Mastaa 20 waliokacha mataifa ya asili

Muktasari:

  • Fainali za Russia zitabaki kwenye vitabu vya kumbukumbu kama ilivyokuwa miaka 88 iliyopita ambapo zilifanyika kwa mara ya kwanza Bara la Amerika ya Kusini kwenye Taifa la Uruguay mwaka 1930.

Eliya Solomon, Mwananchi

Kuanzia Julai 16, 2018 tumeanza safari nyingine ya kupanda milima na mabonde kuelekea kwenye miaka mingine minne ya kushuhudia Fainali za Kombe la Dunia ambazo zitafanyika kwa mara ya kwanza katika nchi za kiarabu, nchini Qatar mwaka 2022.

Fainali za Russia zitabaki kwenye vitabu vya kumbukumbu kama ilivyokuwa miaka 88 iliyopita ambapo zilifanyika kwa mara ya kwanza Bara la Amerika ya Kusini kwenye Taifa la Uruguay mwaka 1930.

Uruguay ni Taifa la Kihistoria katika soka ingawa Brazil inaongoza kwa kutwaa ubingwa mara tano, lakini Taifa hilo lilibakiza kombe hilo kwenye ardhi ya nyumbani Julai 30, 1930.

Pamoja na hayo, Spoti Mikiki inakuletea orodha ya nyota 20 ambao walicheza Fainali za Kombe la Dunia nchini Russia, katika mataifa ya ‘kuazima’ sio kwenye mataifa yao halisi, je! Unawafahamu?

Kylian Mbappe (Cameroon)

Mshambuliaji aliyeng’ara na kutwaa tuzo ya mchezaji bora chipukizi wa fainali za Kombe la Dunia 2018, Kylian Mbappe akifunga mabao manne yaliyochangia kukipa kikosi cha Kocha Didier Deschamps ubingwa, asili yake ni Afrika kutoka Cameroon.

Mshambuliaji huyo wa Paris Saint German (PSG) ya Ufaransa, baba yake Wilfried ni mzaliwa wa Cameroon na mama yake Fayza Lamari anatoka Algeria.

Kuzaliwa kwake Ufaransa kulimpa fursa ya kuchukua uraia wa nchi hiyo ambapo alianza kucheza soka tangu mwaka 2014 ngazi ya vijana.

Diego Costa (Brazil)

Mshambuliaji wa Hispania, Diego Costa asili yake ni Brazil. Costa alizaliwa Lagarto nchini Brazil na wazazi wake Jose de Jesus na Josileide mwaka 1988 na alipewa jina la Diego kutokana na ‘mambo’ makubwa yaliyofanywa na Diego Maradona wa Argentina. Costa aliwahi kukaririwa akidai ameichagua Hispania baada ya kukosa nafasi ya kucheza timu ya Taifa ya Brazil.

N’golo Kante (Mali)

Wazazi wa N’golo Kante walihama kutoka nchini kwao Mali mwaka 1980 na kwenda Ufaransa ambako miaka 11 baadaye alizaliwa kiungo huyo wa Chelsea, ambaye amedhihirisha ni mmoja wa viungo bora kuwahi kutokea duniani.

Mesut Ozil (Uturuki)

Ozil ni kiungo mahiri wa Ujerumani mwenye asili ya Uturuki. Nyota huyo wa Arsenal aliwahi kukaririwa akidai bado analipenda Taifa lake la asili.

Paul Pogba (Guinea)

Pogba ni Mfaransa mwingine mwenye asili ya Afrika, wazazi wa kiungo huyo wa Manchester United walitokea Afrika nchini Guinea kabla ya kwenda Ufaransa ambako mchezaji huyo alizaliwa, Machi 15, 1993.

Jerome Boateng (Ghana)

Libero wa Bayern Munich, Jerome aliyeitumikia Ujerumani kwenye Fainali za Kombe la Dunia asili yake ni Ghana, baba yake ametokea kwenye Taifa hilo la Afrika.

Thiago Alcantara (Brazil)

Baba wa Thiago, Mazinho alikuwa mchezaji wa timu ya Taifa la Brazil kwenye miaka ambayo alizaliwa mwanaye anayecheza Bayern Munich, mtoto huyo wa Kibrazil amechagua kuitumikia Hispania, alizaliwa Aprili 11, 1991.

Samuel Umtiti (Cameroon)

Umtiti ni ‘mtoto’ wa mjini katika Jijini la Yaounde nchini Cameroon ambako aliishi kwa miaka miwili kabla ya familia yake kwenda Ufaransa, ambako alinza kucheza soka kwenye klabu ya Menival na Lyon kabla ya kujiunga na Barcelona, amechagua kuitumikia Ufaransa.

Pepe (Brazil)

Kabla ya kuchukuwa uraia wa Ureno, Pepe ambaye anacheza katika kikosi cha Besiktas ya Uturuki ni mzaliwa wa Brazil na imebainika alikuwa na mpango wa kuitumikia Brazil, lakini baada ya kuona muda unakatika na haitwi aliamua kusaka nafasi Ureno.

Blaise Matuidi (Angola)

Matuidi ni mtoto wa Muangola, Faria Rivelino na mama ambaye ni raia wa DRC Congo, Elise. Blaise alizaliwa Toulouse, Ufaransa na amekulia na kuchukua uraia wa Taifa hilo ambalo limejaa nyota wengi wenye asili ya Afrika. Ni mmoja wa wachezaji walioipa Ufaransa taji.

Marouane Fellaine (Morocco)

Abdellatif ni baba wa nyota wa zamani wa Everton, Fellaine.Baba wa kiungo huyo wa zamani wa Everton alikuwa kipa wa Raja Casablanca ya Morocco ambako alimpata mchezaji huyo aliyeamua kuitumikia Ubelgiji.

Dele Alli (Nigeria)

Pamoja na Dele kuzaliwa kwake Milton Keynes ni mtoto wa Mnigeria, Kehinde ambaye aliishi naye kwa muda mfupi kabla ya kuishi na mama yake Denise nchini England.

Michy Batshuayi (DR Congo)

Michy ambaye asili yake ni Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) aliamua kucheza Ubelgiji. Mwaka 2015 aliombwa na Chama cha Soka DRC kuitumikia nchi hiyo alikataa na kuichagua Ubelgiji.

Raheem Sterling (Jamaica)

Sterling ni mchezaji wa England mwenye asili ya Jamaica, winga huyo wa Manchester City, alihama na mama yake kutoka Jamaica na kwenda England akiwa na miaka miwili baada ya baba yake kufariki.

Romelu Lukaku (DR Congo)

Wazazi wa Lukaku ni Wacongo, lakini kuzaliwa kwake mjini Antwerp nchini Ubelgiji kulimfanya kuchukuwa uraia wa nchi hiyo ambayo alianza kucheza mwaka 2008 katika timu za vijana.

Yussuf Poulsen (Tanzania)

Kutopokea ofa ya kuitumikia Taifa Stars ndiyo sababu iliyomfanya Poulsea, kuchukuwa uraia wa Denmark. Mshambuliaji huyo aliweka rekodi kwenye Fainali za Kombe la Dunia kwa kuwa mchezaji wa kwanza mwenye asili ya Tanzania kucheza na kufunga bao katika mashindano hayo.

Yvon Mvogo (Cameroon)

Mvogo ambaye ni kipa wa Sweden alizaliwa Yaounde, Cameroon, kabla ya kuhamia nchini Sweden, ambako anapata heshima kubwa kutokana na kipaji chake cha kucheza soka ya ushindani.

Sami Khedira (Tunisia)

Khedira alizaliwa Stuttgart nchini Ujerumani. Baba yake ni Mtunisia na mama yake ni Mjerumani, ameamua kuitumikia Ujerumani.

Breel Embolo (Cameroon)

Embolo ni mzaliwa wa mji wa Yaounde nchini Cameroon, mama yake alihamia mjini Basel nchini Uswisi kusaka maisha na mchezaji huyo alianzia soka katika timu za vijana za Uswisi kabla ya kuchagua kuichezea timu ya Taifa hilo.

Martin Olsson (Kenya)

Olsson alizaliwa Gavle, Sweden akiwa na pacha na kaka yake, Marcus, ambaye pia ni mwanasoka wa klabu ya Derby County ya England. Wazazi wao ni mchanganyiko baba anatoka Sweden mama Kenya.