Misingi ya utawala bora inatikiswa, tuzinduke

Wednesday August 8 2018

 

Ni dhahiri sasa kwamba katika kipindi cha miaka miwili sasa tunashuhudia matamko ya kisiasa yakianza kuchukua nafasi ya sheria na suala hili limeanza kutikisa misingi ya utawala bora.

Misingi ya utawala bora inataka kufuatwa kwa utawala wa sheria, kuheshimu katiba, haki za binadamu na mgawanyo wa madaraka.

Lord Denning aliyekuwa Jaji wa Uingereza ambaye alipanua mtazamo wa mahakama za Jumuiya ya Madola, aliwahi kusema “Once great power is granted, there is a danger of it being abused.”, akimaanisha kwamba “pale ambapo madaraka makubwa yanatolewa kwa mtu basi ipo hatari kubwa kwamba yanaweza kutumiwa vibaya.”

Maneno haya ya Jaji Denning yanaakisi kile kinachotokea sasa nchini mwetu ambapo baadhi ya viongozi wamehama kutoka kuongoza kwa sheria na kuongoza kwa matamko ya kisiasa.

Tena matamko mengine yana kila chembe ya ubaguzi ambayo imekatazwa na ibara 12 ya katiba yetu, bahati mbaya sana hatujasikia wakichukuliwa hatua za kisheria. Msumeno unakata upande mmoja.

Tumesikia matamko yanayoashiria kuwaingiza watumishi wa umma katika siasa, jambo ambalo ni la hatari katika nchi ambayo inafuata mfumo wa vyama vingi vya siasa tena tangu 1992.

Matamko na maagizo yanayokinzana na Katiba yetu na sheria zetu zilizotungwa na Bunge ni mengi na kama ningeyaorodhesha hapa nafikiri makala hii ingekuwa labda na maneno 3,000.

Ni lazima tutambue kuwa kuwabana wale walio madarakani ili wasitumie vibaya madaraka waliyopewa kisheria, ndio hatua ya kwanza ya kusimika utawala wa sheria katika nchi yetu.

Kwanza sheria zinazotoa madaraka lazima zitafsiriwe na mahakama kwa ukali mkubwa dhidi ya wale walio madarakani ili wasidhulumu au kukandamiza haki za raia. Pili, watawala wasikubaliwe kutenda chochote ambacho hakiko katika sheria.

Mwaka 1765, Lord Camden ambaye alikuwa Jaji Mkuu wa Uingereza alisema, “lf it is the law, it will be found in our books. If it is not to be found there, it is not law.”

Kwa maneno rahisi ni kwamba Jaji Camden anasema “lwapo jambo ni sheria, litaonekana kwenye vitabu vya sheria. Endapo halimo vitabuni (matamko ya kisiasa), basi hiyo sio sheria.”

Tulipopiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano kwa vyama vya siasa vilivyosajiliwa kisheria kufanya siasa, tulipaswa kutazama kama suala hilo limo ndani ya vitabu vya sheria.

Kuna maamuzi yanayofanyika kwa kuwapendeza watu fulani, sheria inawekwa pembeni na siasa inachukua mkondo wa sheria.

Kwa vingine, maamuzi yanafanywa kwa woga kukidhi mahitaji ya kisiasa ya wakati husika, na sio kwa kuheshimu sheria ambayo haipindi haki wala wajibu. Tukienda hivi tunatikisa misingi ya utawala bora.

Tangazo la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948 kuhusu haki za binadamu linatahadharisha kwamba watu wanaweza kulazimika kuasi ili kupinga dhuluma, maonevu na ukandamizaji.

Hili linaweza kutokea tu pale ambapo utawala wa sheria haupo. Ni wazi kwamba utawala wa sheria unapotoweka, matokeo yake ni machafuko, fujo na maasi na pengine kupelekea vifo vya raia. Tusiilazimishe nchi kwenda huko.

Sisi kama taifa tunayo nafasi ya kujisahihisha kwa kuwataka mawaziri, wakuu wa mkoa na wilaya, kutoa matamko na maagizo yaliyo ndani ya sheria kwani hakuna mtu aliye juu ya sheria.

Vyombo vyetu vya dola navyo vifanye kazi yake ndani na chini ya sheria. Kwa madhumuni gani? Kwa madhumuni ya kulinda haki za wananchi ambao mara nyingi huitwa “wanyonge”.

Ndio maana nasema tusikubali wala kuruhusu misingi yetu ya utawala bora ikatikiswa kwa maslahi ya kisiasa, kwani tayari tunalo angalizo la UN la 1948. Aliye na macho haambiwi tazama.

0769600900

Advertisement