Malimi tayari ndani ya Manchester City

Muktasari:

  • Malimi anaenda kuweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kujiunga na akademi ya Manchester City ambayo imekuja na utaratibu mpya wa kusaka vipaji kutoka ndani na nje ya Ulaya kwa ajili ya kunufaika navyo kwa siku za usoni.

Wiki chache zilizopita, kinda la Kitanzania, Malimi Mbassa amefuzu majaribio ya kujiunga na akademi ya Manchester City ambao kikosi chao cha kwanza msimu uliopita kilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu England.

Malimi anaenda kuweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kujiunga na akademi ya Manchester City ambayo imekuja na utaratibu mpya wa kusaka vipaji kutoka ndani na nje ya Ulaya kwa ajili ya kunufaika navyo kwa siku za usoni.

Kinda huyo ambaye alizaliwa mwaka 2005, alikuwa miongoni mwa wachezaji watatu kutoka Tanzania ambao walipata nafasi ya kwenda kufanya majaribio kwa wapinzani hao wa Manchester United ambao wanatawala kwenye mji wa Manchester.

Mwishoni mwa mwaka jana, Malimi na mwenzake, Daud Maurisi ambaye ni kipa kutoka kwenye Kituo cha Soka cha Magnet Youth Sports Organisation cha jijini Dar es Salaam, walikwenda kufanya majaribio hayo kwa siku 14.

Mara baada ya kufanya majaribio hayo ambayo waliambatana na wasimamizi wao huku kwa upande wa Malimi akiwa na baba yake mzazi, Majaliwa, walirejea nchini na kusubiri majibu ambayo awali waliambiwa watapewa Aprili mwaka huu.

Spoti Mikiki ilikuwa karibu na vijana hao kwa kufuatilia nini kitatokea kwenye majibu yao ambayo wamepewa wiki chache nyuma, tena sio kwa njia ya kutumiwa ilibidi Malimi kusafiri na kwenda kupokea majibu ya majaribio yake.

Aliporejea Malimi alizungumza na jarida hili namba moja kwa kuvumbua na kufuatilia maendeleo ya wachezaji wa Kitanzania wanaocheza au kutafuta maisha ya soka nje ya nchi.

Malimi anasema kuwa alipofika England alipokewa vizuri kama ilivyokuwa awamu yake ya kwanza alipotua nchini humo na kufanya majaribio ya wiki mbili.

“Mazingira yalivyokuwa nilijiona kuwa pengine nimefuzu majaribio yale maana walikuwa wakinipongeza kwa kusema hongera sana, nilichuja kwa kujiuliza hawa sio wajinga kuniambia hongera wakati huo niwe sijafuzu majaribo.

“Mawazo yangu yalikuwa sahihi, waliambia kuwa nimefuzu majaribio kwa hiyo, nitajiunga nao rasmi kwenye akademi yao ya vijana waliochini ya miaka 13.

“Nilifurahi sana kusikia vile, sikuwa na muda mrefu wa kuendelea kukaa Manchester, safari hiyo sikupata nafasi ya kuonana na mastaa mbalimbali wa timu hiyo maana wengi walikuwa tayari wameondoka na wachache niliwaona kwa mbali,” anasema Malimi.

Kinda huyo ambaye anapenda kucheza kama mshambuliaji, anasema alirejea nchini kwa furaha kubwa ambayo imetokana na sehemu ya ndoto zake kutimia.

Ndoto za Malimi ni kucheza soka la kulipwa barani Ulaya na anaamini kupata kwake nafasi ya kujiunga na akademin ya Manchester City kutamfanya kukua kwenye misingi bora ya mpira kabla ya kuanza kucheza soka la ushindani.

“Nataka kuwa msaada kwa taifa langu la Tanzania, nikiwa mchezaji mkubwa inamaana mchango wangu nitautoa pia kwenye timu ya taifa,” anasema kinda huyo.

Awali baba wa Malimi, Majaliwa Mbassa alizungumza nasi na alisema wazi kipindi ambacho mwanawe alifanya majaribio kuwa anamtafutia nafasi ya kujiunga na akademi yoyote nchini England ili kutimiza ndoto zake.

Majaliwa alitambua kuwa kwenye majaribio kuna kufanikiwa na kushindwa kwa hiyo mbinu yake mbadala kama ameshindwa ilikuwa ni kumpigania ili ajiunge na akademi za hata timu za madaraja ya kwanza.

Lakini habari njema kwa familia ya Majaliwa na Watanzania kwa ujumla ni kufuzu kwa kijana huyo ambaye amezaliwa kwenye familia ya wapenda soka kuanzia baba hadi mama.

Katika mazungumzo yetu, Malimi amesema amekuwa akivutiwa kwa ukaribu na uchezaji wa Sergio Khune Aguero na Gabriel Jesus ambao wamekuwa wakicheza kwenye safu ya ushambuliaji ya Manchester City.

Pamoja na kufuzu kwake majaribio kwenye akademi ya Manchester City, Malimi ni ambaye kwa Tanzania anaipenda Simba ni shabiki wa kutupwa wa Manchester United.

“Hata kama nikiwa mkubwa na kuanza kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha Man City siwezi kuwa na kitete kuifunga Man United eti kwa sababu naipenda, nitawafunga ilia sintoshangilia,” anasema Kinda huyo.

Mwisho kabisa, Malimi anasema kujiunga kwake na akademi hiyo utakuwa mwanzo wa vijana wenzake kupata nafasi kwa wingi kwenda kufanya majaribio kwenye klabu hiyo.

Malimi amepanga kuonyesha kipaji chake ili kuwa kivutio kwa makocha wake na waone kuwa Tanzania ni miongonin mwa mataifa Afrika yenye vipaji vya soka.