Madhara ya kunywa pombe wakati unatumia dawa

Muktasari:

  • Swali hilo hufikirisha, hususan kwa dawa za muda mfupi na wagonjwa wenye maradhi makubwa.

Mara nyingi wahudumu wa afya tunaulizwa na wagonjwa wakati tunawapa dawa na matibabu mengine kama wanaweza kunywa pombe au la huku wakiendelea na matibabu.

Swali hilo hufikirisha, hususan kwa dawa za muda mfupi na wagonjwa wenye maradhi makubwa.

Mara nyingi tunawashauri wasitumie pombe.Pombe ni kemikali na pia ni dawa.

Hii huweza kusababisha kuingiliana na kemikali zingine zikiwamo dawa.

Muingiliano kati ya pombe na dawa huweza kuleta athari mbalimbali zenye hatari ndogo na kubwa.

Pombe hufanya kazi katika mfumo wa fahamu wa kati (ubongo) na kuingilia ufanyaji wake wa kazi.

Pombe hupunguza ufanyaji kazi wa mfumo wa fahamu na kusababisha kusinzia au kulala, kupunguza uwezo wa kufikiria na kukumbuka, kuathiri mfumo wa upumuaji, kuathiri mfumo wa utoaji taka mwili na kuathiri mfumo wa chakula.

Pia, pombe huathiri ufanyaji kazi wa ini na figo na huchangia kuharibu viungo hivyo.

Kama kemikali, pombe huweza kuingiliana na dawa na kuzalisha kemikali zingine au matokeo mengine ambayo huweza kuwa hatari.

Huweza kusababisha maumivu makali ya tumbo, usingizi mzito, kuharibu zaidi figo na ini, kuzuia dawa isifanye kazi na kukojoa zaidi.

Pombe pia huweza kukusahaulisha muda wa kunywa dawa au kukupita wakati umelala kwa sababu ya pombe, kukufanya upuuzie dawa na hata kukufanya uache kunywa dawa ili unywe pombe kwa amani.

Pia, pombe huweza kuchangia kupunguza ulaji wa mgonjwa na hivyo kuathiri afya na ufanisi wa dawa.

Dawa zinazoingiliana na pombe

Hadi sasa duniani tuna dawa nyingi na bado wanasayansi wanaendelea kutengeneza nyingine kila siku.

Ukweli ni kwamba, siyo dawa zote huweza kuingiliana na pombe.

Dawa nyingine haziingiliani kabisa na pombe na unaweza ukanywa huku unaendelea na dozi zako.

Dawa zinazoingiliana na pombe ni zile zinazoweza kuungana na pombe na kutengeneza kemikali hatari kwa mwili na kuweza kusababisha madhara kwa uhai au viungo vya mwili. Zipo nyingi sana, endelea kusoma.

Dawa zingine zinazoingiliana na pombe ni zile ambazo ufanyaji kazi wake na athari zake huweza kuongezwa au kupunguzwa na pombe.

Zipo nyingi sana, endelea kusoma.

Kwa kuwa siwezi kuandika dawa zote hapa na nikiandika chache zinaweza kukusababisha kukosea naomba nisiandike hata moja, ila mara zote pata ushauri kutoka kwa mfamasia anayekupa dawa au daktari wakati anakuandikia dawa.

Atakuambia na kukupa maelezo zaidi kuhusu muingiliano kati ya hizo dawa zako na pombe.