MAONI: Ulinzi wa mtoto unaanzia kwa wazazi wake

Hizi ni zama ambazo mambo mengi ya kushangaza yanatokea. Unyanyasaji wa kingono kwa watoto wa shule za msingi umeshamiri katika jamii na wanaotenda ukatili huo ni watu wa karibu kwa watoto hao, aidha walimu, wazazi au ndugu wengine.

Watoto wanakosa watetezi kwa sababu watu wenye jukumu la kuwaangalia ndio hao wanaotenda makosa hayo ya jinai. Jambo hili linahitaji uangalizi wa karibu na wazazi kuvunja ukimya kwa watoto wao. Tukio la hivi karibuni lililoibua taharuki lilikuwa lile la wasichana wa darasa la saba kudaiwa kunyanyaswa kingono na mwalimu wao wa Shule ya Msingi St Florence.

Wanafunzi wanne wa kike wa shule hiyo wanadaiwa kunyanyaswa kingono na mwalimu wao walipokwenda kwenye ziara ya mafunzo huko Kalenga mkoani Iringa. Hakuna mtu ambaye anaweza kuwa na wasiwasi kwamba mwalimu anaweza kufanya ukatili huo kwa wanafunzi wake mwenyewe. Mwalimu ni mlezi kwa sababu ana muda mrefu wa kukaa na mwanafunzi pengine kuliko hata mzazi.

Inapotokea mwalimu aliyepewa jukumu la kumlea mtoto kitaaluma na kinidhamu anakuwa wa kwanza kuhatarisha usalama wa mtoto, basi kuna tatizo kubwa na wazazi wanatakiwa kufuatilia rekodi ya shule husika kabla ya kupeleka watoto wao.

Siyo walimu wote wanafanya uchafu huo, bali wapo wachache ambao kwa tamaa zao wanawarubuni watoto kwa kuwatumia kingono bila ridhaa yao, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Sasa ni wakati wa wazazi kuamka na kutambua kwamba wana dhamana kubwa ya kuangalia ulinzi wa watoto wao kuanzia nyumbani, shuleni na wanapokwenda au kurudi kutoka shuleni.

Maeneo hayo niliyoyataja ni hatarishi kwa ukuaji wa mtoto. Ni lazima mzazi ahakikishe kwamba mtoto wake anakwendaje shuleni, anaangaliwa na nani akiwa shuleni na akirudi nyumbani anakuwa na watu wa aina gani.

Kwa mfano, mwanafunzi anayesoma shule ya kutwa anatakiwa kuelekezwa na mzazi wake njia salama ya kupita baada ya kufanya tathmini na kujiridhisha kwamba haina vihatarishi wakati akipita.

Kwa wale wanaopelekwa na kurudishwa na magari ya shule wako salama zaidi njiani ukilinganisha na wale wanaokwenda kwa kutumia usafiri wa umma au wa miguu.

Wanafunzi hao wanarubuniwa wakiwa njiani. Natambua nafasi ya Serikali kwenye suala hilo hasa katika kumlinda mtoto dhidi ya ukatili kwa kusimamia sheria, lakini jukumu kubwa linabebwa na mzazi.

Yeye ndiye ana dhamana ya kumlinda mwanaye ili akue katika maadili, hekima na kimo.

Wazazi ongeeni na watoto wenu na kuwafungua akili juu ya vihatarishi vinavyoweza kuwakabili. Pia, wafundisheni namna ya kujikinga na vihatarishi hivyo na kuwafundisha kutokuwa waoga kutoa taarifa wanapofikwa na masahibu hayo.

Watoto wengi huwa ni waoga hasa wanapotishiwa kuuawa na wale wanaowanyanyasa kingono. Waondoeni hofu na kuwajengea ujasiri wa kuzungumza nao hata mambo ya siri ambayo wengi wanaona aibu kuzungumza na watoto wao.

Hiyo ni hatua muhimu sana katika ulinzi wa mtoto dhidi ya ukatili wa karne hii ambao umewaacha baadhi ya watoto wakiathirika kisaikolojia, wakiambukizwa maradhi mbalimbali ya zinaa na kuharibiwa mustakabali wa maisha yao ya baadaye.

Mzazi ni mwalimu wa mtoto nyumbani na mwalimu ni mzazi wa mtoto shuleni. Wote wanategemewa kumwandalia mwanafunzi maisha bora ili akiwa mkubwa awe na maadili na kuishi vizuri kwenye jamii yake.

Asasi za kiraia, Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) yashirikiane kuielimisha jamii juu ya haki za watoto na madhara kwa watoto pale inapotokea wamenyanyaswa kingono.