ngumi nchini wanatamani kuona zama za akina Rashid Matumla, Mzonge Hassani, Nasoro Michael, Emmilian Patrick, Joseph Martin na Selemani Kidunda ambao vipaji vya mabondia wa aina ya akina Mzonge vilianza kupotea taratibu baada ya michezo ya Olimpiki ya 2012 nchini Uingereza.

“Tunajipanga upya kama nilivyosema tulikosea mwanzo, lakini naichukulia ile kama changamoto. Tutaanzia pale tulipoishia, lazima ngumi zichezwe nchi nzima, zirudi kwenye hadhi yake iliyokuwepo miaka ya nyuma,” anasema rais huyo.

Lwakatare anasema kuwa wataanza na kalenda ya OBFT ya mwaka 2019 kwa kuhakikisha mashindano ya Taifa yanafanyika Iringa kwa kushirikisha mabondia kutoka mikoa yote nchini na hapo ndipo safari ya timu ya Taifa itaanza.

Mchezo wa ngumi ulivyokuwa

Katika misimu 14 ya michezo ya Madola ambayo Tanzania ilianza kushiriki tangu mwaka 1962 kwenye michezo ya kwanza iliyofanyika Perth, Australia wakati huo ikijulikana kama Tanganyika.

Tangu wakati huo, Tanzania imeweka rekodi ya kushinda medali 21 ambazo ni dhahabu sita, fedha sita na shaba tisa huku mabondia pekee wakichukua medali sita.

Medali ya kwanza ya michezo hiyo ilitoka kwenye ngumi mwaka 1970 wakati bondia Titus Simba (marehemu) alipotwaa medali ya fedha kwa kuingia fainali katika uzito wa kati na kupigwa na John Conth wa England mjini Edinburgh, Scotland.

Willy Isangura aliendeleza rekodi ya medali kwa kutwaa medali ya shaba ya Madola katika uzito wa juu mwaka 1990 kwenye michezo ya Auckland, New Zealand, bondia Haji Ally alitwaa medali ya fedha kwenye uzito wa feather baada ya kupigwa na John Irwin wa England kwenye fainali huku Bakari Mambeya alichukua medali ya shaba kwenye uzito wa light.

Katika michezo ya 1994 Victoria, Canada bondia Hassani Matumla wa Tanzania alitwaa medali ya shaba kwenye uzito wa feather.

Ngumi waliweka rekodi ya kwanza ya kutwaa medali ya dhahabu kwenye michezo ya 1998, Kuala Lumpur, Malyasia.

Bondia Michael Yombayomba alitwaa medali ya dhahabu katika uzito wa bantam, rekodi ambayo mabondia wa Tanzania hawajawahi kuiweka tena kwenye michezo hiyo na tangu hapo hawakuwahi kushinda medali nyingine ya madola.

Kwenye michezo ya Afrika (All African Games) tangu Tanzania iliposhiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1965 nchini Congo Brazzaville ngumi wamevuna medali 11.

Bondia Titus Simba litwaa medali ya shaba kwenye michezo ya 1973 ya Lagos, Nigeria, kwenye michezo ya 1978, nchini Algeria, Lucas Msomba alitwaa shaba.

Katika medali saba ambazo Tanzania ilipata kwenye michezo ya Afrika ya 1987, Kenya, medali nne zilichukuliwa na mabondia.

Bondia Benjamin Mwangata alishinda medali ya fedha, Nassor Michael, Rajabu Hussein na Willy Isangura kila mmoja aliondoka na medali ya shaba katika uzito tofauti.

Bondia Joseph Marwa aliendeleza rekodi katika michezo ya 1991 nchini Misri alipotinga fainali na kutwaa medali ya fedha katika uzito wa kati.

Makoye Isangura aliweka rekodi ya mabondia wa Tanzania katika michezo hiyo kwa kutwaa medali ya dhahabu, Haji Ally Matumla alishinda medali ya fedha na Paul Masele alivuna dhahabu.

Katika michezo ya 1995 iliyofanyika Zimbabwe, Haji Matumla alishinda medali ya shaba kwenye uzito wa kilo 63.5.