Majeshi yetu yasibebeshwe ilani za vyama vya siasa

Muktasari:

  • Hii ni wizara ambayo usipokuwa makini utaishia kugombana na watu bila sababu na hata kuwaharibia kazi wengine bila sababu. Lakini pia, hii ni wizara ambayo usipokuwa makini unaweza kuishia kukaa na kutofanya jambo lolote lile, au usifanye maamuzi yoyote ya maana. Au ukamaliza muda wako kila mtu akikushangaa kwa nini ulikuwa waziri, mifano mnayo mingi.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni moja ya wizara nyeti sana. Hapa kwetu wizara hii inasimamia vikosi mbalimbali vya ulinzi ambavyo vinalinda utulivu ndani ya nchi na vinavyosimamia mambo muhimu ikiwemo Jeshi la Polisi, Magereza, Uhamiaji na idara nyinginezo.

Hii ni wizara ambayo usipokuwa makini utaishia kugombana na watu bila sababu na hata kuwaharibia kazi wengine bila sababu. Lakini pia, hii ni wizara ambayo usipokuwa makini unaweza kuishia kukaa na kutofanya jambo lolote lile, au usifanye maamuzi yoyote ya maana. Au ukamaliza muda wako kila mtu akikushangaa kwa nini ulikuwa waziri, mifano mnayo mingi.

Lugola, mkuu wa Magereza

Alipoanza tu kazi, Waziri Lugola alimfukuza mkutanoni, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini Tanzania kwa kosa la kuchelewa kwenye kikao chake na watendaji mbele ya na vyombo vya habari. Kamishna hakusikilizwa, alifukuzwa tu.

Mahali popote duniani, watumishi wa umma hasa wale wanaofanya kazi kwenye vyombo vikubwa hawaamrishwi hadharani, achilia mbali kufukuzwa hadharani. Kamishna Jenerali wa Magereza ni nafasi nambari moja katika usimamizi wa magereza yote ya Tanzania ikiwa ni pamoja na askari magereza wote.

Kumfukuza mtu anayeheshimiwa na askari magereza wote nchi nzima kwa njia ile si tu kunamdhalilisha, bali kunawavunja moyo wenzake wa ngazi zake na kunawavunja moyo askari wa chini yake ambao ama wataona hakutendewa haki au wataanza kudharau watu wanaoshikilia wadhifa huo kwa kuamini kuwa si lolote na wanaweza kufukuzwa kirahisi tu.

Kiitifaki, waziri ni bosi wa Kamishna wa Kamishna Jenarali, lakini waziri ni mwanasiasa ambaye anapita haraka sana kwenye nafasi yake. Waziri hajasomea masuala ya magereza, amepewa tu kuyasimamia, kumfukuza hadharani kamishna ambaye ametumia miaka zaidi ya 40 kutumikia jeshi la Magereza na ambaye ana uzoefu mkubwa kwenye sekta hiyo, ni kasoro kubwa ya kimaamuzi.

Waziri alipaswa kuhoji kwa nini kamishna amechelewa, angemsikiliza na kumtaka aketi waendelee na mkutano ule, au angelikaa kimya na kumpa kamishna nafasi yake ukizingatia kwamba mkutano ule haukuwa umeanza, au angelimtumia ujumbe wa kiitifaki umweleze kuwa kwa sababu amechelewa aondoke.

Kumbuka hapa tunazungumzia utendaji wa ndani wa vyombo vya ulinzi ambavyo vinapaswa kufanya kazi kwa utulivu na kupeana nafasi na heshima hasa pale suala lililoko linawahusu viongozi wakubwa.

Watumishi wote wa umma duniani, hawadhalilishwi hadharani, kama wamekosea hadharani huachwa, wakirudi ofisini huitwa kwa utaratibu na kuhojiwa, kuonywa, kuandikiwa barua na mambo kama hayo. Tusiruhusu, kwa namna yoyote ile viongozi wadhalilishwe hadharani.

Endapo kwa mfano, Rais Magufuli akisimama hadharani na kumfukuza Waziri Kangi Lugola kwenye mkutano na waandishi wa habari, tukosoe tabia hiyo kwa kuwa Lugola atakuwa hajatendewa haki.

Binadamu yeyote yule anahitaji heshima na anahitaji heshima hiyo ilindwe. Hakuna binadamu anayehitaji kudhalilishwa hadharani hata kama amekosea. Ndiyo maana miaka miwili iliyopita, tulisimama hadharani kukosoa vikali tabia ya baadhi ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuwadhalilisha watumishi walioajiriwa katika idara mbalimbali za wilaya na mikoa yao.

Tulisisitiza kuwa utaratibu wa kuwachukulia hatua za nidhamu watumishi na wafanyakazi wa serikalini zipo kisheria, siyo mambo ya kuagizwa au kufanywa na wanasiasa ambao kwa kweli hawana taaluma ya kutosha kuhusu idara na sekta zote wanazozisimamia.

Ilani ya CCM

Septemba 23, 2017, akiwa jijini Arusha katika sherehe mahsusi ya kuwatunuku vyeo maofisa wapya waliohitimu mafunzo ya uofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Rais JPM alitumia sherehe hizo pia kumuita jukwaani Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kisha wakaanza kuwaita baadhi ya watu waliojitambulisha kama viongozi wa Chadema ambao walikuwa wanahamia CCM.

Zoezi la watu hao likafanywa, wakapewa vipaza sauti kwenye sherehe ya kijeshi, wakaanza kuongea kwa nini wameondoka Chadema.

Haya yalitendeka mbele ya vyombo vya habari na kila Mtanzania aliona. Tangu nchi ilianza demokrasia ya vyama vingi, haikuwahi kushuhudiwa wala kuwahi kufikiriwa kuwa iko siku katikati ya sherehe mahsusi ya kijeshi, kutaanza utaratibu wa kupokea wanachama wapya wa CCM.

Wakati kovu hilo halijapona, Waziri Lugola amewaagiza maofisa wa juu wa vyombo na idara na majeshi yote anayoyasimamia, kutembea na ilani ya CCM kama anavyofanya yeye ili anapokutana nao wamweleze ni kwa namna gani wanaizingatia ilani hiyo kwenye utendaji wao.

Kauli hii ya Lugola haikunishangaza, nikakumbuka yale ya Arusha, kwamba masuala ya majeshi yanaweza kuchanganywa na siasa bila tatizo lolote.

Tamko hili la Waziri Lugola halipaswi kupita hivihivi bila kujadiliwa na hasa kukataliwa kwa sababu ni aina ya maagizo yanayovunja katiba na misingi ya kisheria na utamaduni wa nchi yetu ambao kimaandishi unataka masuala ya majeshi yasihusishwe na siasa.

Kwa kawaida, kwa mfano jeshi la Magereza halihitaji ilani ya CCM kutenda kazi zake. Jeshi hilo lina miongozo ya kutosha kutoka serikalini, ambapo miongozo hiyo ndiyo tafsiri sahihi ya ilani ya uchaguzi wa CCM.

Yaani, yale yanayotendwa na magereza kila siku, hayaibuki vichwani mwao, yanatoka kwenye michakato ya kiserikali ambayo huja baada ya wataalamu wa serikali kukaa na kuchambua ilani ya chama kinachoongoza dola na kuchukua mambo muhimu ambayo yanatumiwa na serikali kwenye miaka mitano ya uhai wa serikali.

Inastaajabisha kuona askari wanalazimishwa kubeba ilani ya CCM, ni kama vile Watanzania wanaambiwa huu ni muda na nyakati za kurejesha enzi za siasa za chama kimoja, hiyo siyo sahihi hata kidogo.

Tunaelekea tulikotoka

Ikiwa taifa letu linaamini kuwa siasa za vyama vingi hazitakiwi hapa Tanzania, na kwamba ukuu wa chama kimoja unapaswa kutamalaki, iko haja ya dhati ya kubadilisha katiba yetu na kufuta mfumo wa vyama vingi Tanzania, na kwa hiyo moja kwa moja sheria zote zilizotungwa kusimamia mfumo wa vyama vingi, zitakuwa zimejifia zenyewe.

Tutarudi enzi ambazo tuliwahi kuwako zamani kabla hatujaenda kwenye enzi mpya. Tunaweza kurudi tulikotoka kwa sababu tunao uwezo wa kufanya hivyo, na kwa sababu waamuzi wa mabadiliko ya katiba ni wabunge walio wengi bungeni, na kwa sababu CCM inao wabunge wengi, inaweza kuwa rahisi kukamilisha jambo hili ili Tanzania yetu ijitambue kwa maneno na kwa vitendo kuwa ni taifa lenye mwelekeo wa chama kimoja.

Lakini, hatutajenga taifa imara kama katiba yetu inasema hivi, watendaji na viongozi wa serikali wanafanya ya kwao. Katiba inazuia watu wa kwenye vyombo vya Ulinzi na Usalama kuwa na kadi za vyama vya siasa au wanachama wa vyama vya siasa.

Kitendo cha kiongozi yeyote kuwalazimisha watendaji wa serikali wabebe ilani za uchaguzi za chama kimoja cha siasa kinakiuka msingi huu mkuu, msingi wa sisi ni kina nani na majeshi yetu yanasimamia nini.

Wapo watu ambao wananufaika na amri za namna hii, lakini katika kipindi cha kati na kirefu kijacho, amri hizo zitakuwa na athari kwenye majeshi yetu, ipo siku nchi itajikuta inao majenerali wenye kadi za CCM, CUF, Chadema, ACT n.k. na wataanza kupigania maslahi ya vyama kimyakimya ndani ya mfumo wa ulinzi wa nchi.

Hali hiyo itakuwa ni kwa sababu mchezo huo ulipoanza tulidhani kuwa unapaswa kuendelea kwa sababu unakinufaisha chama kimoja, tunasahau kuwa humo majeshini pia na wao wana roho na wana mapenzi yao nje ya mfumo waliomo.

Na kisha tusisahau dhamira ya watunga katiba, jambo moja ambalo hugeuka kuwa kosa kubwa ni pale ambapo watumia katiba huanza kuacha kutafakari msingi, sababu na hoja za watunga katiba kuweka jambo fulani kwenye katiba.

Watumia katiba hupenda kuitumia kama watakavyo kumbe msingi wa katiba yoyote ni malengo yake.

Kilichofanya watu wa vyombo vya usalama wazuiwe kubeba ilani za vyama na kadi za vyama kinafahamika, na tumekiona nchi nyingi za Afrika ambako unakuta mkuu wa majeshi ni mwanachama wa kimyakimya wa chama kinachoongoza serikali au kinachotafuta kuongoza serikali.

Na tumeona nchi hizo zikiwa kwenye migogoro mikubwa, na chanzo kikuu ni michezo hii ya kulazimisha shughuli na mambo ya kisiasa yafanywe na watu walioko majeshini.

Viongozi wetu wote wanao wajibu wa kutambua uzito wa mambo haya, na kuyabeba kwa uzito huohuo na wasisahau kuwa vyeo ni dhamana.

Julius Mtatiro ni mchambuzi wa mfuatiliaji wa utendaji wa Serikali barani Afrika; ni mtafiti, mwanasheria, mwanaharakati na ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya m. Simu; +255787536759 ([email protected])