Muswada wa vyama umeongeza malalamiko ya sheria za nchi zinazopitishwa na Bunge la 11

Muktasari:

  • Vyama vya siasa 15 vimeungana kutoa tamko la kupinga muswada wa vyama vya siasa

Mjadala unaoendelea nchini kuhusiana na muswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa, umeibua hoja ya kwa nini miswada mingi imeendelea kuzua mijadala hata baada ya kupitishwa kuwa sheria kamili.

Bunge la 11 linaloongozwa na Spika Job Ndugai ndio linaloongoza kwa kulaumiwa kuhusiana na kupita kiurahisi miswada ya marekebisho ya sheria inayowasilishwa na Serikali na kupitishwa kwa kutumia wingi wa wabunge wa CCM ndani ya Bunge.

Pia, Bunge hilo limelaumiwa kwa upendeleo hasa kwa wabunge wa CCM na kushindwa kuisimamia Serikali ipasavyo.

Hata hivyo, Ndugai mwenye alijinasibu ndani ya Bunge hilo kwamba linaongoza kwa kuwa na wasomi wengi kuliko mabunge yaliyopita kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wasomi ambapo 29 ni wenye shahada za Uzamivu (PhD) na 159 wakiwa na shahada ya kwanza.

Takwimu za wasomi wa Ndugai zinaonyesha wenye PhD kwa CCM wako 27, Chadema mmoja na CUF mmoja. Wenye shahada ya kwanza CCM wako 114, CUF 14 na Chadema 31.

Pia, Ndugai ametamba asilimia 80 ya wabunge ni wenye umri wa kuanzia miaka 40 na kuendelea, kwa maana siyo Bunge a vijana kama inavyodaiwa bali limesheheni wabunge wazoefu.

Pamoja na sifa zilizotolewa na Ndugai bado haliwezi kukwepa lawama kwamba miswada mingi ya marekebisho ya sheria imelalamikiwa sana tangu mwanzo wake hadi inapopitishwa pia imeendelea kulalamikiwa.

Mfano, hivi karibuni Serikali iliwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa ambao pamoja na mambo mengine umeipa nguvu Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ikiwamo kufuta vyama hivyo.

Kuwasilishwa kwa muswada huo kumenyooshewa kidole na wadau wa siasa wakiuona kama ni kitanzi kwao na kuibua mjadala mkubwa.

“Muswada umejaa adhabu za kijinai na hivyo kufanya shughuli za vyama kuwa jinai wakati ni haki ya kikatiba,” anasema John Mrema, mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema,

Mrema alienda mbali zaidi na kusema kuwa muwada huo utatumia general statements (sentensi jumuishi) kama gender, social inclusion, pressure groups bila ya kuyapa tafsiri ya kisheria na kwamba unampa msajili (mamlaka) ya kutafsiri maneno hayo kama atakavyo.

Si sheria hiyo pekee inayolalamikiwa na wadau mbali nchini zipo takribani saba zilizopitishwa na Bunge ambazo zimeibua mjadala kutokana na baadhi ya vifungu vyake kuwa na walakini.

Sheria hizo ni pamoja na ya huduma ya habari, takwimu, mifuko ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2018, walimu, TLS na Epoke.

Katika sheria ya huduma ya habari iliyopitishwa na Bunge Novemba 5, 2016 na kusainiwa na Rais John Magufuli kuna kifungu kinamuhusisha mwandishi kwenye masuala ya uchochezi na inatamka kuwa anaweza kuwa na hatia kama ataandika taarifa za kashfa kuhusu marehemu.

Aidha, sheria hiyo inayotoa adhabu ya kifungo jela kwa mwandishi ambaye hatazingatia masharti ya vitambulisho na usajili, imelalamikiwa na wadau mbalimbali wakiwamo waandishi wenyewe.

Hata hivyo, aliyekuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Nape Nnauye aliwahi kunukuliwa akisema kuwa sheria hiyo ni nzuri kwani inalinda maslahi ya wanahabari kwa kuwataka waajiri kuwalipia matibabu lakini pia wawakatie bima ya kuwalinda na mazingira hatarishi ya kazi.

Kwa mujibu wa Nnauye, sheria hiyo pia inataja kuanzishwa kwa mfuko wa taaluma kwa ajili ya wanahabari utakaowawezesha kujiongeza kielimu ili kuwa na weledi kwenye kazi zao.

Sheria ya takwimu

Hii ni kati ya sheria zinazo lalamikiwa na wadau wa masuala ya takwimu wakisema marekebisho ya sheria ya taifa ya takwimu (NBS) kuomba kibali kabla ya kusambaza kwa umma ni kitanzi cha uhuru kwa watumiaji.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie alikaririwa akisema marekebisho hayo yataondoa uhuru kwa watu binafsi na taasisi katika kutafuta takwimu, kuchambua na kuelezea kwa jamii ili kusaidia kutoa taarifa kwa umma katika kusimamia jambo husika.

“Sheria hii itadhibiti watu wanaotafuta takwimu kutotoa

hadharani hadi wapate kibali. Wakienda kuomba kibali NBS (Ofisi ya Taifa ya Takwimu) kama takwimu zao zitaleta sintofahamu kwa umma hazitaweza kutolewa hadharani. Itaondoa uhuru wa taasisi kutafuta, kuchakata na kutoa hadharani,”.

Epoka

Hii ni Sheria ya makosa ya mtandaoni ya 2015 iliyotengenezwa kudhibiti vitendo vya uhalifu mtandaoni kama udanganyifu wa kifedha, wizi wa fedha zinazotumwa kwa simu, mashambulizi ya kiufundi kwa tovuti na utapeli, imekuwa ikitumika kushtaki watumiaji wa mitandao walioonekana kukosoa mienendo ya Rais au watu wengine katika nafasi nyeti pamoja na taasisi.

Sheria hii pia ni kati ya zilizolalamikiwa na wadau mbalimabli inaainisha uchapishaji wa habari za uongo kama kosa la kihalifu. Kanuni za Huduma za Utangazaji (Utangazaji wa Uchaguzi wa Vyama vya Siasa) wa 2015,

Sheria ya mifuko hifadhi ya kijamii

Nyingine ni sheria ya mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma ambayo inatoa fao la upotevu wa ajira.

Sheria hiyo ambayo imeanzisha mfuko huo wa PSSSF , ilisainiwa Februari 8, na imeanza baada ya kukamilika kwa mchakato wa kuvunjwa kwa mifuko ya PPF, GEPF, LAPF na PSPF kwa watumishi wa umma, huku kwa sekta binafsi ukibaki mfuko wa NSSF

Hata hivyo, mara baada ya kanuni za sheria hizo kutungwa mbunge wa Bunda Mjini Ester Bulaya (Chadema) alionyesha wasiwasi wake juu ya sintofahamu ya kikokotoo cha 1/580.

Bulaya ambaye ni waziri kivuli wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana, na Wenye Ulemavu mwishoni mwa wiki alizungumza na wanahabari kuhusu sintofahamu ya kikokotoo cha 1/580 kilichopo kwenye kanuni za sheria hiyo na kusema kuwa inaeleza kila mstaafu atakuwa akilipwa asilimia 25 ya mafao kwa mkupuo na asilimia 75 inayobaki atalipwa kidogokidogo kila mwisho wa mwezi kama mshahara.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Irene Isaka alitoa ufafanuzi akisema kuwa kinachoendelea katika mijadala mbalimbali ni upotoshaji kwa wanachama kwamba kuunganishwa kwa mifuko kulianza kutumika miaka minne iliyopita.

Tayari Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Agosti 21, 2018 imewasilisha maelezo kuhusu muswada wa sheria ya bodi ya kitaalamu ya walimu Tanzania katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Jijini Dodoma.

Muswada wa sheria hii uliozua mjadala unalenga kuanzisha bodi ya kitaalam ya walimu Tanzania itakayosimamia utaalamu wa ualimu nchini kwa walimu wote walio katika Utumishi wa Umma na Sekta Binafsi kuanzia walimu ngazi ya astashahada, stashahada na shahada.

Pamoja na mambo mengine, Bodi itakayoundwa kwa Sheria hiyo: itasajili, itaweka viwango vya ubora wa ualimu, itasimamia maadili na miiko ya ualimu ya kitaalamu, itafanya tafiti kuhusu masuala ya utaalam wa ualimu na kusimamia maendeleo ya utaalamu wa ualimu kwa ujumla.

Marekebisho ya sheria ya TLS

Kupitishwa kwa Sheria hii kumefanya Tundu Lissu kuwa mwanasiasa wa mwisho kuongoza TLS ambaye alishambuliwa kwa risasi, Septemba 7 mwaka 2017.

Sheria hiyo imelalamikiwa na wadau mbalimbali wakiwamo Chama Wanasheria nchini (TLS) kikipinga Marekebisho ya Sheria ya TLS yanayolenga kuwakataza watumishi wa Serikali na viongozi wa kisiasa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika chama hicho kikieleza kuwa marekebisho hayo yanawabagua wanachama.

Pamoja na mambo mengine marekebisho hayo yanalenga kuweka masharti ya kumtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuzipitisha kanuni zinazotungwa na chama kabla ya kuchapishwa. Pia, kanuni hizo zitachapishwa kwenye Gazeti la Serikali.

Chadema wazungumza

Mbunge wa Bunda mashariki Ester Bulaya alisema kwa sasa nchi imeingia katika utungwaji wa sheria zinazozingatia masilahi ya wachache.

“Ukiangalia sasa si sheria moja tu ambayo inalalamikiwa, watu wenye mamlaka hawajali tena masilahi ya nchi badala yake wanaweka mbele itikadi za vyama,” alisisitiza.

“Wabunge nao wakumbuke nao ni Watanzania, wasifikiri wanafanya kwa masilahi ya chama kumbe baadaye hata wao zitakuja kuwageuka hivyo viongozi wasiwe wabinafsi.”

ReplyForward