Mjadala kuhusu taulo za kike ulivyowasha moto bungeni

Muktasari:

  • Baadhi ya watoto wa kike wamekuwa wakikosa masomo kwa ukosefu wa taulo hizo wanapoingia katika hedhi kwa kati ya siku tatu hadi tano.

Kushindwa kumudu kununua taulo za kike ni miongoni mwa changamoto ambazo zinamkabili mtoto wa kike nchini, hivyo kuchangiakwa kiasi kikubwa tatizo la utoro shuleni.

Baadhi ya watoto wa kike wamekuwa wakikosa masomo kwa ukosefu wa taulo hizo wanapoingia katika hedhi kwa kati ya siku tatu hadi tano.

Hata hivyo, zipo jitihada mbalimbali zinazofanywa na taasisi zisizo za kiserikali na baadhi ya wabunge bungeni kuitaka Serikali sasa ichukue jukumu la kuwasaidia wanafunzi wa kike taulo hizo ili kuwawezesha kuhudhuria masomo kikamilifu.

Katika mjadala huo wa bajeti za mwaka 2018/19 za wizara mbili ambazo ni Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee suala hilo lilijitokeza kwa wabunge wengi kutaka Serikali kuangalia jambo hilo kwa jicho la pekee ili kuwanusuru watoto wa kike.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Jasson Rwekiza anaitaka Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza au kuondoa kodi ya taulo za kike ili kuwawezesha watoto wa kike hasa kutoka familia masikini kumudu gharama za taulo hizo na kuweza kuhudhuria masomo kikamilifu.

“Mwaka 2008 utafiti uliofanywa na Unicef (Shirika la Kimataifa la

Kuhudumia Watoto) ilibaini kwamba asilimia 10 ya watoto wa kike katika shule za msingi na sekondari kusini mwa sahara (Sub Saharan Africa) huacha masomo kwa kushindwa kumudu gharama za taulo za kike,” anasema.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Angelina Malembeka anasema wapo baadhi ya wasichana wanaamua kujisitiri kwa majani na matambala mabovu ili mradi tu waende shule, lakini wapo ambao wanaamua kutokwenda shuleni na hivyo kuwafanya kukosa masomo na kupoteza mwelekeo.

“Kwanini ile mikoa ambayo inalima pamba nchini isitengeneze viwanda vidogovidogo ambavyo vitatengeneza pamba, angalau kuwawezesha wanafunzi hawa kujisitiri halafu ziuzwe kwa bei nafuu au ikiwezekana zitolewe bure ili waweze kushiriki vizuri masomo,” anasema.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Maria Kangoe ambaye anajitanabaisha kama championi wa hedhi salama, anasema hajisikii vizuri kama hataishauri Serikali juu la taulo za kike.

“Suala la hedhi salama tumekuwa tukilichukulia poa kwa sababu sio ugonjwa ndio kweli si ugonjwa, lakini tatizo la hedhi kutokuwa salama ni changamoto kubwa sana na limekuwa linasababisha magonjwa mengi mno,” anasema.

Anasema dawa nyingi za antibiotics wanazosambaza Serikali katika vituo vya afya na hospitali zimekuwa zikitumiwa na wanawake.

“Wanawake ambao wanatibiwa magonjwa ambayo yanatokana na ukosefu wa hedhi salama ni lazima tukubaliane Serikali iangalie namna ya kuweza kutoa nyenzo (taulo za kike) kwa wanawake na wasichana kutumia katika siku zao,” anasema.

Anasema anachomaanisha ni kwamba ni muhimu kutoa kinga kuliko kuacha magonjwa yatokee ndio watoe dawa, hivyo suala hilo ni muhimu sana Seriklai kuliangalia licha ya kwamba wanayo mambo mengi yakutekeleza.

“Tunaamini kabisa Serikali hii sikivu itaenda kujitafakari upya pamoja na kwamba ina mambo mengi tunaamini mnao wadau wengi ambao mnaweza mkawa-aproach wakaweza kuwasaidia katika hili. Lakini, wakati tunafikiria hili tuangalie namna ya kupunguza bei ya taulo hizi za kike kwa kuanzia na VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) kama zinaweza kufutwe,” anasema.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Sabrina Sungura anasema wapo baadhi ya wasichana wamefikia hatua ya kutumia kinyesi cha ng’ombe na wengine wameathirika kwa kuumwa kutokana na hedhi isiyo salama.

“Nampongeza mbunge (Maria) kwa sababu wasichana wetu wa vijijini wamefikia hatua mpaka wanatumia mavi ya ng’ombe wakati wa siku zao na wengine wameathirika mpaka wanaumwa,” anasema.

Mbunge wa Urambo (CCM), Magreth Sitta anasema licha ya kushindwa kuhudhuria masomo kwa wanafunzi wa kike kutokana na kukosa taulo za kike wengine wamekuwa wakiacha shule kabisa hasa wale wanaotokea familia duni.

“Suala hili ni muhimu sana. Ninaomba kwa taadhima na heshima Serikali kuangalia suala hili kwa undani na kuona jinsi gani ambavyo itaweza kumsaidia mtoto wa kike,” anasema.

Hata hivyo, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Munde Abdallah anatofautiana na wenzake kwa kutoliunga mkono suala hilo na kutaka Serikali iachwe kujikita katika kazi inazozifanya.

“Kumekuwa na mjadala wa kuiomba Serikali igawe taulo za kike bure kwa wanafunzi, mimi siungi mkono na sababu ninazo. Rais anafanya kazi kubwa anajenga barabara, anasomesha watoto bure, madawati bure sijui kila kitu bure, tunataka tupeleke na taulo bure,” anasema.

“ Kwa sasa bado nchi yetu haijafikia tuache Serikali ikite kwenye kazi inazofanya. Mimi siungi mkono naendelea kupinga na nitaendelea kupinga siku zote. Rais ameshatusomeshea watoto wetu bure na sisi kama wazazi tuwajibike, tuna sababu ya kuwajibika hatuwezi kutegemea kila kitu kiwe bure kwa Serikali,” anasema.

Anasema hata nchi ya Uingereza hawatoi taulo hizo za kike bure na kuhoji kwa nini Tanzania wanata zitolewe bure.

Mbunge mwingine ni Mussa Mbarouk (CUF-Tanga Mjini), anasema tayari Rais Uhuru Kenyata wa Kenya amesaini sheria kwamba wanafunzi wote wa kike nchini humo watakuwa wanapewa bure taulo hizo.

“Sasa mimi najiuliza ukitazama Kenya mbuga ninazozijua mimi ni Tsavo na Maasi Mara, lakini sisi tuna mbuga za wanyama, tuna Mlima Kilimanjaro Kenya hawana, tuna mkonge, katani, pamba, pareto, alizeti na mazao mengine, tuna bandari tatu, Kenya wana bandari moja tu wameweza kufanya hilo,” anasema.

Sakata la taulo za kike limeshaibuliwa mara kadhaa na Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Upendo Peneza ambaye karibu kila bajeti tangu aingie bungeni mwaka 2015 amekuwa akilisemea kwa kuitaka Serikali kutafuta njia ya kuwasaidia watoto hao bila mafanikio.

Upendo anasema inawezekana Serikali kulifanikisha hilo kwa kutenga fedha Sh46.7 bilioni ili kuwawezesha watoto wa kike kupata taulo za kike kwa ajili ya kujihifadhi.

Ingawa alishapeleka hoja binafsi kwa ajili ya kuishauri Serikali kutoa taulo hizo kwa wanafunzi nchini lakini haikufanikiwa kupenya, Upendo anasema bado nia yake iko palepale ya kuipeleka hoja hiyo bungeni.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Kakunda anasema kwa kutumia muongozo wa ruzuku za uendeshaji wa shule za sekondari wanaoelekeza kutumia asilimia 10 ya ruzuku kwa ajili ya dawa na mahitaji maalum kwa wanafunzi wa kike wawe na utaratibu wa kuwanunulia taulo wanafunzi hao maalum kwa utaratibu utakaoratibiwa na mkuu wa shule husika.