Mbinu nne za kupambana na unyanyasaji wa ‘kingono’ kazini

Kila mara zinaibuka tuhuma za unyanyasaji unaohusishwa vitendo vya kuombwa au kulazimishwa kufanya ngono maofisini. Ingawa wanaume pia hunyanyaswa, kwa kiasi kikubwa wanawake ndio waathirika wakubwa. Mara nyingi huwa ni mabinti wenye umri mdogo, wanaofanya kazi katika nafasi za chini wakisimamiwa na wanaume waliowazidi umri. Makundi haya ndio huathirika zaidi.

Uwiano wa unyanyasaji wa kijinsia unaonyesha takribani asilimia 85 ya wanawake makazini wamewahi kukumbana na vitendo vya unyanyasaji wa aina hii huku wanaume ikiwa asilimia 43. Inaeleza taarifa ya utafiti uliowahi kufanywa na taasisi wa Kimarekani ya Center on Gender Equity and Health uliotolewa mapema mwaka huu. Mwishoni mwa mwaka jana harakati zilizopewa jina maarufu la #MeToo ziliendeshwa duniani kote ambako wanawake wengi walijitokeza kukiri kunyanyaswa na mabosi wao au wasimamizi wanaume kazini.

Kashfa iliyomkumba mcheza sinema maarufu Bill Cosby na bilionea mtayarishaji wa filamu Harvey Weistein inatoa taswira ya mazingira ambayo wanawake wengi wanapitia katika mazingira ya kazi. Zilikuwa taarifa za kushtusha kwamba kumbe hata wanawake waliojiimarisha au kupata heshima wakiwamo waigizaji wakubwa na wanamuziki duniani nao walipitia katika mkondo huo.

Hii iliamsha woga wa kuhoji: “Mimi ni nani hata nisikumbane na vitendo hivi kazini ikiwa wanawake ninawaona mfano nao hawakuweza kuiepuka kadhia hii?”

Hata hivyo, wanawake na baadhi ya wanaume wanaonyanyaswa kingono kazini wana nafasi ya kuripoti uhalifu huo kwa wakubwa wao ikiwamo vyama vya wafanyakazi au mamlaka nyingine za Serikali inapobidi.

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, Tumaini Nyamhokya anakiri kwamba kuna changamoto katika ufuatiliaji wa kesi za unyanyasaji wa aina hii makazini hasa linapokuja suala la kutoa ushahidi kwa kuwa wengi hawafahamu namna ya kuweza kuwanasa.

“Kuna unyanyasaji wa aina nyingi ambao unatokea makazini na huu wa kingono ukiwamo, hapa kwetu (nchini) bado kuna kaugumu fulani hasa kwa sababu halijachukuliwa kwa uzito ndio maana wanaokumbana na kadhia hizi wengi huishia kushindwa katika madai yao kutokana na kukosekana kwa ushahidi,” anasema.

Pia baadhi ya waathirika kuona soni kutoa taarifa wanapokumbana na kadhia hii au kuhofia kupoteza kazi ni changamoto nyingine kubwa inayowakabili.

Kupitia vyama vya wafanyakazi, Nyamhokya anasema wamekuwa wakitoa mafunzo na kuhimiza waajiri kufanya hivyo kwa wafanyakazi wao ili wajue nini cha kufanya wanapokutwa na mikasa ya aina hii.

“Iwe mwanamke au mwanamume, linapokuja suala la kuthibitisha kuwa amenyanyaswa kingono ni lazima aonyeshe kuwa kitendo hicho kinaathiri utendaji wake wa kazi na kilifanywa kwake kutokana na jinsia yake,” anasema.

Unatakiwa kufanya haya unaponyanyaswa kingono

Wakili wa kujitegemea, Abdul Lyana anasema hakuna kesi ngumu duniani linapokuja suala la ushahidi kama za aina hii kwa sababu wengi hutengeneza mazingira ambayo kumkamata inakuwa ngumu.

Kwa kuwa wengi hawazifahamu sera za mahali wanapofanyia kazi, unapokutana na unyanyasaji wa kingono, unatakiwa kuisoma sera na kuchukua hatua stahiki kama inavyoelekezwa.

Mwathirika anatakiwa kuandaa taarifa kamili kuhusiana na matukio hayo kwa kuandika katika karatasi kila alichoambiwa au kitendo alichofanyiwa. Kama ana shahidi au mashahidi anaweza kuuorodhesha.

Katika hatua nyingine anashauriwa kuwashirikisha watu wake wa karibu kama vile marafiki au ndugu kwa kuwa vitendo hivi husababisha msongo wa mawazo na kushusha ari ya kufanya kazi.

Hii inaelezwa kuwa hatua muhimu katika kupambana na unyanyasaji wa kingono kazini kwa kuwa matukio kama haya huacha vidonda katika maisha hata kama hatachukua hatua zaidi.

Baada ya yote hayo hatua inayofuata ni kutoa taarifa kwa kiongozi wake. Anaweza kuwa ofisa anayemsimamia moja kwa moja au ofisa rasilimali watu. Pia unaweza kuwasilisha malalamiko kwa kiongozi wa umoja wa wafanyakazi au mwakilishi wa vyama vya wafanyakazi ingawa haulazimishwi kufanya hivi iwapo unaona hawawezi kuwa na msaada katika shauri lako.

Unawezaje kuthibitishwa kunyanyaswa kingono?

Kwa kuwa ushahidi wa kunyanyaswa kingono hupambwa na maneno ‘alisema’, ‘akasema’, ‘akanishika hapa’, Mtaalamu wa mwanasheria wa masuala ya kazi, Jean Boler anasema ni vyema kuweka katika maandishi kila tukio na iwapo mawasiliano yanafanyika kwa njia ya simu, tafuta namna yoyote ya kurekodi na kama ni ujumbe mfupi wa maandishi (sms) na uhifadhi. Ili kuthibitisha unyanyasaji wa kingono hakikisha unaweka katika maandishi mtiririko wa matukio hayo kwa kuandika eneo, tarehe na muda ambao mhusika amekuwa akikufanyia unyanyasaji. Orodhesha kila kinachotokea ikiwamo matamshi na matendo aliyokufanyia mnyanyasaji.

Kukua kwa teknolojia kunaweza kusaidia katika ushahidi kwa kutafuta picha za video kutoka katika maeneo mliyokutana. Pia unaweza kumrekodi kwa simu bila mwenyewe kufahamu au unaweza kumuweka mtu wa tatu kwa aajili ya kazi hiyo.

Uzalishaji kazini

Mtoa taarifa ya kunyanyaswa kazini anaweza ashindwe katika shtaka hilo iwapo utendaji wake kazini siyo mzuri kwani mhusika anaweza kujitetea kuwa ni mbinu ya kujitetea kutokana na utendaji wake mbovu akisaidiwa na rekodi mbalimbali zilizopo ofisini kama vile onyo au kusimamishwa kazi.

Ingawa inaweza kuwa sehemu ya utetezi kuwa umeshindwa kufanya vizuri kutokana na vitendo hivyo, ni vizuri kuwa na rekodi nzuri ya kazi wakati wote. Hii pia itakusaidia kutozingirwa na ‘mafisi’ wanaotaka kutumia udhaifu wa kushindwa kufanya kazi.

Je, unaweza kutoa taarifa polisi?

Lyana anasema kutokana na mazingira mdai anaweza kulifikisha suala hilo polisi na baadaye kesi ikasikilizwa mahakamani ikiwa ya kijamii (civil) au jinai.

“Inategemea na namna muhusika amekuwa akitendewa, kama alikuwa akipewa vitisho hiyo itakuwa jinai,” anasema.

Hukumu ya kesi hizi inaweza kuwa fidia au kifungo iwapo kesi hiyo ilifunguliwa kama jinai kutokana na ushahidi wa mdai aliouwasilisha mahakamani.