Marais Afrika waungane na Uhuru kudai fedha ‘zilizofichwa’ Ulaya

Muktasari:

  • Alianza Julai alipokutana na Rais wa Uswisi, Alein Berset alipoingia katika makubaliano ya nia ya kuona fedha zilizohifadhiwa katika mabenki ya nchi hiyo na Wakenya zinarejeshwa nchini humo na Agosti akakutana na Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May ambapo wamekubaliana kuwa mali na fedha taslimu za Wakenya zilizoko nchini humo na katika kisiwa cha Jersey zinaanza kurudishwa nchini humo.

Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita Rais wa Kenya ameanzisha juhudi mpya za kutaka kurejeshwa nyumbani kwa mamilioni ya shilingi zilizoibwa nchini humo na kuhifadhiwa katika mabenki ya Ulaya na katika visiwa vijulikanavyo kama “pepo za wakwepa kodi ulimwenguni”.

Alianza Julai alipokutana na Rais wa Uswisi, Alein Berset alipoingia katika makubaliano ya nia ya kuona fedha zilizohifadhiwa katika mabenki ya nchi hiyo na Wakenya zinarejeshwa nchini humo na Agosti akakutana na Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May ambapo wamekubaliana kuwa mali na fedha taslimu za Wakenya zilizoko nchini humo na katika kisiwa cha Jersey zinaanza kurudishwa nchini humo.

Balozi wa Uswisi nchini Kenya, Jacques Pitteloud alisema kuwa nchi yake iko tayari wakati wowote kuzikamata fedha na mali ambazo zimehifadhiwa katika mabenki nchini humo ili zirudi zikasaidie watu masikini.

Juhudi za sasa inawezekana zikawa kama mpya, lakini kwa wafuatiliaji wa siasa za Kenya wanakumbuka mwaka 2003 wakati wa utawala wa Rais Mwai Kibaki chini ya aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma nchini humo, John Githongo kulipofanyika mambo mengi hasa ya kuchunguza mali na fedha hizo sehemu mbalimbali duniani.

Serikali ya Kenya inaamini kuwa kiasi cha Sh158 bilioni za Kenya zilizoibwa katika kashfa ya Goldenberg na 112 bilioni zilizoibwa katika kashfa nyingine ya Angloleasing zimefichwa katika akaunti za siri katika mabenki mbalimbali barani Ulaya.

Wakati wa utawala wa Kibaki, Serikali ya Kenya iliingia mkataba na kampuni binafsi ya mjini New York, Marekani kupeleleza na kufichua mabilioni ya dola na mali zinazohamishika na zisizohamishika zilizokuwa zimehifadhiwa ughaibuni.

Kampuni hiyo Kroll, iligundua kuwa baadhi ya fedha zilizoibiwa Kenya zilitumika kununulia hoteli mbili kubwa za kifahari, jijini London Uingereza, mahekalu ya kitajiri nje ya Jiji la London na magari ya kifahari. Wakati huo kampuni hiyo ilinasa kiasi cha dola bilioni 1 za Marekani ambazo zilikuwa zimefichwa na mafisadi ambao ni raia wa Kenya. Wapelelezi hao waligundua kuwa wezi hao walihifadhi fedha zao katika mabenki yanayoheshimika ulimwenguni.

Nchini Uswisi iligundulika kuwa kiasi cha shilingi za Kenya 160 bilioni zilihifadhiwa nchini humo.

Inaendelea uk 24

Inaendelea uk 24

Kampuni ilikabidhi taarifa yake kwa Serikali ya Kenya mwaka 2004 ingawa haikuwahi kutolewa kwa umma ilizitaja nchi za Uswisi, Uingereza, Luxembourg na baadhi ya visiwa vya Karibeani kuwa vilikuwa vinara katika kuhifadhi fedha zilizoibwa kutoka katika nchi hiyo.

Taarifa hiyo iliitaja Kenya kama nchi iliyokuwa na wizi na ulaji rushwa wa viwango sawa na wakati wa utawala wa Mobutu Sese Seko wa iliyokuwa Zaire sasa DRC, Nigeria ya Sani Abacha na Philipines ya Ferdinad Marcos.

Kampuni hiyo ilitumiwa na Serikali ya Nigeria wakati wa utawala wa Olusegun Obasanjo kufuatilia kiasi cha dola bilioni tatu za Marekani zilizoibwa wakati wa Utawala wa dikteta Sani Abacha kati ya mwaka 1993 hadi 1998 ambapo walifanikiwa kupata kiasi cha dola 1.5 kutoka mabenki ya Uswisi.

Vilevile nchi hiyo ilifanikiwa kurejeshewa kiasi cha dola milioni 149 kutoka katika kisiwa pepo kwa wakwepa kodi cha Jersey nchini Uingereza. Kenya ilikuwa nchi ya kwanza kusaini makubaliano ya umoja wa mataifa ya kupambana na rushwa UNCAC kwa sababu imekuwa mwathirika mkubwa wa vitendo hivyo, ambavyo kwa hakika vimemeza juhudi zote za kujenga uchumi imara wa nchi hiyo ambayo ilikuwa moja ya nchi zenye ustawi bora wa kiuchumi katika miaka ya sabini barani Afrika.

Kenya na Nigeria ni mifano tu, lakini ufisadi umetamalaki barani Afrika na kila nchi ina genge la wezi ambao ni watu binafsi wakishirikiana kwa karibu na vigogo ndani ya serikaki ambao wameamua kuwa fedha za kodi na misaada kutoka kwa wafadhili zinaibiwa na kwenda kuwekwa kwenye mataifa yaliyoendelea ambayo kwa hakika yanarudisha fedha hizohizo kuwa mikopo na misaada.

Mfano wa Tanzania

Nchini Tanzania katika kipindi cha mwisho wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete kulikuwa na juhudi ambazo ziliongozwa na mbunge kijana Zitto Kabwe, kujaribu kushawishi Serikali iongee na mataifa hayo ili kupata uwezekano wa kurejesha fedha ambazo zimefichwa huko, lakini inavyoonekana hoja hiyo kwa sasa imekosa mvuto ingawa mataifa hayo yapo tayari kufanya hivyo ikiwa serikali itafanya bidii kudai kilicho chake.

Miaka ya mwanzo baada ya uhuru wa nchi za Afrika hadi 1980, wizi wa fedha katika mataifa haya ulikuwa ukifanywa na maofisa wa serikali kwa kuiba fedha ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara, shule na hospitali ambapo wahusika walikuwa wakihamisha na kuzipeleka ughaibuni.

Kwa sasa hali imebadilika kuanzia pale Ukomunisti ulipo poromoka na mabadiliko ya kiuchumi duniani ambapo nchi zilianza kuvutia uwekezaji na mitaji kuanza kuvuka mipaka ya nchi, wizi wa fedha za umma umepata mwenza wake ambaye ni makampuni makubwa ambayo yameingia katika kuendeleza sekta mbalimbali za kiuchumi kama uchimbaji wa madini, uvuvi, utalii na kilimo.

Makampuni haya yakishirikiana na watendaji waovu walioko katika idara mbalimbali za serikali hasa katika kodi na sheria, wameendelea kuhujumu juhudi za kuendeleza uchumi na kuondoa umasikini kwa kuingia mikataba mibovu ya kisheria ambayo mwishoni inanyima mapato muhimu katika ukusanyaji wa kodi.

Makampuni yanatumia ujanja wa kupandisha gharama za uendeshaji na ununuzi wa huduma na mitambo ya kufanyia kazi na hapohapo kutoa ankara zinazoonyesha kuwa mapato ya uuzaji wa kile kilichopatikana ni madogo, hivyo kufanya mataifa ya Afrika yashindwe kupata fedha za kuhudumia watu wake.

Ukwepaji huu wa kodi ambao mara nyingi hufanywa kwa kukodi huduma kutoka makampuni mama ambayo yapo kwa majina katika makaratasi lakini kiuhalisia hayapo, ni hewa katika nchi ambazo ni maficho ya wakwepa kodi katika nchi za Panama, Visiwa vya Karibeani, Uswisi na Luxembourg.

Kitengo cha Uchumi cha Umoja wa Mataifa kanda ya Afrika (Uneca), mjini Addis Ababa, Ethiopia kinakadiria kuwa Afrika inapoteza kati ya dola bilioni 50 hadi 148 kwa mwaka kutokana na ukwepaji kodi na utoroshaji wa raslimali zilizopo barani Afrika. Upotevu huu ni mara tatu ya fedha za misaada zinazotolewa na nchi zilizoendelea duniani.

Hivyo basi, kama kutakuwa na udhibiti wa mapato na kuzuia wizi huu bara la Afrika linaweza kutoa mikopo kwa nchi tajiri kama ifanyavyo China.

Nchi zilizoendelea kiviwanda duniani (G8) mwaka 2008 zilikubaliana kuwa ni lazima kila nchi iwe na mikakati ya kuonyesha namna inavyoweza kuyabana makampuni yanawekeza katika nchi masikini kwa sababu bila kufanya hivyo, nchi hizi nazo zilikuwa zikipoteza kodi.

Mwaka huohuo Marekani ilitunga sheria ya kuzilazimisha nchi kama Uswisi ambazo zilikuwa zimegubikwa na usiri mkubwa kutoa majina ya Wamarekani ambao walikuwa na akaunti zao katika mabenki ya nchi hiyo ili walipe kodi nchini mwao.

Baada ya hapo Uswisi nayo ikatunga sheria ya kutaifisha fedha za raia wa kigeni ambao wanaonekana kuwa na fedha ambazo hazina maelezo jinsi zilivyopatikana na kuruhusu mataifa mengine kuomba taarifa za raia wao ambao ni wateja katika mabenki ya nchi hiyo, tofauti na ilivyokuwa mwanzo.

Juhudi za kurejesha fedha zilizoibwa kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika ni ngumu kwa sababu ya vikwazo tofauti ambavyo bado vipo, hasa sheria zinazoongoza mabenki makubwa duniani ambapo mfanyakazi wa kawaida hawezi kutoa siri ya mteja.

Kuwepo kwa maofisa wa serikali ambao wanaweza kufanya juhudi hizo lakini kwa kuwa ndiyo wahusika wa wizi huo basi hakuna kinachoendelea na hili linaonekana wazi kwani licha ya nchi za Marekani, Uswisi na Uingereza kuwa tayari kushirikiana na nchi za Afrika kutafuta zilipo fedha zao lakini ni nchi chache sana zimeitikia wito huo.

Afrika ina tatizo kubwa la kuwepo kwa wataalamu wazuri wa masuala ya kodi na sheria kwa sababu ili kurejesha fedha zilizoibwa au kodi iliyokwepwa, kunahitajika wapelelezi wenye utaalamu wa juu na wabobezi wa sheria za kimataifa za mabenki.

Kwa kuwa wanaoiba fedha kutoka katika mataifa ya Afrika wana ukwasi mkubwa, hivyo basi wana uwezo wa kuajiri wanasheria wa viwango vya kimataifa hivyo basi zoezi zima linakuwa la gharama kubwa wakati mwingine kuliko hata hizo fedha zinazopiganiwa.

Ni wajibu wa viongozi wa nchi za Afrika kuungana na Rais Kenyatta kudai kurudishwa kwa fedha zilizoibwa kutoka barani humu, kwani mataifa tajiri yanayohifadhi fedha hizo yako tayari kutoa ushirikiano wa hali na mali unaohitajika. Fedha za mikopo na misaada zinazotolewa na mabenki na mataifa ya Ulaya zinakuwa mzigo mzito usiobebeka na unatishia ustawi wa kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiusalama wa mataifa hayo.

[email protected] Simu 0783 165 487