Maganga ni zao la Marsh linalotesa Singida United

Beki wa kulia wa Singida United, Boniface Maganga

Muktasari:

  • Maganga ambaye alikuwa akiitwa Taifa Stars chini ya kocha aliyepita Salum Mayanga, amejiunga na Singida United, Juni mwaka huu akitokea Mbao FC ya Mwanza.

Beki wa kulia wa Singida United, Boniface Maganga (22) ameonekana kufurahia maisha yake mapya ya soka akiwa na timu hiyo ya Singida kutokana na kuingia kwake moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza.

Maganga ambaye alikuwa akiitwa Taifa Stars chini ya kocha aliyepita Salum Mayanga, amejiunga na Singida United, Juni mwaka huu akitokea Mbao FC ya Mwanza.

Spoti Mikiki imezungumza na mchezaji huyo wa zamani wa Simba ambaye amesema chimbuko lake kisoka lilipoanzia, changamoto alizokutana nazo pamoja na malengo yake.

Chimbuko

“Mpira nilianza kuucheza kwenye kituo cha marehemu, Silverster Marsh, namshukuru sana alichangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa soka langu, kupitia yeye nilijua namna ya kucheza mpira kwa nafasi,” “Mbali na mpira alitufundisha maisha ya utafutaji na hata kuishi na watu vizuri kunavyoweza kumuongezea mtu thamani,” anasema mchezaji huyo ambaye alikulia kwenye kituo hicho, miaka ya 2010.

Changamoto

“Baada ya kukomaa nilijiunga na Simba 2012, changamoto zilianza kujitokeza zile ambazo marehemu kocha wangu Marsh alikuwa akituambia kuwa zipo kwenye soka,” “Miongoni mwa changamoto hizo ilikuwa nafasi ya kucheza, nilipofika Simba niliwakuta Ibrahim Ajib, Shiza Kichuya na Mussa Mgosi hivyo nilitolewa kwa mkopo Mtibwa Sugar ambapo nilicheza na baadaye nikajiunga na kujiunga na Mbao,” anasema Maganga.

Malengo

“Natamani sana kucheza Ligi ya Afrika Kusini kwa sababu Ligi yao ni bora, inaweza kunifanya nikaonekanza zaidi, kupata bahati ya kwenda Ulaya moja kwa moja sio mchezo,”

“Kingine natamani siku moja kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha timu ya Taifa, ni ndoto yangu kulisaidia Taifa langu,” anasema beki huyo.