Mambo mazito yamhusisha gavana na mauaji ya mwanafunzi

Muktasari:

  • Kauli ya siasa ni mchezo ni mchafu, inaweza kuwa na maana nyingi na pengine tukio la Gavana wa Jimbo la Migori, Okoth Obado lililopo magharibi mwa Kenya yuko kwenye wakati mgumu baada ya kuhusishwa na mauaji ya mwanafunzi Sharon Otieno anayeelezwa kuwa ‘mchepuko’ wake.
  • Gavana Obado ambaye amekamatwa na polisi anadaiwa kuhusika na mauaji hao kwa lengo la kukwepa aibu na kutunza heshima yake ya kisiasa kwenye jamii, baada ya Sharon kukataa kutoa ujauzito unaodaiwa ni wa gavana huyo.

Kitumbua kimeingia mchanga. Kila mmoja anauliza, kulikoni? Kama ilivyo kawaida ya Wakenya, siasa zimeingizwa katika kizungumkuti cha mauaji ya kinyama cha binti mmoja aitwaye Sharon Otieno.

Hadi wiki jana, binti wa watu aliyekuwa ameumbwa akaumbika, mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Rongo aliuawa. Mrembo huyo pia alikuwa na mimba wa miezi saba.

Sharon aliyekuwa na umri wa miaka 26, alitekwa nyara pamoja na mwanahabari Barrack Oduor Jumatatu wiki jana. Siku mbili baadaye, mchungaji wa ng’ombe aliuona mwili wake ndani ya msitu ukiwa umekatwakatwa kwa silaha yenye ncha kali.

Mafuriko ya simanzi yaliloa kila pembe ya nchi huku Wakenya wakitaka watu waliohusika na kifo chake wanaswe na kufikishwa mbele ya mahakama ili mwanafunzi huyo apate haki.

Habari kuhusu mauaji hayo zimeendelea kugonga vichwa vya habari tangu kisa hicho cha kusikitisha kilipofanyika.

Hii ni kwa sababu mtuhumiwa mkuu wa mauaji hayo anatajwa bwanyenye mmoja mwanasiasa ambaye mrembo huyo alikuwa ana uhusiano wa kimapenzi.

Duru za kuaminika zanasema kwamba bwanyenye huyo ambaye pia ni Gavana wa Jimbo la Migori, Okoth Obado ambaye tayari amekamatwa na polisi, alikuwa amemsihi Sharon atoe mimba hiyo kwa sababu yeye hataki aibu ndogondogo kwa sababu ya wadhifa na nafasi yake katika jamii.

Si ajabu kwamba waliomuua Sharon walimpasua tumbo na kumuua mtoto.

Wanavyosema wanasiasa

Wanasiasa na wananchi wamegawanyika kuhusiana ni nani anayefaa kulaumiwa kwa mauaji hayo. Baadhi ya wanasiasa wanasema lawama zinazoelekezwa kwa Gavana Obado zinachochewa na siasa kwa sababu mwanasiasa huyo ni adui wa kinara wa ODM, Raila Odinga.

Ili kufahamu siasa za eneo la Nyanza haswa katika majimbo yanayomilikiwa na Wajaluo, chama kinachoenziwa sana ni ODM. Obado ni kama muasi. Huku wanasiasa wengine kutoka maeneo haya wakigombea viti kwa tiketi ya ODM, Obado hugombea kiti hicho kama mgombea binafsi.

Jimbo la Migori linapanga kuchagua seneta mpya kwenye uchaguzi mdogo. Makachero wako mbioni kujua mbivu na mbichi kuhusu aliyemuua mwanafunzi huyo na waliopanga mauaji hayo.

Vidole vingi vya lawama vinaelekezwa kwa Obado kwa sababu inadaiwa alimwamuru msaidizi wake mkuu, Michael Oyamo “atatue shida kati yake na Sharon”.

Tangu aanze uhusiano wa kimapenzi na Gavana Obado, maisha ya Sharon yalibadilika kabisa. Alikuwa anasafiri kwa ndege takriban kila wiki akielekea ughaibuni au katika majiji ya Kenya huku wengine wakihangaishwa ndani ya daladala. Mwanafunzi huyu aliyependa maisha ya anasa, alikuwa anapokea marupurupu si haba kutoka kwa mpenziwe anayesimamia fedha za jimbo zima.

Sharon alikuwa amemwambia mwanahabari Oduor kwamba, Gavana Obado ameanza kubadilika na kumsihi kila mara atoe mimba, jambo ambalo msichana huyo alikataa. Mama yake Sharon, Melinda Auma alisema Obado alikuwa ameahidi kumnunulia nyumba bintiye. Pia, alikiri kwamba alijua kuwa wawili hao walikuwa wapenzi wa chanda na pete.

Sharon alipokataa kutoa mimba, mambo yakaenda mrama na hatimaye kuuwa kwake. Gavana Obado alikuwa anahofia mimba hiyo ingemsababishia shida nyingi katika familia na pia kisiasa. Lakini, sasa kila mtu anabeba mzigo wake, kama vile inavyosema Bibilia.

Gavana wa Nairobi aibuka

Gavana wa Nairobi, Mike Sonko amemshauri Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP), Noordin Haji ahakikishe mshukiwa mkuu wa mauaji hayo amenaswa.

Sonko anamtaja Obado kama mshukiwa mkuu na kushangaa kwa nini aamue kumuua binti wa watu kwa sababu ya mimba. “Mbona Obado hakutumia kinga kuhakikisha anazuia kumpa mimba Sharon?’ Sonko anahoji.

Seneta wa Makueni, Mutula Kilonzo Jr pia analaani kitendo hicho.

Jumatatu iliyopita, Sharon alimpigia simu Oduor akimwarifu kwamba, Oyamo angetaka kuzungumza naye kuhusu suala hilo la uhusiano kati yake na Obado. Sharon na Oduor walifika kwenye hoteli inayoitwa Graca katika jimbo hilo la Migori kama walivyoambiwa na Oyamo. Lakini, Oyamo alipofika akawaambia wawili hao kuwa mkutano umehamishiwa hadi mahali pengine. Wote waliingia katika gari jeusi lililomleta Oyamo na gari likaanza safari.

Mita 50 hivi, Oyamo akashuka na watu wawili wa miraba minne waliingia ndani ya gari hilo na gari likaendelea. Watu hao waliokuwa na silaha walianza kuwatesa Sharon na Oduor huku gari likiendeshwa.

Akitoa taarifa yake kuhusu yaliyojiri wakati wa utekaji nyara, Oduor alisema aliruka na kutafuta msaada katika nyumba moja karibu na barabara. Mwanahabari huyo alijeruhiwa magotini na kwenye viganja vyake.

Uchunguzi wa makachero unaonyesha kuwa Sharon alikuwa amehofia maisha yake na kumtumia Gavana Obado ujumbe kwa simu akimuuliza kwa nini ameachwa mikononi mwa watu asiowajua. Ujumbe huo ndio ulikuwa mawasiliano ya mwisho kutoka kwa msichana huyo ambaye alipatikana akiwa uchi huku akiwa amenajisiwa na kumwagiwa tindikali kwenye sehemu zake za siri.

Kwa nini mtu auliwe kinyama hivi? Inamaanisha waliokuwa wanamuua walikuwa wanamchukia na walitaka pia kiumbe alichokuwa amekibeba tumboni kife.

Mwili wa kiumbe kitoto umefanyiwa uchunguzi wa DNA ili ijulikane babake ni nani.

Duru za kuaminika zinasema Sharon alikuwa ameolewa na alikuwa na watoto wanne. Alimwacha mumewe Januari mwaka huu.

Obado alihojiwa na makachero Jumanne Septemba 11 kuhusiana na uhalifu huo wa kutatanisha.

Pia, Oduor amehojiwa kwa sababu alitoa habari nyeti aliyoambiwa na Sharon kuhusu uhusiano wa Obado na mwanafunzi huyo. Matamshi ya Oduor yamemweka Gavana Obado katikati ya kizungumkuti hiki cha mauaji.

Uchunguzi wafanyika

Wachunguzi wa visa vya mauaji waliotumwa katika majimbo ya Migori na Homa Bay kuchunguza uhalifu huo tayari wamerekodi taarifa kutoka kwa watu saba miongoni mwao ni wazazi wa Sharon na marafiki. Watu hao wote wanamlaumu Obado kwa mauaji ya Sharon.

Wakili Cliff Ombeta ambaye anamwakilisha Gavana Obado alifukuzwa wiki jana alipohudhuria upasuaji wa kutafuta jinsi Sharon alivyouliwa. Uchunguzi ulionyesha kuwa Sharon alifariki kwa sababu ya kuvuja damu.

Mwili wake ulipatikana katika msitu wa Kodera katika Jimbo la Homa Bay.

Tangu awe Gavana wa Migori miaka sita iliyopita, Obado amekuwa akikumbana na masahibu makubwa ya kisiasa.

Muda mfupi kabla ya uchaguzi mkuu wa 2013, Obado alikaidi amri ya Raila ya umoja wa kisiasa katika majimbo yanayomilikiwa na Wajaluo. Licha ya hayo, alishinda uchaguzi wa ugavana baada ya kumshinda mgombea wa ODM, Profesa Akong’o Oyugi.

Katika uchaguzi wa mwaka jana. Obado alipinga ODM tena wakati wakora waliohusishwa na yeye waliingia uwanja wa michezo wa Migori na kuvunja mkutano wa kisiasa uliokuwa unahutubiwa na Gavana wa Mombasa, Hassan Joho ambaye alikuwa anampigia debe Achilo Ayacko, aliyekuwa anagombea ugavana wa jimbo hilo.

Msemaji wa Obado ameonya dhidi ya kuhusisha mwanasiasa huyo na kifo cha Sharon.

Gavana wa Jimbo la Garissa, Ali Korane pia anapambana na madai kwamba alihusika na jaribio la kumuua aliyekuwa msimamizi wa fedha katika jimbo hilo, Idris Mukhtar ambaye alimiminiwa risasi wiki tatu zilizopita jijini Nairobi.

Washukiwa sita walinaswa na kuwekwa rumande huku uchunguzi zaidi ukifanywa. Lakini mshukiwa mkuu David Mwai ambaye alimpiga risasi Mukhtar alipatikana amefariki.

Taarifa zilizotolewa na washukiwa zasema Gavana Korane alitoa hundi ya Sh1.8 milioni kama ada ya kuwalipa wauaji wa Mukhtar.

Wakenya wanatarajia haki itatendeka katika mauaji ya Sharon na pia katika jaribio la mauaji ya Mukhtar.