Mipango ya maendeleo izingatie matumizi ya takwimu

Muktasari:

  • Kila kukicha, mipango kadhaa huwekwa kwa ajili ya kutatua kero zilizopo kwenye jamii. Kufanikisha kila linalopangwa, matumizi ya takwimu yanahitajika. Zipo mamlaka zinazoongoza na kusimamia ukusanyaji wa takwimu, lakini takwimu za ndani pia zinaweza kusaidia kufanikisha dhamira hii.

Serikali kupitia taasisi zake inabuni, kuendeleza na kusimamia miundombinu ya ukusanyaji wa takwimu nchini. Upatikanaji wa takwimu kwa kiasi kikubwa sio changamoto tena.

Idara za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika taasisi nyingi zimeimarisha mifumo ya ukusanyaji wa takwimu kuanzia ngazi ya chini ya utendaji kwa matumizi mbalimbali.

Umuhimu wa takwimu sio agenda tena, wengi wanatambua umuhimu wake katika kupanga mipango ya maendeleo na mgawanyo wa rasilimali. Swali la msingi ni taasisi ngapi zinatumia takwimu zilizopo kama nyenzo ya kufanya uamuzi wa masuala tofauti. Taasisi mbalimbali za Serikali na sekta binafsi zinatumia fedha nyingi kukusanya takwimu kila mwaka. Hii inahusisha takwimu zinazokusanywa wakati wa sensa na utafiti mbalimbali.

Kukusanya, kuchakata na kuziweka takwimu kwenye mfumo unaofaa kwa matumizi pamoja na kuzihifadhi kwa matumizi ya baadaye ni gharama kubwa.

Mbali na matumizi ya kiasi kikubwa cha fedha kuwekeza kwenye miundombinu ya ukusanyaji na uhifadhi wa takwimu ikiwamo kuandaa madodoso, mifumo ya Tehama, vyombo vya usafiri, posho, shajala na gharama nyingine, matumizi ya takwimu bado ni changamoto katika taasisi mbalimbali iwe za uma hata binafsi.

Mwaka 2015 Marekani linatajwa kutumia takwimu za ofisi ya sensa ya nchi hiyo kufanya uamuzi wa kutumia Dola 675 bilioni kutekeleza programu 132 na mwaka 2009 ikatumia Dola 400 bilioni.

Dunia ya sasa haishii kwenye kukusanya takwimu bali inawekeza zaidi kwenye matumizi yake. Zipo taasisi nyingi ambazo zina takwimu nyingi lakini hazitumiki kama nyenzo muhimu ya kufanya uamuzi sahihi utkaosaidia kutatua tatizo lililopo.

Sheria ya takwimu ya mwaka 2015 inaeleza moja ya majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ni kuishauri Serikali na jamii kwa ujumla katika masuala yote yahusuyo takwimu rasmi.

Serikali na jamii kwa ujumla haipaswi kufanya uamuzi wowote wa kutekeleza mradi wa maendeleo au uwekezaji wa muda mrefu bila kuwa na takwimu sahihi kutoka mamlaka iliyopewa jukumu hilo kisheria au chanzo kingine cha uhakika.

Matumizi ya takwimu ni muhimu sana katika kupanga kutoa au kutokutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza jambo lolote linaloonekana kuwa na ushawishi. Serikali inapotaka kutoa fedha kwa ajili ya hudumaya jamii au uchumi katika eneo fulani ni vyema takwimu zikatumika kuongeza uzito wake.

Endapo utafanywa uamuzi wa kutoa fedha, utoaji wa fedha kwa taasisi unapaswa kufikiwa kwa kutumia takwimu pia. Takwimu zitaonesha uadilifu na uamini wa taasisi husika.

Matumizi ya takwimu yanasaidia kufanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi au programu mbalimbali zinazoanzishwa na Serikali au wadau wengine wa maendeleo au uendelezaji wa jamii kwa namna yoyote iwayo.

Ipo mifumo inayokusanya takwimu kuanzia ngazi ya kituo; elimu na afya. Mifumo hiyo inapaswa imuwezeshe mkuu wa taasisi kuzitumia kuweka mikakati na kupanga mipango ya maendeleo na mgawanyo wa rasilimali katika taasisi yake. Hivyo hivyo kwa ngazi ya halmashauri na mikoa.

Miongoni mwa changamoto zinazodhoofisha upatikanaji wa takwimu sahihi ni kwa mkusanyaji au mtoa takwimu kutokuwa na uwezo wa kuzitumia takwimu anazokusanya kuweka mipango au kufanya uamuzi.

Wataalamu wanasema umuhimu wa takwimu unaonekana pale zinapotumika, sio zinapokusanywa. Endapo taarifa zozote zitakusanywa kisha ripoti yake ikafungiwa kabatini, tatizo lililopo halitotatuliwa wala mradi uliopangwa hautotekelezwa kwa viwango vinavyotarajiwa.

Kwa kuona umuhimu wa kukusanya na kutumia takwimu kwenye maeneo tofauti ya kimkakati, sheria ya takwimu ya mwaka 1999 iliekeza sensa ya watu na makazi ifanyike kila baada ya miaka 5 kuanzia mwaka 2001 nchini Afrika Kusini.

Haituwa na tija wala haitaleta maana endapo Serikali itaendelea kuwekeza rasilimali ikiwamo fedha za walipa kodi katika kukusanya takwimu bila kuhakikisha zinatumika katika ngazi mbalimbali kufanya uamuzi sahihi na wenye tija kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Matumizi ya takwimu ni nyenzo ya kutuonyesha endapo tutafikia uchumi wa kati kabla au ifikapo 2025 na kupima mwenendo wa viashiria vingine vya kiuchumi na kijamii.

Ni muhimu kuendelea kusisitiza matumizi ya takwimu wakati upatikanaji na ubora wake ukiendelea kuimarishwa.

Takwimu zinabeba mafanikio ya shughuli mbalimbali. Kitengo cha uokozi hakiwezi kujipanga kama hakifahamu ni watu wangapi wamehusika kwenye janga lililotokea mahali popote ambako msaada unahitajika.

Serikali pia haiwezi kukiimarisha kikosi hicho kama haina takwimu za watu wanaohitaji huduma zake wakati wowote ili kufanya maandalizi yanayohitajika.

Idara za Serikali zinapaswa kushiriki kukusanya takwimu zitakazosaidia matumizi ya ndani hasa utekelezaji wa majukumu yake.