Mambo muhimu ya kukusaidia kuyalinda mahusiano yako

Muktasari:

  • Makubaliano na maelewano haya ya kuaminiana na kupendana ndiyo yanayoyafanya mahusiano baina ya wawili hawa kuwa yenye afya, ingawa pia wawili hawa hawawezi kuepuka ukweli kwamba ni lazima wote kujitoa kwa dhati katika kuilinda heshima na hadhi ya hisia za kila mmoja bila kujali hali tofauti watakazozipitia katika maisha.

Mahusiano yoyote baina ya watu wawili waliomaanisha kuwa pamoja kama mke na mume au wachumba ni kitu chema na kinachotakiwa kuheshimiwa na wote. Wakati wawili hawa wanaanza mahusiano yao wanakuwa na uelewa na makubaliano kwamba wataikita mioyo yao katika kuaminiana.

Makubaliano na maelewano haya ya kuaminiana na kupendana ndiyo yanayoyafanya mahusiano baina ya wawili hawa kuwa yenye afya, ingawa pia wawili hawa hawawezi kuepuka ukweli kwamba ni lazima wote kujitoa kwa dhati katika kuilinda heshima na hadhi ya hisia za kila mmoja bila kujali hali tofauti watakazozipitia katika maisha.

Hata hivyo, tusisahau kwamba wako watu, tena wengine ni marafiki kabisa na wapenzi hawa ambao kiu yao nikuona mambo yanawaharibikia na uelekeo wa mahusiano yao unabadilika kabisa. Watu hawa maranyingine tunawaita “wadudu hatarishi wa mapenzi”.

Sio kwamba watu hawa ni wabaya wakati wote ila maranyingi wanaweza kabisa kumshawishi na kumwekea mazingira mtu aliyeko kwenye mahusiano yake ili tu ajikute amejiingiza kwenye mahusiano ya pembeni yaliyo batili na mwisho kujikuta anahatarisha mahusiano yake ya kwanza. Kama unajihisi kuhusika au kutamani kuwajua zaidi hawa “wadudu hatarishi wa mapenzi” basi mambo yafuatayo yatakusaidia katika kuyalinda mahusiano yako.

Fahamu kwamba sio mara zote wadudu hawa hatarishi wa mapenzi wanajua wanachokifanya

Kama ilivyo kwa wanyama wengine wanaoshiba kwa kuwala wanyama wengine msituni, wasivyojua wala kufahamu maumivu na mateso wanayopitia hawa wanaoliwa, wadudu hawa hatarishi wa mapenzi nao hufanya vile vile.

Mtu wa jinsi hii unakuta anaamua kumchagua yeyote aliyeko kwenye mazingira yake kama vile ofisini, au kwenye kundi la marafiki bila yule anayechaguliwa kujua, na taratibu humvuta mtu huyu na kuanzisha urafiki wa karibu sana na wenye hisia. Mara nyingi watu hawa huchagua mtu ambaye tayari yuko kwenye mahusiano ya ndoa, mchumba au mahusiano mengine yenye kumaanisha.

Watu hawa “wadudu hatarishi wa mapenzi” wanaweza kuwa wakiume au wakike, wanaweza kuwa wenye kuvutia au hata wasiovutia, wanaweza kuwa wa rangi, kabila au umri wowote, ila kiukweli wanaweza wasifahamu nini hasa nia na madhumuni yao, wao wanafahamu tu kwamba wanafurahisha hisia zao kwa kujiingiza kwenye aina hii ya urafiki na hawafikirii kabisa madhara ambayo tabia zao hizi zinaweza kusababisha kwa mtu huyu mwingine aliye na ndoa yake au mahusiano yake ya kudumu au hata kwa watoto wake.

Wadudu hawa hatarishi wa mapenzi wana kiu ya kuwatawala wenzao ili waonekane wao ni wenye thamani zaidi.

Hisia wanazo hisi wadudu hawa zinatokana na kule kufahamu kwamba wana nguvu na wanaweza kumtawala mtu mwingine, mtu wa jinsi hii hujitahidi kuweka mazingira ili huyu mtu mwingine aanze kuvutiwa na kuwa na hisia kwake, na kwa kufanya hivi mdudu huyu hujisikia raha sana. Hali hii humfanya ajisikie mwenye thamani na mwenye nguvu, na taratibu huongeza kiwango cha hisia kwa mwingine akijua fika kwamba sio sawa.

Mara nyingi mtu huyu “mdudu hatarishi wa mapenzi” huamua kwa dhati kabisa kutofanya mahusiano au urafiki huu uingie kwenye mapenzi, kwasababu yamkini nia na kiu yake sio kufanya mapenzi au anaweza kujua kabisa kwamba akiruhusu urafiki huu ukaingia kwenye kufanya mapenzi basi urafiki wao unaweza kufikia mwisho na kwahiyo ile raha anayoipata kwa kuwa karibu na huyu mwenzake ikaisha.

Wadudu hawa hatarishi hawana nia ya kuvunja mahusiano uliyonayo na mpenzi wako.

Nia na madhumuni ya wadudu hawa sio kukutenganisha na mpenzi wako, la hasha bali wao wanakuwa kama kupe aliyenasa juu ya ng’ombe akimyonya damu ng’ombe pasipo nia ya kumuua ng’ombe yule ila tu yeye kuitosheleza njaa yake ya kunyonya damu. Watu hawa hushibisha hisia zao kwa kule kuwa karibu na wewe kihisia wakiunyonya utamu wa hisia za mapenzi toka kwako ambazo kiukweli ungetakiwa kuziingiza kwenye mahusiano uliyonayo na mpenzi wako. Hali hii sio salama wala sio ya afya kwa yeyote anayejihusisha, sio anaye nyonya wala anayenyonywa.