Mwalimu aacha kushika chaki ajikita kuuza dagaa

Muktasari:

  • Maisha hutegemea zaidi jinsi muhusika anavyojishughulisha. Yanaweza kutegemea ajira au kwa kujiajiri…Mwalimu Fredy Mlay ni miongoni mwa watu wachache walioacha ajira zao serikalini na kuamua kujiajiri. Anatengeneza dagaa wanaovulia Ziwa Viktoria na kuwasafirisha mikoani.

Ubunifu katika biashara huongeza thamani, matamanio kwa wateja na utofauti wa bidhaa hata kama inauzwa na watu wengi katika eneo moja.

Jambo hilo humfanya muuzaji kujiamini katika anachokifanya kwa sababu mnunuaji anakuwa na kila sababu ya kuipenda bidhaa yake.

Mwalimu Fredy Mlay (35) ni muuza dagaa safi walioandaliwa vizuri ambao mtu anaweza kuwatumia bila kuwapika tena.

Anafanya biashara hiyo baada ya kuamua kuacha kuitumia stashahada yake ya ualimu wa shule za msingi (ODPE) kwa kuona kazi hiyo haitamlipa vile anavyohitaji.

Kuachana na ajira ambayo vijana wengi wangependa kuwa nayo kumempa msukumo wa kujikita katika ujasiriamali.

Mlay ambaye ni mkazi wa Musoma hununua dagaa wabichi kutoka kwa wavuvi na kuwatengeneza vizuri bila kugusa mchanga na kuzifungasha katika ujazo wa nusu kilo.

Anasema alianza kuifanya biashara hiyo Septemba 2016 baada ya kumaliza chuo akiwa na mtaji wa Sh70,000 uliomuwezesha kununua beseni moja la dagaa, vifungashio, kutengeneza nembo na kununua mafuta. “Baada ya hapo nilifungasha katika ujazo wa nusu kilo ambayo nauza kwa Sh2,000 kila kopo moja na nikapata Sh100,000,” anasema Mlay.

Anasema aliamua kuchagua biashara hiyo kwa sababu anaamini dagaa ni kitoweo rahisi kuanzia uandaaji wake, upatikanaji wa malighafi na zinadumu kwa muda mrefu bila kuharibika zikiwekwa sehemu salama. “Ni chakula cha watu wengi kuanzia wanafunzi wanaoishi hosteli mpaka maofisini. Zinauzika, zinaliwa na watu wa imani zote na haisumbui kupata soko,” anasema Mlay.

Kutokana na mabadiliko ya upatikanaji wake, anasema beseni moja la dagaa ziwani hulipata kwa kati ya Sh18,000 zikiwa nyingi na Sh25,000 zinapoadimika.

Miaka miwili tangu aanze biashara hiyo, anasema mtaji wake umekua hadi kufika Sh1 milioni na ana uwezo wa kuuza kuanzia mabeseni 10 hadi 20 kila wiki.

Anasema hivi sasa biashara yake imetanuka na kuanza kupatikana katika baadhi ya mikoa kupitia oda maalumu zinazotolewa na wateja wanaohitaji huku naye akijitahidi kufanya kila analoweza kuwavutia wateja wengi zaidi.

“Zamani tulikuwa tunasafirisha kwa basi ila baada ya Serikali kuwa wakali sasa hivi tunasafirisha kwa malori ya mizigo yanayoenda Dar na Arusha na tunaweza kuwafikia wateja wetu kwa wakati,” anasema Mlay.

Anasema wateja wake huwapata kupitia stika zilizobandikwa kwenye bidhaa zake zikiwa pamoja na namba yake ya simu ya mkononi na mitandao ya kijamii.

Kwa uzoefu alioupata, anasema sasa amekuwa muuzaji wa jumla akiwauzia wasambaji wa rejareja kwa bei ya punguzo pamoja na kuwasafirishia.

Ili kuwafikia wateja wengi zaidi hasa mikoani anasema anatafuta mawakala ili owe rahisi kutekeleza lengo alilonalo.

Kama yalivyo malengo ya wajasiriamali wengi, Mlay anawaza kufika mbali katika kile anachokifanya ili aweze kula matunda aliyoyatarajia baada ya kuachana na ualimu na kuamua kujikita katika biashara.

Anasema moja ya malengo yake ni kuwa mfanyabiashara mkubwa wa dagaa safi ndani na nje ya nchi mwenye uwezo wa kuajiri vijana wengi kwa ajili ya kuuza na kusambaza.

“Kwa sasa tupo sita tunasaidiana kufuata dagaa ziwani na kuwaandaa ili wasipate mchanga, kuwakaanga, kufungasha, kusafirisha na hapo kila mmoja analipwa kwa kazi aliyoifanya tunaachana,” anasema Mlay