TUONGEE KIUME: Mapenzi na ‘siasa chafu’ ni kurwa na doto

Sunday September 9 2018

 

By Kelvin Kagambo

Kama hazifanani hivi lakini zinafanana karibu kila kitu. Ukiwa huna msongo wa mawazo wa madeni mengi uliyonayo, ukatulia na kuliwaza hili unaweza ukagundua ni kweli ndoa na siasa chafu zinafanana mno.

Hapa sisi tuna sababu tatu za msingi.

Hongo

Karibu ndoa zote zinaanza na hongo. Mmoja ambaye ataanza kuonyesha kumuhitaji mwenzie lazima kuna chambo atumie kumnasa (hasa muhitaji akiwa ni mwanaume). Lazima ataanza kwa kuhonga pesa mbili tatu, kumtoa mrembo out, kumnunulia vizawadi vya hapa na pale ilimradi tu binti aone kuna mtu anamjali. Binti akishanasa kinachofuatia ni kuisoma namba.

Au kama mchakato hautaanzia kwa binti mwenyewe, labda utaanzia kwa wazee wa familia. Lazima wazee wanunuliwe sana pombe ili kuhakikishiwa kwamba anayetaka kumchukua binti yao sio mtu wa kawaida.

Viongozi wote wanaofanya siasa chafu kwenye mataifa ya Afrika wameingia madarakani kwa mtindo huu. Wa kugawa vikanga na makofia kama mabanda ya juisi ya miwa kwa wapiga kura. Na wazee wa kijiji wakamwagiwa kilo za unga na mchele kama hawana akili nzuri.

Uongo

Kama hivi tunavyozungumza wewe ni mwanandoa, na uliingia kwenye ndoa bila kutumia hata chembe ya uongo, kuwa wa kwanza kuokota mawe kuwapiga waongo.

Ndoa ni uongo; mwanzo utamdanganya binti wa watu, “Mimi niko hivi, mimi niko vile, nitakufanyia hivi, nitakufanyia vile” halafu mwisho wa siku hatoona ‘vile’ wala ‘hivi’ yoyote. Kadanganywa. Na uongo haushii mwanzo tu, unaendelea hadi ndani ya ndoa.

Huku kwenye siasa tushadanganywa sana, tushaambiwa sana ‘mkinichagua mimi hii Shule ya Msingi Mtakoma itakuwa na madawati hadi vyooni’; lakini leo tuna miaka sijui 50 sijui 40 ya uhuru na bado kuna watoto wetu wanalijua dawati kama msamiati tu, hajawahi kuliona.

Ndimi Mbili

Mwanamke mnaoana leo, mnakaa miaka 10 kwenye ndoa, mnabarikiwa watoto watatu wenye afya. Miaka yote hiyo 10 mnaambiana nakupenda, namshukuru Mungu kupata mwenza kama wewe, wewe ni mwenza wa tofauti sana, bila wewe mimi siwezi kuishi na mapochopocho yote ya mapenzi humo ndani.

Lakini kwa bahati mbaya likatokea jambo likapelekea mkatengana hapo ndipo utaelewa maana ya neno ‘ndimi mbili’. Utaambiwa mwanaume gani wewe, nimekuvumilia tu miaka 10 yote hiyo, huna lolote, unadhani bila wewe siwezi kuishi na makorokoro yote ambayo ni kinyume cha yale mliyokuwa mnaambiana kipindi cha ile miaka 10 yenu.

Sasa hii huijui kwenye siasa? Leo fulani ataitwa fisadi na chama pinzani, akihamia chama pinzani watamsafisha na kusema hakuna malaika kama huyo. Mwanasiasa mwingine naye atakaa miaka 10 chama fulani akikipigania kichukue madaraka, lakini akihama atakwambia kile chama ni cha mafisadi, wabinafsi na wabaguzi — na aliiishi humo kwa miaka 10 akituomba wananchi tukiingize madarakani. Ni kazi nzito.

Advertisement