Mohamed Salah, naitizama Altare

Muktasari:

  • Tatizo alilolipata Neymar ni kuwa yeye hakuwa kwenye ushindani wa hao wawili hivyo pamoja na ubora wake, bado alitakiwa kumfanya mfalme wa Barcelona, Lionel Messi aweze kumnyanyasa Cristiano Ronaldo.

Aliwahi kuishi Neymar Jr kwenye kizazi alichokuwepo Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, lakini kulikuwa na tatizo moja tu daima nalo liliitwa Barcelona.

Tatizo alilolipata Neymar ni kuwa yeye hakuwa kwenye ushindani wa hao wawili hivyo pamoja na ubora wake, bado alitakiwa kumfanya mfalme wa Barcelona, Lionel Messi aweze kumnyanyasa Cristiano Ronaldo.

Moja ya sababu kubwa zilizomwondoa Neymar katika klabu ya Barcelona ilikuwa hata wakati ambao Messi alienda likizo ya makusudi dhidi ya Paris St Germain bado kazi kubwa ya Neymar katika maajabu yale ya ushindi wa mabao 6-1 haikuzungumzwa.

Neymar aliamini kuwa alikuwa mrithi sahihi wa kizazi hiki cha wanaume hawa wawili mpaka alipoona miaka 25 inafika na hakuna dalili yoyote ya kukabidhiwa kijiti. Hapa hata mamlaka za Brazil zilianza kunong’ona na bahati nzuri kwao ni mfalme kuliko hata Messi alivyokuwa kwa taifa lake la Argentina. Bahati mbaya nyingine kwa Neymar ilikuwa kuingia kwenye klabu ya Paris St Germain kwa mikogo na kumkuta kocha Unai Emery ambaye majina ya wachezaji yalimzidi nguvu.

Wakati dunia ikiwa katika bumbuwazi pasi na kufahamu yupo ambaye angekuwa binadamu anayeweza kuwapa tabu wanaume hawa wawili, kulikuwa na kikosi ambacho hakuna aliyekuwa anakidhania. Wakiwa wanaimba nyimbo yao ya You’ll Never Walk Alone kwa mwaka wa 27 pasipokuwa na kombe la ligi, klabu ya Liverpool ilikuwa imemsajili mchezaji mmoja mzuri wa kawaida anayeitwa Mohammed Salah.

Hakuna ambaye alishitushwa na usajili huu na wengi walifahamu kuwa alikuwa ameletwa kuongeza unyumbulifu na kasi kikosini hapo kwani funguo zote zilikuwa mikononi mwa Philippe Coutinho ambaye angeamua kila tukio muhimu la klabu hiyo ndani ya uwanja. Uwezekano wa Mohamed Salah kuwa mchezaji bora kwenye kikosi cha Liverpool kwa msimu huu ulikuwa mdogo kuliko ule wa Leicester City kutwaa ubingwa wa Ligi kuu ya England. Ilikuwa haifikiriki, haikuwa inaleta maana na wala haikuwa hoja kuwa angeweza kutikisa katika ligi pia katika dunia ya leo.

Katika ligi ambayo Romelu Lukaku alisajiliwa Manchester United, Alvaro Morata akitua Chelsea na uwepo wa Aguero, Harry Kane, Kevin De Bruyne na Eden Hazard ni mwendawazimu pekee ambaye angeweza kuliwaza jina la Mohamed Salah mbele hata ya Sadio Mane ambaye ndiye aliyekuwa mchezaji bora zaidi wa Liverpool kabla hajapata majeraha msimu wa 2016/2017. Ni maisha ndivyo yalivyo, mwenye suti huonekana na fedha kuliko mavazi ya jinzi mtaani.

Miezi sita baadaye tangu aingize mguu wake ndani ya uwanja wa Anfield, kuna kituo cha mawasiliano ambacho kilikuwa kinatoa vifurushi vya bure vyenye jina kila akifunga, migahawa iliyopo Liverpool ikawa inatoa chakula anachokipenda bure kwa wanaokuwepo mgahawani muda anaofunga bure. Kijakazi akageuka mfalme, dunia ikageuka na kila alichoshika kikageuka dhahabu. Akageuza kila jiwe alilolikuta katika klabu ya Liverpool na kusimika misingi yake ambayo inaweza kudumu kwa muda mrefu kabla hajajitokeza mwingine kuivunja.

Wakati akiwapa Liverpool sababu ya kupaza sauti mpaka nyikani, huku nyumbani raia wa Misri walipata sababu kubwa zaidi za kupiga magoti na kuabudu. Alifunga kila bao muhimu lililowapeleka kwenye michuano ya Kombe la Dunia inayofanyika Urusi. Amewaweka kwenye ramani ambayo wengi wao wamekwisharidhika na mchango wake bila kujali nini kitatokea kwa ujumla wa matokeo ya kundi A lenye timu za Uruguay, wenyeji Urusi, Saudi Arabia na Misri wenyewe.

Katika hili ndipo ambapo Mohamed Salah anaweza kuwa salama zaidi. Sababu ya kufanya vyema kwenye klabu ya Liverpool ilikuwa kucheza bila presha ya kutizamwa kama ilivyokuwa wengine na hakuna ambaye alimpa nafasi kubwa hata kwenye kikosi cha Liverpool. Pamoja na kuwa amejipatia jina kubwa hapa alipo kuna madhabahu takatifu zaidi kuliko zile alizotoka. Hapa ndipo Messi anajaribu kufunika ufanisi wa Cristiano Ronaldo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ronaldo akijaribu kuhakikisha inakuwa nafasi yake ya kutwaa Ballon D’Or ya sita na kuwa mwanadamu wa kwanza kufanya hivyo huku Neymar akitaka kuwakumbusha watu kuwa anaishi.

Kwenye hesabu hizi ngumu, kila mmoja anamtazama, Mohamed Salah atafanya jambo gani hili kuhalalisha uwepo wa jina lake na kukamilisha utatu mtakatifu wa mwaka huu kwa maana ya yeye, Lionel Messi pamoja na Cristiano Ronaldo. Kundi ilipo Misri sio gumu lakini lina changamoto ya kila timu kuamini inayo nafasi kubwa. Nafasi pekee ya upendeleo aliyokuwa nayo Mohamed Salah dhidi ya wengine wote ni ufinyu wa kikosi chake ukilinganisha na washindani wake.

Mohamed Salah hatakiwi kuifikisha timu yake nusu fainali ili ajisimikie jina kubwa zaidi kwa mwaka huu. Madhabahu yake itapigiwa kila goti iwapo akifanikiwa kufika japo robo fainali kwa juhudi zake za wazi. Bahati nzuri nyota yake inaonekana kung’ara zaidi kwa sababu anapendeka kwa wengi. Hana makuu, hazungumzi kupita kiasi na ni muumini mzuri. Kuna wengi wanaopewa nafasi ya kufika mbali kutokana na uimara wa vikosi vyao, lakini kwenye moyo wa Salah ni tofauti. Roho inaniambia utakuwa muendelezo wa mwaka wake mzuri.

Haya mambo huwa yanaenda na nyota, na Salah ameshika kasi msimu huu. Iwapo kama wataweza kujilinda vyema basi anao uwezo wa kuwa na madhara makubwa kwa sababu hata timu yake inampenda na inacheza ikimtizama yeye. Naitizama Altare ya kombe la dunia, ninapata kila hisia kuwa itabarikiwa na miguu yake. Atakuwa na msimu bora.