Msemo wa ajali haina kinga utatuponza

Muktasari:

  • Watu wengine hufunga milango ya kulijadili suala hili ili watu wasizungumzie umuhimu wa kuchukua tahadhari kwa kuingiza imani ya kidini kwa kugongea msumari kuwa kila tukio ni rehema ya Mola na haliepukiki.

Kwa miaka nenda miaka rudi jamii nyingi duniani na hata hapa kwetu zimejipumbaza na msemo wa “Ajali haina kinga”, badala ya kuchukua tahadhari za kujikinga.

Watu wengine hufunga milango ya kulijadili suala hili ili watu wasizungumzie umuhimu wa kuchukua tahadhari kwa kuingiza imani ya kidini kwa kugongea msumari kuwa kila tukio ni rehema ya Mola na haliepukiki.

Linalostaajabisha ni kuona watu hawa hujifanya hawana habari ya mafunzo ya kidini yanayowataka waumini kuchukua hadhari za maafa yanayohatarisha au kupoteza maisha yao.

Huu mwenendo wa kuweka mbele imani ya ajali haina kinga na watu kufanya mambo ya kuhatarisha au kupoteza maisha yao au ya wenzao umeota mizizi Zanzibar.

Siku hizi kila siku unasikia habari za ajali kutokana na watu kuendesha vyombo kwa mwendo kasi hata kwenye maeneo hatari.

Ukifanya utafiti mdogo tu utaona madereva wa daladala hawajali sheria za usalama barabarani na wanaona wanaokwenda kwa miguu kama watu wanaowaudhi na abiria waliowapakia kama vile wamebeba mawe au vipolo vya nazi.

Wanaoendesha pikipiki hujifanya watu waliopoteza mishipa wa fahamu na wanaoendesha baiskeli hawaoni umuhimu wa kuwa na taa wanapokuwa barabarani usiku. Ninafarijika ninaposikia maofisa wa Idara ya Polisi ya Usalama Barabarani wanapoikumbusha jamii umuhimu wa kuwa waangalifu ili kuepusha ajali.

Lakini, matokeo yake huwa kama vile wanazungumza na ukuta au mti kwani hao wanaowataka kuwa waangalifu hawajali licha ya kila siku kusikia habari za ajali na watu kupoteza maisha au kukatwa mguu au kujeruhiwa vibaya na kuwa vilema.

Lilio baya zaidi ni kuona vijana wadogo, baadhi yao wa miaka kama 12 wakiendesha kwa mwendo wa kasi vyombo vya moto barabarani.

Hapa inafa tujiulize: Hivyo wazee wanaowapa watoto wao wadogo vyombo vya moto ni watu wenye akili timamu?

Huu sio mwendo sahihi wa mzee kuonyesha mapenzi kwa mtoto bali ni wa kumtafutia njia ya kuhatarisha maisha yake.

Wakati umefika kwa Kikosi cha Usalama Barabarani kutafuta njia za kukomesha mwendo huu, si kwa kuwakamata hawa watoto tu bali na wazee wao au wale wanaowapa hawa vyombo vya moto.

Sheria zetu za Usalama Barabarani zinahitaji kufanyiwa mapitio, hasa kwa sehemu inayohusu magari yanayobeba abiria kutokana na ongezeko kubwa la ajali zinazosababishwa na madereva wa daladala.

Wengi wa hawa madereva ni washika sukani tu na uamuzi wa kuondoka au kuegesha gari hutokana na maagizo ya kondakta.

Konda akigonga kuashiria dereva aondoke hufanya hivyo, bila ya kuangalia kama ipo gari nyuma yake inayopita au hapo alipoambiwa simama ni eneo salama.

Sidhani ni sahihi kumpa leseni ya kuendesha daladala mtu mwenye uzoefu wa chini ya miaka miwili au mitatu ya kuendesha gari kwa nidhamu na kwa kufuata sheria.

Katika nchi nyingi huoni kijana wa miaka 20, kama ilivyo Zanzibar, anapewa leseni ya kuendesha daladala ijapokuwa watu wenye umri huu wanaitwa watu wazima.

Sababu ya kufanya hivyo ni kwamba wengi wa vijana wa umri huu huwa bado wanazo akili za kitoto na hawajali usalama wanapokuwa barabarani.

Katika baadhi ya nchi mtu ambaye hajatimia umri wa miaka 25 na kwingine ikiwa hana familia, anabaki kuendesha gari binafsi au taksi na si mabasi.

Sheria hii, ijapokuwa wapo wanaoiona ni ya kibaguzi, imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali za barabarani na kunusuru maisha ya watu.

Kwa upande mwingine Kikosi cha Usalama Barabarani kinapaswa kujipanga vizuri kutokana na tabia ya baadhi ya askari wa kikosi hiki kusemekana hawasimamii vizuri sheria.

Hawa askari wachache wanalipaka matope Jeshi la Polisi na kupelekea baadhi ya wana jamii kuwapa askari wa Usalama Barabarani majina ya kila aina, kama watoza kodi barabarani au wachumia tumbo.

Eneo jingine linalofaa kuangaliwa kwa uzito wake ni la baadhi ya askari kujificha vichochoroni au maeneo yenye kona kungojea mtu afanye kosa wamkamate.

Tabia ya askari kujificha na kungojea kosa lifanyike na kumkamata aliyetenda kosa si sahihi. Tutafute njia za kuwafanya madereva waogope kufanya kosa kwa kuwaona askari barabarani na si kungojewa watende

Magari bila bima

Bima ina umuhimu mkubwa katika usafiri na hasa kwa kutilia maanani uwezekano wa chombo cha moto kupata ajali.

Lakini kwa Zanzibar hili suala la bima za magari halijumuishi zile za serikali kama vile ajali zinayaogopa na kuyakimbia gari hizi.

Mjumbe mmoja wa Baraza la Wawakilishi hivi karibuni aliuulizia swala hili na kuambiwa kwamba hata magari yote ya mawaziri yaliyokuwapo nje ya Baraza yalikuwa yamekatiwa bima kamili.

Mwakilishi huyo alitoka nje ya Baraza na kuangalia vioo vya magari ya mawaziri na kugundua hata gari la waziri aliyesema hivyo halikuwa na kipande cha kuonyesha ilikuwa imekatiwa bima.

Sina uhakika kama magari ya majaji ambao huwatia hatiani wanaoendesha magari ambayo hayakukatiwa bima nayo yamekatiwa bima.

Wakati umefika wa kuliangalia suala la watu kupoteza kwa wingi maisha yao barabarani kwa mapana na sio kunyoosheana vidole vya lawama au kutoa maelezo ya ubabaishaji.

“Sikusudii kuudhihaki msemo wa ajali haina kinga, lakini tukumbuke umuhimu pia wa msemo wa Amini uyaonayo, sio uyasikiayo.”

Tunayoyaona barabarani yanatisha. Tunastahili kuchukua hatua za kujikinga na hili janga linalotupotezea maisha ya mamia ya watu, wakiwemo vijana ambao hata chumvi haijakolea katika damu zao.

Kwa pamoja tuwajibike na kwa pamoja tuwawajibishe wasiojali maisha yao na ya wengine.