Mambo usiyoyajua kuhusu Kofi Annan

Muktasari:

Mbali ya kushinda Tuzo ya Amani ya Nobel, Annan anatajwa kuwa mwanadiplomasia aliyefanya mageuzi yenye manufaa UN

Kofi Atta Annan mwanadiplomasia wa kimataifa mzaliwa wa Ghana, amefariki dunia. Dunia nzima inaomboleza kifo chake. Amefariki akiwa na umri wa miaka 80. Ametoka mbali.

Ndoto ya Annan kuwa mwanadiplomasia ilianzia katika shule ya bweni nchini Ghana ambako alijifunza moja ya masomo muhimu zaidi.

Somo hilo ni lile alilokuja kusema baadaye kwamba “mateso ya watu popote duniani yanahusu wote kila mahali”. Kofi alisafiri na ndoto hiyo hadi kuwa mwanadiplomasia wa juu duniani.

Wazo au fikra hiyo ilionekana kumshawishi Annan katika maisha yote ambayo ilimpaisha na kuchukua jukumu muhimu la kutatua migogoro ambayo imeikumba dunia, kuanzia janga la maambukizi ya Virusi vya Ukimwi - VVU / UKIMWI, hadi Vita vya Iraq na, na baadaye mabadiliko ya tabianchi.

Tabia yake ya kujali ubinadamu ndiyo ilimwezesha kushinda Tuzo ya Amani ya Nobel, lakini pia kuwashinda wakosoaji wake.

Annan, mwanadiplomasia wa kwanza mweusi kutoka Afrika kuongoza Umoja wa Mataifa (UN), ndiye bila shaka alikuja kuwa mmoja wa wanadiplomasia madhubuti na kutambuliwa katika historia ya kisasa.

Mapambazuko

Aprili 1938 Kofi Atta Annan alizaliwa na dada yake Efua Atta wakiwa mapacha katika mji wa Kumasi. Majina ya kwanza ya mapacha hao yalimaanisha “walizaliwa siku ya Ijumaa” katika kabila la Akan, wakati jina lao la kati lilimaanisha “mapacha”.

Alikulia katika familia tajiri - babu zake walikuwa viongozi wa jadi, wakati baba yake alikuwa gavana wa mkoa - katika nchi ambayo bado ilikuwa chini ya utawala wa Uingereza.

Kisha, siku mbili kabla ya kusherehekea siku ya kuzaliwa akifikisha umri wa miaka 19, hatimaye nchi ilipata uhuru wake, ikawa Ghana.Mchango muhimu wa maisha ya baadaye ya Annan hauwezi kubezwa.

“Nilitembea kikakamavu kama kijana aliyeridhika kwamba mabadiliko yanawezekana, hata mabadiliko makubwa ya kimapinduzi,” Annan alikiambia kikundi cha Wacanada mwaka 2012.

Baada ya kuhitimu chuo kikuu, kwanza katika Ghana iliyotoka kupata uhuru, kisha katika Chuo cha Macalester nchini Marekani, alipata kazi yake ya kwanza UN.

Nafasi yake kama ofisa bajeti katika Shirika la Afya Duniani (WHO) hakuonyesha dalili za kazi aliyokuja kuifanya miongo minne baadaye kufikia mwaka wa 1997 alipochaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa UN.

Lakini kabla ya kufikia ngazi hiyo, alikumbwa na kashfa kubwa katika kazi yake.

Mauaji ya kimbari

Mwaka 1993, alikuwa amepanda ngazi hadi kuwa msaidizi wa katibu mkuu na mkuu wa idara ya kulinda amani.

Mwaka uliofuata, yalizuka mapigano yenye mrengo wa kikabila kati ya Watutsi na Wahutu nchini Rwanda ambapo watu waliouawa walifikia 800,000 katika siku 100. Kisha, mwaka 1995, Waislamu wapatao 8,000 waliuawa na majeshi ya Serbia katika eneo lililotengwa na UN kuwa salama huko Bosnia.

Katika matukio hayo yote, Annan na idara yake waliwekwa kikaangoni - hasa baada ya kuonekana kuwa idara yake ilipuuza kwa kiasi kikubwa taarifa walizokuwa wamepewa, zikionya kwamba mauaji ya kimbari yalikuwa yanapangwa Rwanda.

Katika maadhimisho ya kumi ya mauaji ya kimbari, Annan alikiri mapungufu yake.

“Mimi binafsi, kama mkuu wa idara ya kulinda amani ya UN kwa wakati ule, niliomba askari kutoka makumi ya nchi,” alisema mwaka 2004. “Niliamini kwa wakati ule kwamba nilikuwa nikitekeleza wajibu wangu kwa ubora zaidi.

“Lakini nilitambua baada ya mauaji ya kimbari kuwa kuna mambo zaidi ambayo ningeweza kufanya, na nilipaswa, kupaza sauti na kuomba msaada. Kumbukumbu hii yenye uchungu, pamoja na ile ya Bosnia na Herzegovina, imeshawishi sana mawazo yangu, na matendo mengi, kama katibu mkuu. “

Pamoja na hayo, mwaka 1997, akiwa na umri wa miaka 59, Annan alifanikiwa kurithi nafasi ya Boutros Boutros-Ghali kama Katibu Mkuu wa UN.

Migogoro

Annan alirithi shirika ambalo, baada ya miaka 52, lilikuwa kwenye ukingo wa kufilisika.

Kutokana na juhudi zake aliweka mikakati ya kufanyia marekebisho taasisi, kupunguza ajira 1,000 kutoka nafasi 6,000 katika makao makuu ya New York, huku akijaribu kuyashawishi mataifa yaliyokuwa yakisitasita kuchukua jukumu la ufumbuzi wa majanga mengi duniani. Pia, alipata wakati mgumu kuishawishi Marekani kulipa madeni ambayo ilikuwa ikidaiwa na UN.

Halafu alielekeza nguvu zake kuimarisha ustawi wa baadaye, kwa kuanzisha Malengo ya Milenia - kuweka vipaumbele vya kutekeleza kufikia mwaka 2015 kama kupunguza viwango vya umaskini na kuzuia kuenea kwa VVU / UKIMWI.

“Nilikuwa nasema kwamba herufi SG zinazomaanisha ‘secretary-general’, ni kifupi cha scapegoat (kisingizio),” aliliambia shirika la BBC.

Mnamo 2001, Annan na UN walipewa Tuzo ya Amani ya Nobel. Alisifiwa na Kamati ya Nobel ya Norway wakati akikabidhiwa tuzo hiyo kuwa ni “mtu aliyeleta maisha mapya kwenye shirika”.

Mwaka huo huo, alichaguliwa kwa kishindo kuongoza kwa muhula wa pili. Lakini mabalaa bado yalikuwa kwenye kona.

Kashfa

Mwaka wa 2003, Marekani - miongoni mwa nchi zilizokuwa zikimuunga mkono - ilitangaza nia yake kwenda vitani Iraq. Hatimaye, Marekani ilikiuka taratibu za UN na kuivamia Iraq kwa kushirikiana na washirika wake.

Hii ilisababisha ufa kati yake na taifa hilo lenye nguvu za kijeshi duniani. Akizungumzia uvamizi, baadaye aliiambia BBC: “Kutokana na mtazamo wetu na kutokana na mkataba wa UN, haikuwa halali.”

Mpasuko huu mpya kati yake na Marekani ulimsababishia matatizo baada ya kuibuka “kashfa ya mafuta kwa chakula” mwaka 2004, ikimhusisha kitaaluma na binafsi.

Mpango huo ulioanzishwa mwaka 1996 ili kuuza kiasi kidogo cha mafuta kutoka Iraq iliyokuwa imewekewa vikwazo, kwa mahitaji ya kibinadamu, ulibadilishwa na baadhi ya wale waliohusika, ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara, maofisa wa UN, wanasiasa wa kimataifa na wanadiplomasia.

Shida zaidi ilikuwa ukweli kwamba mtoto wa Annan mwenyewe, Kojo, alikuwa amepokea malipo kutoka kampuni iliyopewa mkataba ili kufuatilia mpango huo.

Uchunguzi uliofanywa mwaka uliofuata ulimsafisha kuwa hakutumia ushawishi usiofaa kwa niaba ya mwanawe, lakini alipatikana kuwa na mapungufu namna alivyosimamia mpango huo.

Ndipo wanasiasa wa Marekani walianzisha kampeni wakimtaka ajiuzulu. Jibu lake? “Hapana.”

Anastaafu

Miezi 18 baadaye yaani Desemba 2006, aling’atuka. Katika umri wa miaka 70, watu wengine wangefurahi na kupumzika.

Yeye na mke wake wa pili, mwanasheria wa Sweden Nane Marie Lagergren, ambaye alimuoa mwaka 1984, waliamua kwenda Italia kwa mapumziko ya wiki sita.

Kwa mujibu wa The Guardian, baada ya wiki moja alijikuta amechoka na akaamua kuvinjari na kununua gazeti, mara alijikuta amezungukwa na vijana waliotaka atie saini kwenye wasifu wao wakimfananisha na mwigizaji wa Marekani Morgan Freeman. Ili asiwaangushe, alisaini kwa jina la Freeman kisha akatoweka.

Pengine kasi ambayo alipata ilimchochea kuchoka ilikuwa ishara ya kilichokuja kutokea: alianzisha Mfuko wa Kofi Annan, ambao unalenga maendeleo endelevu duniani, usalama na amani, mwaka 2007.

Mwaka uliofuata, aliongoza jukumu la kidiplomasia lenye mafanikio zaidi nchini Kenya.

Jukumu hilo lilikuwa la kuwezesha mkataba wa kugawana madaraka kati ya kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga na Rais wa zamani Mwai Kibaki kukomesha machafuko yaliyoibuka baada ya uchaguzi mkuu na kusababisha vifo vya watu 1,000, na wengine 300,000 kulazimishwa kukimbia nyumba zao.

Mwaka 2012, alichaguliwa na UN na Umoja wa Nchi za Kiarabu kuwa Mwakilishi Maalum wa Syria katika mpango wa kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwaka uliofuata alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Wazee, asasi iliyoanzishwa na Nelson Mandela Kusini mwa Afrika, ili kuwaleta pamoja viongozi wa zamani wa kimataifa kufanya kazi kwa ajili ya amani na haki za binadamu.

Miaka minne baadaye aliombwa na kiongozi wa Myanmar Aung San Suu Kyi kuongoza tume huru ya kuchunguza mgogoro wa Rohingya nchini mwake.

Aliendelea kuwa mjumbe mwenye sauti katika masuala kama mabadiliko ya tabianchi.

“Nimegundua kwamba kustaafu ni kazi ngumu,” Annan alitania alipozungumza na BBC siku alipoadhimisha ‘bethdei’ yake ya 80.

Pia, Annan alikuwa mwenyekiti mwanzilishi wa Umoja wa Mageuzi ya Kilimo Afrika (AGRA), ambayo hujihusisha na usalama wa chakula na matarajio bora kwa kuinua kilimo endelevu na haraka kwa kuwajali wakulima wadogo.