Mkapa alia na tatizo la vipaumbele kubadilika kila utawala mpya

Muktasari:

  • Tatizo la viongozi wa Afrika kwa mujibu wa Mkapa ni kwamba katika mabadiliko ya utawala kwenye awamu mbalimbali za uongozi, kumekuwa na tabia ya utawala mpya kuacha mipango iliyofanywa na utawala uliopita na kuamua kuunda mipango mingine mipya ya maendeleo. Alionya kwamba mabadiliko ya Afrika hayatatokea kwa mtindo wa kila utawala kuanza upya na kuacha yale mazuri yaliyofanywa na utawala uliotangulia.

Video ya Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa kuhusu tatizo sugu Afrika la utawala mpya kuachana na kila kitu kilichofanywa na uongozi uliotangulia, inasambaa kwenye mitandao ya kijamii. Inaonekana Watanzania walichelewa kuiona au kuipata.

Rais Mkapa alisema hayo Agosti 3, mwaka huu katika mkutano wa Jukwaa la Uongozi Afrika (African Leadership Forum), Kigali, Rwanda. Kongamano hilo lilipewa utambulisho; Financing Africa’s Transformation for Sustainable Development, yaani kufadhili mabadiliko ya Afrika kwa maendeleo endelevu.

Viongozi mbalimbali walitoa mchango wao, alikuwapo mwenyeji, Rais Paul Kagame, Rais wa Somalia, Hassan Mohamed, Katibu Mkuu wa Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa, Dk Mukhisa Kituyi na Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo.

Mkapa alijenga hoja kuhusu maendeleo ya Afrika, kwamba Afrika itaendelezwa na Waafrika wenyewe na siyo kuisubiri Marekani au Jumuiya ya Ulaya. Alisema ni wajibu wa Waafrika kuamua kuiendeleza Afrika au kubaki bila maendeleo. Alikosoa ukusanyaji kodi bila kuwawezesha wananchi.

Alisema wananchi lazima wawezeshwe ili wawe wazalishaji. Aligusia kwamba wakati wa uongozi wake alijitahidi kufikia sekta isiyo rasmi na kuirasimisha, kitu ambacho kiliwasaidia sana watu wa makundi husika. Aligusia suala la ubinafsishaji na ilivyoundwa taasisi maalumu ndani ya serikali ya kusaidia kurasimisha Sekta isiyo rasmi, na iliwasaidia.

Akasema suala hilo lingempeleka pale tatizo la Afrika lilipo, kwamba katika mabadiliko ya utawala katika awamu mbalimbali, kila tawala mpya unapoingia madarakani, iwe baada ya miaka mitano au miaka kumi, unaacha kila kitu kilichofanywa na uongozi uliotangulia.

Mkapa alitoa mfano wa kauli ya Rais wa Pili, Ali Hassan Mwinyi, kwamba “kila zama na kitabu chake”. Alisema pamoja na ukweli wa dhana hiyo, haimaanishi kitabu kilichopita hakina mambo ya msingi kwa kitabu unachoandika sasa. Alionya kuwa mabadiliko Afrika hayatatokea kwa mtindo wa kila utawala kuanza upya na kuacha mazuri yote ya uongozi uliotangulia.

Tuongeze uzani

Mkapa alizungumza jambo jema kabisa. Pengine aliamua kutoa nyongo kwa yale yaliyomkwaza baada ya mambo mazuri aliyoyaanzisha na kutarajia yangeendelezwa, kufa kifo kisicho na maelezo. Hata hivyo, hapa tuiongezee uzani kauli yake.

Wanasiasa wanapaswa kutambua kuwa Serikali hubaki moja. Mabadiliko hufanywa kwa viongozi lakini Serikali huwa inabaki ileile. Hili ni eneo ambalo wanasiasa hawana budi kuheshimu.

Uwepo wa Serikali hujengwa na misingi yake, vilevile huwa na nguzo zake zinazoishikilia. Mabadiliko ya kiutawala hayapaswi kusababisha nguzo zote zinazoishikilia Serikali zibomolewe au hata msingi wenyewe.

Chukua hii; Serikali ambayo inabadilika kila baada ya uchaguzi na kila baada ya utawala mmoja kwenda mwingine, hapo ni kama hakuna Serikali, bali nchi inaenda kulingana na matakwa ya mtawala aliyepo.

Serikali huonekana pale ambapo mtawala anaikuta Serikali, anaisoma mahali ilipofikia, anaendeleza yale mazuri, anaimarisha yenye udhaifu kisha maeneo anayoona yanahitaji marekebisho, anafuata mchakato wa kikatiba na kisheria kuyabadilisha.

Ni maelekezo ya kikatiba kwa Serikali kupitia Bunge kutungia sheria mabadiliko inayofanya. Hii msingi wake ni kuwa asije kutokea mtawala mpya akafanya vinginevyo au mtendaji kwa kiburi tu akaacha kutekeleza. Sheria zinatungwa ili kuyapa nguvu na uhalali mabadiliko yanayofanywa.

Ukomo wa mtawala mpya

Haina maana kuwa mtawala mpya hapaswi kufanya mabadiliko yoyote. Anaruhusiwa kufanya mabadiliko ambayo anakuwa ameyapa uhalali wa kisheria. Haamki asubuhi tu na kuagiza mambo fulani yaanze na mengine yakome.

Utawala mpya hukaribisha mawazo mapya ya kiuongozi lakini mawazo hayo hayawezi kuwa sera ya Serikali mpaka kwanza yachakatwe ndani ya Baraza la Mawaziri na kisha yapitishwe bungeni.

Hali ya nchi ilivyo ni kama kila mtawala huingia madarakani na watunga sera wapya, vilevile wabunge na mawaziri wote wapya, kiasi kwamba anafanya mabadiliko makubwa yenye kufukia juhudi za awamu zilizomtangulia pasipo kukutana na changamoto wala ukosoaji.

Hawatokei mawaziri waliokuwepo katika Baraza la Mawaziri lililotangulia kutetea uamuzi uliofanyika katika utawala uliotangulia. Wabunge hawasimami kuupigania uamuzi wao walioutungia sheria na watunga sera wanakaa kimya kabisa utadhani hawakuwepo.

Fikra za mtawala kuona kama anaanza upya ni kusema kabla yake hakukuwa na Serikali, wakati mwingine hata kama mhusika naye alikuwa miongoni mwao. Tuna bahati ya akuwa na marais ambao awali walikuwa kwenye baraza la mawaziri kwa muda mrefu. Mfano, Mkapa mwenyewe alikuwa ndani ya serikali ya awamu ya kwanza na ya pili, akaja Jakaya Kikwete na sasa Rais John Magufuli.

Wabunge nao hufumbia macho ni kuhalalisha mawazo hayo kana kwamba Serikali haikuwepo. Hiyo ni kashfa kubwa maana wabunge wanapaswa kujiuliza walikuwa wanafanya nini katika Serikali iliyopita ikiwa usimamizi wao wote unabatilishwa?

Tusome kwa mifano

Alichokilalamikia Mkapa kilimkasirisha pia Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, kwamba Serikali ya Rais Mwinyi, iliacha hata yale mazuri ambayo yalifanywa katika Serikali ya Awamu ya Kwanza.

Tafsiri hiyo ni kuwa Rais Mwinyi alianza upya baada ya Mwalimu Nyerere, ni kama ambavyo Mkapa aliingia na Serikali mpya, vivyo hivyo kwa aliyemfuatia, Jakaya Kikwete na Rais wa sasa, Dk John Magufuli. Kila mmoja kwa uwezo wake alijitahidi kuisimamisha Serikali ya maono yake.

Kila utawala mmoja unapopisha madarakani na kuingia mwingine, ule mpya haujali uwekezaji mkubwa ambao ulifanywa na mtangulizi wake. Hushindwa kuzingatia kuwa katika kila mpango, sera na sheria, maana yake fedha za wananchi zimetumika. Anabadilisha tu.

Hili lisemwe kuwa linaweza kutajwa kama kila aina ya kashfa za rushwa na ufisadi. Ukweli ambao hauzungumzwi ni kwamba ufisadi mkubwa ambao unatendeka serikalini ni matumizi makubwa ya fedha za umma katika utunzi wa sera, mipango, kuandaa miswada na utungaji wa sheria ambazo mwisho hazitekelezwi.

Wakati Mkapa anaondoka madarakani, aliacha Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (Mkukuta). Kalenda yake ya utekelezaji ilikuwa miaka mitano, yaani kuanzia mwaka 2005 mpaka 2010. Kwa mantiki hiyo, Mkukuta ulitakiwa kutekelezwa ndani ya muhula wote wa kwanza wa Rais Kikwete.

Oktoba 2004, Serikali ya Tanzania iliingia makubaliano na Serikali ya Norway, kuhusu kufanya mapitio ya biashara na rasilimali za wanyonge ili kuzifanya ziwe rasmi. Mapitio hayo ndiyo yaliyozaa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita).

Kuhusu Mkukuta, Mkapa alikaa na baraza lake katika ukumbi wa Karimjee, mtaalamu kutoka Peru, Jens Clausen, akawapiga msasa mawaziri kuhusu njia na mbinu sahihi za kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa mazingira ya Kitanzania.

Clausen pia ndiye alikuwa kiongozi wa timu ya wataalamu waliofanya mapitio ya rasilimali na biashara za Watanzania kisha kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuzirasimisha. Pitia miaka 10 ya Kikwete, huoni utekelezaji wa Mkukuta wala Mkurabita.

Dola za Marekani 7milioni ambazo kwa sarafu ya wakati huo zilikuwa takriban Sh9.1 bilioni, zilitumika kwa ajili ya Mkurabita peke yake. Kutotekelezwa kwa mapendekezo ya wataalamu kuhusu Mkurabita, maana yake fedha hizo zilitumika bila faida yoyote.

Matokeo Makubwa Sasa

Kuhakikisha kuwa Tanzania inaongeza mwendo kuelekea Malengo ya Milenia 2025, mwaka 2012 iliweka vipaumbele vinane na kuviweka kwenye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).

Vipaumbele hivyo vya BRN ni maji, elimu, nishati, afya, kilimo, uchukuzi, mazingira ya biashara na uhamasishaji wa rasilimali. Ifahamike kuwa BRN ilipatikana baada ya Serikali ya Awamu ya Nne kuwapa kazi watunga sera wataalamu kutoka Malaysia.

Baada ya Kikwete kuondoka madarakani, mapambio ya BRN yamekoma na kitengo kikafutwa. Rais Magufuli alikuwa kwenye Baraza la Mawaziri la JK, kama ambavyo JK alikuwa kwenye Baraza la Mawaziri la Mkapa. Magufuli anaifahamu maana kamili ya BRN kama ambavyo JK alijua kila kitu kuhusu Mkukuta na Mkurabita.

Katika kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia iliyopo Karne ya 21, Serikali iliandaa mpango wa kutengeneza walimu 8,000 wa masomo ya Sayansi. Mpango maalumu ulianzishwa na kupitishwa na Bunge wa kuchukua wanafunzi wanaofanya vizuri mitihani ya Sayansi kidato cha nne na kuwapa ruzuku ya asilimia 100 kisha kuwadahili Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Wanafunzi hao walidahiliwa kusoma diploma maalumu ya ualimu wa Sayansi na kupewa ruzuku ya asilimia 100 kutokana na ukweli kuwa ualimu si kipaumbele kwa wanafunzi wenye kufaulu kidato cha nne. Ruzuku hiyo ilitolewa kama kivutio cha wanafunzi kuacha ndoto zao na kufuata urahisi wa kusoma ualimu wa Sayansi.

Baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani posho maalum kwa wahadhiri waliokuwa wanawafundisha wanafunzi hao ilizuiliwa. Uamuzi huo ndiyo baadaye ukaibua ‘tamthiliya’ za wanafunzi zaidi ya 7,000 kuondolewa chuoni.

Mwisho asilimia 95 ya wanafunzi hao waliokuwa wanasoma Udom wamesambazwa kwenye vyuo vya ualimu vya kawaida. Hivyo, mpango wa diploma maalumu ya ualimu wa Sayansi umeshazikwa.

Kupuuzwa kwa BRN kulikofanywa katika Bajeti ya 2016-2017, kusingefanikiwa endapo Bunge lingethibitisha uwepo wake na kujitambua kwake kama mhimili huru unaoisimamia Serikali.

Mpango ambao umemeza fedha za nchi haupaswi kuachwa kisa tu utawala ni mpya, bali kinachotakiwa ni mtawala mpya kujenga hoja za kuufuta kisha kulishawishi Bunge nalo liridhie mapendekezo hayo.