Mwakagenda awataka wananchi Mbeya kutofanya makosa

Muktasari:

  • Mwakagenda alitoa rai hiyo juzi wakati akimnadi mgombea udiwani wa Kata ya Iwambi jijini hapa, Elisha Mwandele katika mkutano wa kampeni uliofanyika ofisi ya Mtaa wa Ndeje 2-Iwambi. Jiji la Mbeya lina kata tatu zinazofanya uchaguzi huo ambazo Chadema zimeweka wagombea ambazo ni Iwambi, Nsalaga na Maanga.

Mbeya. Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, Sophia Mwakagenda (Chadema) amewataka wananchi wa kata zinazofanya uchaguzi mdogo wa marudio jijini Mbeya kutofanya makosa na badala yake wawachague wagombea wa Chadema ili kuendeleza nguvu ya pamoja kwani jiji hilo linaongozwa na Chadema.

Mwakagenda alitoa rai hiyo juzi wakati akimnadi mgombea udiwani wa Kata ya Iwambi jijini hapa, Elisha Mwandele katika mkutano wa kampeni uliofanyika ofisi ya Mtaa wa Ndeje 2-Iwambi. Jiji la Mbeya lina kata tatu zinazofanya uchaguzi huo ambazo Chadema zimeweka wagombea ambazo ni Iwambi, Nsalaga na Maanga.

Alisema Chadema ndio inaongoza Jiji la Mbeya kwani meya anatoka Chadema na mbunge pia ni wa chama hicho, hivyo itakuwa jambo la busara kwa wananchi wa Kata za Iwambi, Nsalaga na Maanga kutofanya makosa kwa kuchagua wagombea wa CCM.

“Ndugu zangu wana Iwambi msidanganyike leo hii tunafanya uchaguzi, lakini haya yote yanatokana na madiwani wetu tuliyowafukuza kutoonesha mchango wowote, kila tulipoleta fedha za miradi huku wao walikuwa hawafuatilii utekelezaji wake. Lakini, mwisho wakakosa nidhamu kabisa hivyo chama kikafanya uamuzi mgumu.”

“Leo hii tumewaletea Elisha Mwandele ambaye atasimamia Kata ya Iwambi tunataka mumchangue na kutofanya makosa ya kumrudisha Hamphrey Ngalawa ambaye anakuja kuwaomba kura kwa tiketi ya CCM,” alisisitiza.