Msajili wa vyama asisitiza kutoa ruzuku kwa CUF ya Lipumba

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema ofisi yake itaendelea kutoa ruzuku kwa upande wa mwenyekiti wa CUF anayetambulika na ofisi hiyo, Profesa Ibrahim Lipumba akisema alipata maelekezo kutoka katika chama hicho.

Chama hicho kimekuwa kwenye mgogoro wa muda mrefu tangu Profesa Lipumba alipoamua kujitoa kwenye nafasi yake ya uongozi Julai 2015, akipinga chama hicho kushirikiana na Chadema iliyokuwa imemsimamisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kugombea urais.

Hata hivyo, Profesa Lipumba alirejea katika nafasi yake Agosti 2016 akisema kuwa barua yake ya kujiuzulu uenyekiti haikujibiwa, suala ambalo limezua mvutano na kuunda kambi mbili kati yake na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Awali ofisi ya msajili wa vyama vya siasa ilisitisha utoaji wa ruzuku kwa chama hicho, lakini baadaye ikaendelea kutoa kwa upande wa Profesa Lipumba ambao umemteua Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya kukaimu nafasi ya katibu mkuu. Katibu Mkuu wa CUF ambaye ni mtendaji mkuu ni Maalim Seif Sharif Hamad.

Akizungumza ofisini kwake hivi karibuni, Msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi alisema ameendelea kutoa ruzuku kwa kuwa alipata barua kutoka kwa upande huo.

Alipoulizwa madai ya akaunti inayotumika kuwekea ruzuku hiyo kutokuwa rasmi, Mutungi alisema, “Una uhakika gani? Muulizeni Mtatiro.”

Julius Mtatiro aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya uongozi wa CUF upande wa Maalim Seif, ameshaachana na chama hicho na kujiunga na CCM hivi karibuni.

Alipoulizwa kwa simu, Mtatiro alisema hawezi tena kuzungumzia mambo ya CUF kwa kuwa ameshakihama chama hicho.

“Mimi nilikuwa mwenyekiti wa kamati ya uongozi wa CUF, lakini sasa nimeshaondoka niko CCM, nilishasema sitaki kabisa mambo hayo,” alisema.

“Ukiniuliza mambo ya CCM nitakujibu, nilikuwa Ukonga na sasa natoka Liwale,” alisisitiza.

Awali akizungumzia malalamiko ya vyama vya siasa kuhusu kuzuiwa kufanya mikutano na maandamano, mwanasheria mwandamizi wa ofisi hiyo, Monica Mwailolo alisema kifungu cha haki za vyama katika sheria ya vyama vya siasa haitekelezwi na ofisi ya msajili wa vyama hivyo pekee, bali na idara nyingine.

“Hatuwezi kuwazuia polisi wanapokataza mikutano na maandamano kwa sababu hatuna investigative power (nguvu za upelelezi),” alisema Monica.

Akifafanua zaidi kuhusu mabadiliko ya sheria hiyo, Mwailolo alisema kwa sasa ofisi hiyo imeshakusanya maoni ya vyama vya siasa na yamepelekwa kwenye kamati maalumu kabla ya kupelekwa bungeni.

Uhai wa vyama vya siasa

Kuhusu uhai wa vyama visivyoshiriki uchaguzi, alisema licha ya baadhi ya vyama vya siasa kutoshiriki uchaguzi kwa muda mrefu, bado havijapoteza sifa ya kuwa na usajili wa kudumu.

“Ili chama kisipoteze sifa ya usajili wa kudumu ni kuendelea kutunza zile sifa zilizokifanya kisajiliwe. Tunajua malengo makuu ya chama cha siasa ni kushika dola, lakini ushiriki uchaguzi ni uamuzi wa chama,” alisema Mwailolo.

Hata hivyo, alisema, “Si kwamba vyama vidogo havishiriki uchaguzi, sisi huwa tunafuatilia hizo chaguzi, kwa mfano uchaguzi mdogo wa Buyungu vyama 10 vilishiriki kwa kuweka wagombea ubunge na vingine vikaweka wagombea udiwani katika kata mbalimbali nchini.”

Alisema Ofisi ya Msajili imekuwa ikifanya uhakiki mara kwa mara ikiwa pamoja na uhakiki wa mwaka 2016 ulioviondoa vyama vitatu vya ambavyo ni Chausta, APPT-Maendeleo na Jahazi Asili katika orodha ya vyama vyenye usajili wa kudumu.

“Septemba 19 hadi 20 tulifanya mkutano na vyama vya siasa uliohusu jinsi ya kuendesha vyama vya siasa kama taasisi. Wanasiasa walipotakiwa kutoa maoni, wengi walilalamika kutokuwa na fedha za kuendesha vyama,” alisema.

Alifafanua kuwa sheria imeweka utaratibu wa kupata ruzuku kuwa lazima vyama viwe na wawakilishi kama wabunge na madiwani, lakini hawazuiliwi kuwa na vyanzo vingine. Japo ni lazima waeleze vyanzo vya fedha hizo,” alisema.