Mazao ya kilimo hai yalivyo na soko kitaifa na kimataifa

Muktasari:

  • Mazao yanayozalishwa kwa kutumia kilimo hiki kwa kawaida huwa na bei ya juu, kutokana na ukweli kuwa ni salama zaidi kwa afya ya mlaji.

Kilimo hai ni kilimo kisichotumia mbolea wala dawa za viwandani katika uzalishaji wa mazao yake.

Mazao yanayozalishwa kwa kutumia kilimo hiki kwa kawaida huwa na bei ya juu, kutokana na ukweli kuwa ni salama zaidi kwa afya ya mlaji.

Aidha, mazao hayo hayana madhara ya muda mfupi wala mrefu, hivyo mtumiaji hana hofu ya kupatwa na magonjwa.

Utafiti unaonyesha kuwa katika soko la dunia bei ya mazao ambayo hayakutumia kemikali aina yoyote, imekuwa ikiongezeka kulinganisha na yale ambayo yamekuwa yakitumia kemikali hizo.

Wakati bei za mazao kama kahawa, pamba na sukari zimekuwa zikiyumba katika soko hilo, bei ya mbogamboga katika soko hilo imekuwa ikiongezeka na kuwapatia fedha nyingi wakulima wanaolima zao hilo kwa kutumia mfumo wa kilimo hai.

Hata hivyo, wanaharakati wa kuendeleza kilimo hai wamefanikiwa kuwashawishi wakulima kujihusisha na kilimo hai baada ya kuelezwa faida za kuuza kwa bei ya juu na umuhimu wa kutunza mazingira.

Wakulima wanasemaje?

Mkulima anayezalisha mazao kwa kufuata misingi ya kilimo hai, Zadock Kitomari anasema kuwa, unapoanza kujishughulisha na kilimo hai ambacho hakitumii kemikali unaona kuwa uzalishaji unakuwa mdogo, lakini kwa kadri unavyoendelea uzalishaji unakuwa mkubwa.

Anaeleza kuwa, kilimo hai ni aina ya kilimo kinachoangalia uhai wa mazingira, uhakika na usalama wa mlaji na usalama wa chakula, jambo linalomhakikishia mkulima kipato kwa kutumia fursa alizonazo.

Akizungumzia upatikanaji wa masoko ya kilimo hai, Kitomari anasema; “Masoko ya kilimo hai yapo, isipokuwa yanapatikana tu kwa wale wakulima waliothibitishwa na kufanyiwa utafiti kuwa ni kweli mazao yao yanazalishwa kwa misingi ya kilimo hai.”

Anasema kuwa, mashirika kama OICOS, na MESULA yamekuwa yakisaidia wakulima kwa kiasi kikubwa kujiingiza katika vikundi vya uzalishaji kwa misingi ya kilimo hai, kuwapa elimu sahihi kuhusu kilimo hai pamoja na kuwatafutia masoko ya pamoja.

Anaongeza kuwa, wakulima wengi wamekuwa wakilalamika kuwa hakuna soko lakini tatizo kubwa hawajajikita hasa katika uzalishaji kwa kufuata misingi ya kilimo hai.

Aidha, wanatakiwa kuangalia jamii inayowazunguka kwanza kwani soko linaanzia nyumbani kabla ya kuingia katika masoko makubwa.

Sifa za shamba la kilimo hai

Moja, ni lazima eneo lako la kilimo liwe na mboji. Wakulima wengi wanadai kuwa wanafanya kilimo hai lakini ukitembelea maeneo yao hayana mboji.

Mbili, hakikisha unatengeneza mboji hiyo kila wakati kwa kutumia mabaki ya mifugo na mazalia mengine isipokuwa taka ngumu.

Tatu, Lazima shamba liwe na uzio kwa ajili ya kuzuia sumu kali zinazotoka kwenye mashamba yanayotumia kemikali na dawa za viwandani na hata kuzuia wanyama waharibifu.

Nne, uzio wa mkulima wa kilimo hai lazima uwe na miti ya dawa, ambayo hukinga wadudu waharibifu na pia hutumiwa kutengenezea dawa.

Tano, mkulima wa mazao ya kilimo hai ni lazima awe na elimu ya kutosha juu ya kilimo hai na aweze kuwaelimisha na kuwashauri wakulima wenzake waliomzunguka kuhusu faida na hasara za kilimo hai.

Kauli ya wataalamu

Wataalamu mbalimbali wanaeleza kuwa, kwa sasa bidhaa zinazotokanana kilimo hai zinazidi kuongezeka na hii ni kutokana na baadhi ya wanajamii kufahamu kwa kiasi kikubwa madhara yanayotokana na mazao yanayozalishwa kwa kutumia madawa na kemikali za viwandani.

Lukas Rwechoka, anasema wakulima wamekuwa na mwamko mkubwa kuhusiana na uzalishaji wa mazao na bidhaa za kilimo hai, ila tatizo kubwa limekuwa soko ambalo mara kwa mara limekuwa likiwakatisha tamaa ya kuendelea kuzalisha bidhaa hizo.

Je, wakulima wanatakiwa kufanya nini ili kuondokana na tatizo hili? Wakulima wa mazao ya kilimo hai wanatakiwa wawe waaminifu na wafuatae misingi yote ya uzalishaji wa mazao ya kilimo hai.

Aidha, wasiwe wadanganyifu katika shughuli nzima ya uzalishaji wa mazao na bidhaa zote zitokanazo na kilimo hai.

Uelewa kwa walaji wa ndani nao bado ni changamoto kubwa. Kuhusu walaji wa nje, wao wana uelewa mkubwa na wakisaidiwa na sera za nchi zao na ufafanuzi mzuri juu ya mazao yatokanayo na kilimo hai.

Je, kuna njia yoyote ambayo wakulima wanaweza kutumia kurahisisha upatikanaji wa soko la bidhaa za kilimo hai wanazozalisha?

Rwechoka anasema: “Njia ambayo wakulima wanaweza kutumia kurahisisha upatikanaji wa soko la bidhaa za kilimo hai ni kuwa wakweli na waaminifu katika shughuli zote za kilimo hai.

Anaongeza: ‘’Wanatakiwa kuwa na takwimu sahihi na kufahamu kwa ufasaha hatua za uzalishaji tangu kulima, kupanda, kuhudumia mazao, kuvuna na kuhifadhi mazao hayo. Ili kufanikisha hayo, hakuna budi kuwaruhusu wakaguzi (mawakala) wa kilimo hai walioidhinishwa wafanye ukaguzi na kutoa mwongozo na ushauri juu ya suala zima na kuwataarifu wanunuzi juu ya hatua sahihi zilizofuatwa katika kilimo hai.’’

Makala haya ni kwa hisani ya mtandao wa mkulimambunifu. www.mkulimambunifu.org