#WC2018: Mbappe kautendea haki umri wake Russia

Muktasari:

  • Mbappe aliwaacha midomo wazi wapenzi wa soka kwenye mchezo wa robo fainali dhidi ya Argentina kwa kufunga mara mbili kwenye mchezo huo ambao walishinda kwa mabao 4-3.

Fainali za Kombe la Dunia kule Russia zimemalizika lakini kulikuwa na dogo mmoja tu, huyu anachezea Paris Saint-Germain na timu ya taifa la Ufaransa, Anaitwa Kylian Mbappe, alikuwa gumzo kutokana na kiwango alichokionyesha kwenye fainali hizo za Russia.

Mbappe aliwaacha midomo wazi wapenzi wa soka kwenye mchezo wa robo fainali dhidi ya Argentina kwa kufunga mara mbili kwenye mchezo huo ambao walishinda kwa mabao 4-3.

Hapo ndipo alipoifikia rekodi ya Pele ya mwaka 1958 kwa kufunga mabao mawili katika mechi moja ya fainali za Kombe la Dunia akiwa na umri mdogo.

Mbappe ni mzaliwa wa Ufaransa japo baba yake, Wilfried alitokea Cameroon wakati huo mama yake, Fayza Lamari akitokea Algeria.

Wilfried ambaye ni baba wa Mbappe anajihusisha na masuala ya soka kwa kuwa wakala, mama yake naye alikuwa mchezaji wa zamani wa mchezo wa mpira wa mikono.

Mshambuliaji huyo ambaye alizaliwa Desemba 20, 1998 alianza kucheza soka la vijana kwenye akademi ya AS Bondy, 2004 akiwa na umri wa miaka sita, alidumu kwenye kituo hicho hadi 2013.

Ndani ya mwaka huo wa 2013, Mbappe alijunga na akademi nyingine ya Monaco, pindi akiwa kwenye akademi hiyo alianza kupata nafasi za kucheza mara kwa mara kwenye timu za taifa za vijana za Ufaransa.

Kiwango chake bora, kiliifanya Monaco kumpandisha msimu wa 2015/16 kwenye kikosi B cha timu hiyo, lakini hakudumu na baadaye akapandishwa kwenye kikosi cha kwanza na kupata nafasi ya kucheza moja kwa moja.

Msimu wa 2016/17, Mbappe alifunga mabao matatu ‘hat trick’ kwa mara ya kwanza kwenye kombe la ligi dhidi ya dhidi Stade Rennais, Disemba 14, 2016, Monaco ilishinda mchezo huo kwa mabao 7-0.

Februari 11 ndani ya mwaka huo,Mbappé alifunga mabao matatu mengine kwenye mchezo mmoja upande wa Ligi Kuu Ufaransa ‘Ligue 1’ dhidi ya Metz , wakiibuka na ushindi wa jumla ya mabao 5-0.

Baada ya kuwa na msimu mzuri akiwa na Monaco, Psg ilimchukua kwa mkopo na alipofanya vizuri kwa kipindi kifupi alisajiliwa moja kwa moja na matajiri hao wa Ufaransa.

Mbappe alitua Psg kwa kuweka rekodi ya kuwa mchezaji ghari zaidi kijana ambaye aliigharimu timu hiyo, Euro 145 million. Mbappe ni kati ya mchezaji ghali zaidi duniani akiwemo Neymar.

Wenzake na Mbappe

Ukimwacha mchezaji huyo, wapo wa miaka kati ya 20 na 21 waliotisha Kombe la Dunia. Baadhi yao ni Gabriel Jesus, 20, (Man City), Albert Gudmundsson, 20, (Iceland) anachezea pia, PSV Eindhoven.

Marcus Rashford, 20, anachezea England na Manchester United, Kasper Dolberg (Denmark) na Ajax, Ousmane Dembélé (Ufaransa) na Barcelona, Achraf Hakimi (Morocco) na Real na Luka Jovic anayechezea Frankfurt ya Serbia.

Pia yumo Trent Alexander-Arnold, 21, ( England) na Liverpool na pia dogo mwingine ni Ruben Dias (Ureno) anayechezea SL Benfica. Vijana hao wana uwezo wa kucheza fainali nyingine mbili, ya 2022 Qatar na zile za Marekani/Mexico na Canada za 2026.