Mkutano vyama vya kikomunisti na fursa lukuki kiuchumi nchini

Muktasari:

  • Mwaka huu Nchi ya China inatimiza miaka 40 ya kufanya Mageuzi na Kuchangamana Kimataifa na Mkutano huu wa Dar es Salaam utakuwa hatua kuelekea katika kongamano kubwa la ushirikiano wa China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation – FOCAC) litakalofanyika jijini Beijing, China.

“Tushirikiane kujenga jamii ambayo ina matarajio ya pamoja ya baadaye na kufanya kazi pamoja ili kujenga Dunia bora,” hayo ni maneno ya Rais wa China, Xi Jinping zilizopelekea majadiliano ya kidunia kati ya Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC) na vyama vingine vya siasa vya duniani.

Mwaka huu Nchi ya China inatimiza miaka 40 ya kufanya Mageuzi na Kuchangamana Kimataifa na Mkutano huu wa Dar es Salaam utakuwa hatua kuelekea katika kongamano kubwa la ushirikiano wa China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation – FOCAC) litakalofanyika jijini Beijing, China.

Kwa hiyo ni dhahiri kwamba Tanzania, Afrika na China katika mkutano huu watajikita katika mjadala mpana na wa kina wa kuziangazia changamoto na fursa lukuki zitokanazo na kujengeka zaidi kwa uhusiano na ushirikiano wa Afrika na China.

Mkutano huu unafanyika kwa mara ya kwanza katika historia ya Afrika, vyama vya siasa zaidi ya 38 kutoka washiriki zaidi ya 130 kutoka nje ya bara hilo watakutana nchini katika mkutano kidunia wa vyama hivyo.

Mkutano huo ulioandaliwa kwa ushirikiano wa CPC na CCM ni wa pili baada ya ule wa Beijing, China uliofanyika Desemba 2017.

Pamoja na mambo mengine, mada kuu itakayoongoza mkutano huo ni vitendo na nadharia za vyama vya siasa vya Afrika na CPC katika kufanya uchaguzi wa njia sahihi za kujiletea maendeleo na zinazoendana na mazingira halisi ya nchi za Afrika.

Fursa kiuchumi

Wakati wachambuzi wa masuala ya kisiasa wakiona fursa muhimu kiuchumi katika mkutano huo, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole anasema hiyo pia ni heshima kwa Tanzania na CCM kuwa mwenyeji wa mkutano huo. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Mwanza Kamata anasema mkutano huo ni fursa kwa Tanzania kujitangaza kiuchumi na kujifunza siasa za China zilizosaidia ukuaji wa uchumi wake.

“Ukweli ni kwamba siasa zikiwa mbovu uchumi hauwezi kukua, kwa hiyo hii ni fursa kwa Tanzania kujifunza aina ya siasa zilizotumika China ambazo licha ya kuwa ni za kijamaa, mafanikio yake ni makubwa. Hili ni taifa la pili kwa uchumi wa juu likiongozwa na Marekani,” anasema.

Dk Kamata anasema kisiasa Tanzania imekuwa ya mfano kwa kuwa imekuwa kwa amani licha ya kuwapo kwa mabadiliko ya kiutawala.

“Kuwa na amani hilo ni suala kubwa, kwa hiyo licha ya Tanzania kujifunza kutoka kwa China, mataifa mengine yanayo fursa ya kujifunza namna Tanzania, chini ya utawala wa CCM ilivyoimarisha na kudumisha amani hiyo,” anasisitiza.

Mhadhiri huyo anasema CCM ni chama kikongwe Afrika kwa hiyo kuna nafasi kubwa ya kuwaelimisha nchi nyingine zitambue utaratibu na michakato ya kisiasa kwa mataifa mengine kujifunza katika kujenga utulivu kisiasa.

Akizungumzia mkutano huo, Polepole anasema ni imani yao kwamba Tanzania itanufaika kwa muda mfupi wakati wa mkutano huo kwa kutoa huduma mbalimbali kwa wageni hawa, lakini pia itanufaika maradufu kwa matokeo ya mkutano huu na mwendelezo wake.

“Itakuwa fursa kubwa kwa Tanzania kukumbusha na kusisitiza msimamo wake katika diplomasia ya kisiasa na kiuchumi na hasa katika zama hizi za uongozi wa awamu ya tano ambayo imejikita kuleta maendeleo ya haraka kwa watu wake,” anasema.

Fursa ya kujitangaza

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Dk Jimson Sanga anasema mkutano huo ni wakati wa Tanzania kutumia nafasi hiyo kujitangaza kidunia.

“Huu ni mkutano wa kisiasa wa kidunia kwa hiyo, Tanzania inaweza kutangaza zaidi fursa zake za kiuchumi ikiwamo, sekta ya utalii,” anasema.

Dk Sanga anasema yapo mambo ambayo hata nje yanaweza kuwapo, lakini yale ya kitamaduni ndiyo ya msingi zaidi na yanapaswa kujulikana kidunia.

Kwa nini Tanzania

Polepole anasema CCM imechaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo baada ya CPC na Serikali ya China kuvutiwa na mwelekeo wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Magufuli.

“Mkutano huu ni sehemu ya matokeo mazuri ya utendaji kazi wa uongozi wa awamu ya tano ya chama na Serikali chini ya Rais Magufuli,” anasema.

Anaongeza kuwa tangu uongozi wa awamu ya tano umeingia umejikita katika kushughulika na shida za watu kwa kuimarisha nyanja zote za kiuchumi na kijamii.

Anasema mambo ambayo yamefanyika hadi kuvutia mkutano huo ni pamoja na kuimarisha nidhamu ya viongozi na watumishi wa umma, kuweka nidhamu katika makusanyo na matumizi ya fedha za umma, kuongeza uaminifu, uadilifu, uchapakazi, pamoja na mapambano dhidi ya rushwa, vitendo vya ubadhirifu wa mali za umma na uhujumu uchumi.

“Kwa hiyo mkutano huu wa Dar es Salaam utakuwa hatua kuelekea katika kongamano kubwa la ushirikiano wa China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation – FOCAC), litakalofanyika jijini Beijing, China,” anasema.

Wazo la mikutano

Polepole anasema wazo la mkutano huo linatokana na fikra za Katibu Mkuu wa CPC, Xi Jinping ambaye pia ni Rais wa China.

“Rais wa China anapendekeza fikra ya mwelekeo mpya wa namna tunaenenda kidunia akitaka tushirikiane kujenga jamii ambayo ina matarajio ya pamoja ya baadaye na kufanya kazi pamoja ili kujenga dunia bora,” anasema.

Anasema fikra hizo ndizo zilizoibua majadiliano ya kidunia kati ya CPC na vyama vya kisiasa duniani.

Wakati China inatimiza miaka 40 ya kufanya mageuzi na kuchangamana kimataifa, mkutano huo utajikita katika mjadala mpana na wa kina wa kuziangazia changamoto na fursa zitokanazo na kujengeka zaidi kwa mahusiano na ushirikiano.

“Jambo moja ambalo lina mfanano kati ya China na Tanzania, CCM na CPC ni itikadi ambayo inatoa mwelekeo wa sera za China na Tanzania, ambazo zinaamini katika itikadi ya ujamaa.

Nini kitajadiliwa hasa?

Baadhi ya mada ndogo zitakazojadiliwa katika mkutano huo, ni pamoja na majukumu ya kimaendeleo na chaguo la njia za kujiletea maendeleo kwa China na Afrika, fursa zilizopo na changamoto za ushirikiano kati ya Afrika na China na wajibu wa vyama vya siasa katika ujenzi wa maendeleo ya kitaifa na mashirikiano baina ya China na Afrika.

“Mada zote hizi zinalenga kutupa hamasa katika jitihada zetu Afrika na China kuchagua njia sahihi za kukua, kujiletea maendeleo, kupendekeza programu ya vyama vya siasa kwa kongamano la ushirikiano wa China na Afrika litakalofanyika Beijing,” anasema.

Pamoja na mambo mengine, hapana shaka kwamba hiki pia ni kielelezo kwamba China inaendelea kusimika mizizi yake Afrika na kuongeza wigo wa soko la bidhaa zake.