Mitalaa isiyoakisi mazingira tatizo vyuo vikuu

Dar es Salaam. Suala la mitalaa isiyoakisi mazingira ya Kitanzania kwenye elimu ya juu nchini limetajwa kuwa moja ya kikwazo kikuu cha kuporomoka kwa mchango wa wasomi kwenye maendeleo nchini kwa kuwa haiwajengi kuwa wabunifu.

Hayo yalibainishwa hivi karibuni katika mhadhara wa Kavazi la Mwalimu Nyerere uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Akihutubia mhadhara huo, msomi kutoka Chuo cha Jawaharlal Nehru cha nchini India, Profesa Prabhat Patnik alieleza mambo mbalimbali ambayo yamefanya elimu ya juu barani Afrika kupoteza malengo na kugeuka taasisi za biashara.

Alisema elimu ya juu inatakiwa kuzalisha wasomi ambao watakuwa chachu ya mabadiliko kwenye jamii kwa kuongeza ubunifu kwenye uzalishaji mali.

“Chuo hakiwezi kuwa kama nakala ya chuo kingine. Huwezi kuiga vyuo kama Havard na Oxford na ukatumia mfumo wake sehemu yoyote ile.

Dhana ya kwamba elimu ni moja si sahihi kwa sababu wao wameendelea kuliko sisi,” alisema.

Wasomi wa ndani walikubaliana na mtazamo huo akiwamo Jaji Joseph Warioba aliyesema kuna haja ya kuhuisha mfumo wa elimu ili uendane na mahitaji ya Taifa.

“Ni lazima tupambane na viashiria vyote vinavyohatarisha mustakabali wa elimu yetu maana hakuna namna nyingine “ alisema Warioba.

Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Slaam, Dk Ng’wanza Kamata alisema kushuka kwa ubora wa elimu, kunajidhihirisha hata kwenye ufanyaji wa utafiti vyuoni.

“Ukilinganisha Dissertation (tasnifu) ambayo imefanywa na mwanafunzi wa masters (shahada ya uzamili) wa leo na ya mwanafunzi wa shahada miaka ya 1970, utaona kuna tofauti kubwa, hazifanani hata kidogo,” alisema.

Masuala mbalimbali yalizungumzwa katika mhadhara huo uliojumuisha watu wa kada mbalimbali wakiwamo wasomi maarufu nchini.